Kaimu Mganga mkuu wa hospitali ya mkoa ya Mount Meru, alisema hadi jana jumla ya watu 19 walikuwa wamelazwa kutokana na vurugu hizo za maandamano na imebainika watu 16 wamepigwa risasi.
"Hapa tuna watu 19 wamelazwa wodi ya majeruhi na kati yao 16 wamepigwa risasi maeneo mbali mbali ya mwili huku wengine wakiwa wamejeruhiwa kwa vitu vingine"alisema Chande.
Taarifa ya Dk Chande inatofautina na ile ya Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha,Thobias Andengenye ambaye alisema watu waliojeruhiwa kwa risasi ni tisa tu.
Alisema hospitali hiyo pia hadi jana ilikuwa miili ya watu watatu waliofariki kwa kupigwa risasi mmoja Ismail Omar (40) akiwa amefariki jana asubuhi huku wengine wawili, Denis Shirima na Mwita Waitara walifikishwa hosipitalini hapo wakiwa wamefariki tayari.
Kati ya majeruhi hao 16, majeruhi wanne ndio wamefunguliwa kesi na jana walisomewa mashitaka ya kufanya mkusanyiko bila ya kibali wakiwa kitandani.
Mmoja ya majeruhi hao, Frank Joseph ambaye amelazwa hospitali hapo, alikutwa amepigwa risasi kiunoni na hali yake ilikuwa mbaya huku dereva wa gari la mbunge wa viti maalum Grace Kiwelu, Cyprian Mungure jana akielezwa kuwa yupo mahututi.
Hadi jana ilikuwa bado haijafahamika idadi kamili ya majeruhi katika vurugu hizo ambao wamelazwa hospitali nyingine za binafsi za Selian, St Thomas, KCMC na nyingine.
Mama mkwe wa ZCO Dar naye apigwa risasi
Wakati huo huo, Mama Mkwe wa Mkuu wa upelelezi wa kanda maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, juzi pia alipigwa risasi na kukimbizwa hospitali ya AICC na baadaye alihamishiwa hospitali ya dini ya Selian.
Alipigwa risasi kwenye paja na hali yake ilikuwa sio nzuri ambapo jana baadhi ya maofisa wa polisi walikuwa wakihaha kumsaidia kupata matibabu.
Slaa awatuliza Chadema
KATIBU mkuu wa Chadema, Dk Wilibroad Slaa jana aliwatuliza mamia ya wakazi wa jiji la Arusha , waliokuwa wamefurika nje ya viwanja vya mahakama Kuu Kanda ya Arusha kutokana na vurugu zilizotokea juzi huku akiwapongeza ,kwa kuwaunga mkono katika mkutano na maandamano ambayo hata hivyo yalisababisha vurugu kubwa zilizosababisha vifo vya watu watatu na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa.
Akihutubia umati wa wananchi nje ya uzio wa mahakama hiyo, Dk Slaa aliwataka wakazi wa Arusha, kutulia kwani ujumbe wao umefika huku chama hicho kikijiandaa kutoa tamko kutokana na vurugu zilizotokea.
"Ndugu zangu tunawashukuru sana kwa heshma kubwa ambayo mmetupa, lakini hapa tupo nje ya mahakama na tumeombwa kuwatuliza na naomba muheshimu eneo hili kwani lipo chini ya mahakama," alisema Dk Slaa.
Naye Mbunge wa jimbo la Arusha, Gobless Lema, aliwataka wakazi wa Arusha, kutambua kuwa walichokifanya ni mwanzo wa kudai haki zao na kamwe wasiogopo chochote.
"Ndugu zangu poleni kwa yaliyotokea lakini tulichokifanya ni mwanzo wa kudai haki za wanyonge, kudai taratibu za sheria za nchi kufuatwa,"alisema Lema.
Katika mkutano huo, mamia ya wananchi hao, walikuwa wakiomba kutolewa tamko juu ya watu waliouawa katika vurugu hizo na hatma ya tukio hilo.
"Tunaomba tuelezwe ndugu zetu waliouawa haki zao zitakuwaje...polisi wamevunja sheria na wametuonea sanam,"alisema mmoja wa wafuasi hao wa Chadema.
Kituko cha mzee Mtei mahakani
Muasisi wa Chadema, Edwin Mtei jana alifanya kituko cha aina yake mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya mkoa wa Arusha, Charles Magesa pale alipojitokeza kutaka kuwadhamini wafuasi wote wa chama hicho ambao walifikishwa mahakamani.
Mzee Mtei alifikia uamuzi huo, baada ya hakimu Magesa kuuliza wadhamini ambapo alisimama na kusema yeye anataka kuwadhamini wote lakini hata hivyo, alitakiwa na hakimu kudhamini mtu mmoja pekee.
Akiwa mbele ya mahakama hata hivyo, Mzee Mtei alisema anamdhamini, Freeman Mbowe lakini hata hivyo, alijikuta hana nyaraka muhimu na hivyo kutoa fursa kwa wafuasi wengine wa Chadema kuwadhamini watuhumiwa na wote walipata dhamana.
Comments
huu unyanyasaji hamuuoni? au kwasababu maslahi yetu yapo pazuri nchi hii inawaka moto ..