Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kamati ya Zitto yatengua maamuzi ya Waziri Maige

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imetengua maamuzi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ya kutaka wawekezaji wa mahoteli kwenye hifadhi za Taifa watozwe asilimia 10 ya kodi ya mapato.

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alisema kiasi hicho cha kodi ni kidogo na kinaitia Serikali hasara isiyokuwa ya lazima.  Kabwe ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema hayo wakati wa kupitia hesabu za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa). 

Alisema Tanapa ilipaswa kuingiza kiasi cha Sh21 bilioni ya mapato kwa mwaka, hii inatokana na kila mgeni anayefika kwenye hifadhi za Taifa kulipa kodi stahiki kwa Serikali.

 “Kwa mujibu wa Sheria za Bunge, ninatengua maamuzi ya waziri ya kutoza asilimia 10 ya mapato kwa wawekezaji wa mahoteli kwenye hifadhi za taifa, badala yake nataka watozwe dola 10 hadi 50 kama ilivyopendekezwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Tanapa,” alisema Zitto.

Alisema Tanapa inatakiwa kubadili utaratibu wa utozaji wa kodi hiyo na kuwasilisha taarifa zao kabla ya kikao cha Bunge cha Juni, mwaka huu ili wajumbe wa kamati hiyo waipitie mapema na kujiridhisha.  Alisema Bodi ya Tanapa imetakiwa kuwasilisha taarifa utenguzi wa maamuzi hayo kwa Waziri mwenye dhamana ili atambue na kuthibitisha kuridhishwa kwa maamuzi hayo kabla ya Kikao cha Bunge cha mwezi ujao.

“Tunamtaka Waziri kudhibitisha kuridhishwa na maamuzi ya kamati kabla ya Kikao cha Bunge kijacho na kwamba kama atakataa maamuzi haya, lazima aandae majibu kwenye kikao kijacho cha Bunge, kwa sababu hana mamlaka ya kuwapunguzia kodi wawekezaji hawa,” alisema.

Alisema hatua ya Waziri Maige inakwenda kinyume na sheria kwani hana mamlaka yoyote ya kuizuia bodi ya wakurugenzi kufanya maamuzi ya kuongeza mapato ya kodi ya shirika hilo na kusisitiza kuwa kitendo hicho ni sawa na kuwabeba wawekezaji hao kinyume na taratibu.  Alisema kamati imeridhishwa na matumizi ya fedha kwa kipindi cha mwaka 2009/10 ambayo imepitishwa na Bodi ya Tanapa.

Mkurugenzi wa Tanapa, Edward Kisha alisema shirika lake lilipendekeza wawekezaji hao kutozwa kiasi cha dola 10 hadi 50 ili kuongeza mapato kwa Taifa ili kuliwezesha lijiendeshe bila hasara. “Bodi ya Tanapa ilipendekeza wawekezaji hao kulipa kiasi cha dola 10 hadi 50, lengo ni kuongeza mapato kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii na kwamba Serikali inaweza kuingiza mapato kupitia utalii,” alisema Kisha.

Alisema wakati kamati ya bodi hiyo ikifanya marekebisho ya kuongeza kodi kwa wawekezaji hao, Chama cha Wawekezaji wa kwenye Mahoteli kiliwasilisha barua ya malalamiko ya kupinga ongezeko hilo kwa waziri ambaye aliamua kuwapunguzia kodi hiyo.

 Hata hivyo, kamati hiyo imeitaka bodi hiyo kufanyia kazi baadhi ya kasoro zilizojitokeza hasa suala zima la kufuata utaratibu wa sheria ya ununuzi wa mali za shirika, kurekebisha utaratibu wa mfumo wa bima kwa wafanyakazi wake.

Tags:

0 comments

Post a Comment