Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Posho ya chakula, malazi vyuoni kuongezwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
LICHA ya hali kuendelea kuwa ya utata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Serikali imekubali kuwapandishia posho ya chakula na malazi wanafunzi wote wa vyuo vikuu nchini, lakini watalazimika kusubiri hadi bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Msimamo huo wa Serikali ulitolewa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, ambaye alikwenda chuoni hapo kutoa msimamo wa Serikali baada ya wanafunzi hao kugoma kuanzia Ijumaa iliyopita.

Hata hivyo, kauli yake hiyo iliongeza jazba kwa wanafunzi hao, ambao mara baada ya Waziri kuwahutubia, waliwashambulia polisi kwa mawe na chupa za maji.

Kitendo hicho kiliwafanya polisi kuwatawanya kwa mabomu ya kutoa machozi huku baadhi ya wanafunzi wakikamatwa na wengine wakiumizwa kutokana na purukushani za kukimbia kipigo hicho cha polisi.

Wanafunzi hao wanadai kuongezwa posho kwa asilimia 100 kutoka Sh 5,000 wanayokopeshwa na Serikali hadi Sh 10,000 kwa kile wanachodai kuwa ni gharama za maisha kuongezeka, hali inayowafanya waishi na kusoma kwa shida.

Madai mengine ni pamoja na kutaka kuachiwa kwa wanafunzi wenzao waliokamatwa Ijumaa iliyopita na pia walitaka kila mwanafunzi apewe Sh 100,000 wakati wakisubiri mikopo ya muhula wa pili.

Madai hayo yalitolewa na wawakilishi wa wanafunzi waliosimama mbele ya Waziri kuzungumzia shida yao; na ndipo Waziri alipojibu hoja hizo, likiwamo la kuwaambia kuwa madai yao ya kuongezwa posho yamekubaliwa na Serikali. Majibu hayo yaliwafanya wanafunzi hao kuhoji, “Twambie ni kiasi gani na lini?”

Ndipo Dk Kawambwa akawaambia hajui itakuwa ni kiasi gani, kwani Hazina ndiyo itakayotoa majibu baada ya kupiga hesabu na kusomwa kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Hata hivyo, majibu ya Dk Kawambwa hayakuwaridhisha wanafunzi hao, ambao kabla ya kuanza hotuba yake, walimhadharisha aepuke kuzungumza siasa badala yake atoe majibu juu ya matatizo yao.

Akijibu hilo la posho, Dk Kawambwa alisema: “Kwa kuwa mnataka nisiseme siasa hapa nami nawaambia Serikali imekubali kupandisha posho hiyo, lakini si sasa hivi tusubiri bajeti.” Wanafunzi walijibu, “mbona Dowans haina bajeti na mnaharakisha kuilipa? Yaani sisi madai yetu ndiyo yasubiri bajeti tutaishije?

Walipaza sauti wanafunzi hao na kumtaka Waziri ashuke kwa walichodai kuwa hakuwa na majibu ya matatizo yao.

Hata hivyo, Dk Kawambwa aliendelea kutoa majibu ya suala la kutaka wapewe Sh 100,000 kila mwanafunzi wakati wakisubiri mkopo wa muhula wa pili, alipowaambia kuwa Serikali haina kiasi hicho cha fedha za kutosheleza wanafunzi zaidi ya 94, 000 ambao wanasoma vyuo vikuu nchini.

“Hapa nazungumza na wanafunzi wa vyuo vyote, idadi hiyo ya wanafunzi ni kubwa kupewa kiasi hicho cha fedha leo, haiwezekani,” alijibu Dk Kawambwa na kuitikiwa na sauti za wanafunzi kwa kelele za “uwiiiiiiiiiiii … uwiiiii!” Dk Kawambwa aliendelea:

“Ukweli ndio huo, hapa sizungumzi siasa kama mlivyonitaka.” Ndipo wanafunzi nao wakadakia kwa wimbo “Mashangingi yauzwe, mashangingi yauzwe, tupewe fedha za kujikimu.”

Kuhusu madai ya tatu ya kuachiwa wenzao bila masharti, Waziri Kawambwa alisema wanafunzi hao wameachiwa kwa dhamana, hoja ambayo wanafunzi hao pia waliipinga kuwa iweje waachiwe kwa dhamana wakati hawana makosa!

“Kwa nini waachiwe kwa dhamana? Mbona mafisadi wako huru bila dhamana … tunataka kesi ifutwe,” walipaza sauti wanafunzi hao na kujibiwa na Dk. Kawambwa, “Ile ni Mahakama na ni mhimili mwingine wa Dola, sina uwezo wa kuamrisha waachiwe huru.”

Kwa ujumla mkutano baina ya Waziri na wanafunzi hao ulionekana kama haukukidhi walichokuwa wanakitaka wanafunzi hao, na baada ya Waziri kuondoka, waliwazomea polisi na kuwatupia chupa na polisi kujibu kwa mabomu ya kutoa machozi.

Madai ya wanafunzi hao yalianza Ijumaa iliyopita baada ya kuandamana; lakini Polisi ikatawanya maandamano hayo na tangu siku hiyo baadhi ya mawaziri akiwamo Dk. Kawambwa na Shamsi Vuai Nahodha ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani wamekuwa wakifanya vikao na viongozi wa wanafunzi wa chuo hicho, ili kupata muafaka wa malalamiko yao.

Hata hivyo, wanafunzi hao waliahidi kuendelea na madai yao katika njia wanazozijua wao kwa kile wanachodai kuwa maisha yanaendelea kuwa magumu na hawawezi kuishi kwa Sh 5,000 kwa siku.

Juzi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama hicho aliwahadharisha wananchi kuacha kuingia katika migogoro na migomo na badala yake kutumia njia za kistaarabu kuwasilisha malalamiko na madai yao.
Tags:

0 comments

Post a Comment