Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Baraza kuijadili Chadema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KATIKA jitihada za kuhakikisha amani nchini inadumu, Baraza la Vyama vya Siasa, litakutana mwishoni mwa wiki hii kujadili hali ya kisiasa pamoja na nidhamu ya vyama hivyo.

Kwa mujibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, mkutano huo utajadili
mambo mbalimbali likiwamo la Chadema kutumia mikutano ya hadhara tofauti na inavyotakiwa ikitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Serikali.

Tendwa alisema ofisini kwake Dar es Salaam jana kuwa suala la Chadema limeonekana
kutishia amani ya nchi na kwamba linapaswa kujadiliwa na Baraza hilo.

“Mkutano huu ni wa kawaida na utakuwa wa kwanza mwaka huu, tutajadili masuala mbalimbali kuhusu hali ya siasa nchini, uhusiano wa vyama vya siasa na nidhamu za vyama kwa jumla.

Vile vile tutajadili suala la viongozi wa Chadema kutumia mikutano ya hadhara kutoa matamshi ya uchochezi yanayotishia amani ya nchi kwa kuwa si sahihi na hatutaki hali hiyo iendelee.

Alisema, huenda Baraza hilo likakutana keshokutwa kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote
na litakuwa la wazi kwa waandishi wa habari.

“Hakutakuwa na usiri katika mkutano wetu, hivyo waandishi wa habari wanaweza kuhudhuria,” Tendwa alisema bila kueleza mahali mkutano huo utakapofanyika na kusisitiza
kuwa taarifa itatolewa kwa vyombo hivyo.

Hivi karibuni, viongozi wa Chadema walikaririwa na vyombo vya habari wakitoa kauli zenye
kuchochea Watanzania waichukie Serikali iliyoko madarakani kwa madai kuwa imeshindwa kumaliza matatizo ya wananchi.

Mbali na kuzunguka katika mikoa mbalimbali nchini kueneza kauli hizo za uchochezi zinazodaiwa kutishia amani ya nchi, viongozi hao walidaiwa kuvuka mipaka
kwa kumpa Rais Jakaya Kikwete siku tisa za kutatua matatizo ya wananchi, jambo linaloelezwa kuwa si sahihi wala la busara.

Hata hivyo, Msajili alikemea matumizi hayo mabaya ya haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, yaliyooneshwa na viongozi hao wa Chadema na kuamua kulibeba suala hilo kwenye Baraza kwa ajili ya kujadiliwa zaidi.

Kadhalika, Rais Kikwete naye alilizungumzia suala hilo katika hotuba yake ya kila mwisho wa
mwezi kwa umma, na kulikemea vikali huku akihadharisha kuwa linaweza kuchochea chuki na umwagaji damu usio wa lazima.
Tags:

0 comments

Post a Comment