Kutoka kushoto ni Jaffer Amin, Vincent Nyerere, Madaraka Nyerere & Maalim |
MBUNGE wa Musoma, Vincent Nyerere (CHADEMA), ametoa siku 30 kwa mmiliki wa kiwanda cha nguo cha Mutex kuhakikisha awe ameondoka iwapo atashindwa kuzalisha mali kiwandani hapo.
Pamoja na hayo, mbunge huyo pia ametoa siku kama hizo kwa mtumishi wa Manispaa ya Musoma, aliyetajwa kwa jina la Ruchungura ambaye anadaiwa kujimilikisha bustani ya manispaa hiyo kinyume cha sheria, kuirejesha haraka vinginevyo atachukuliwa hatua za kisheri.
Akizungumza juzi na umati mkubwa wa watu waliofurika katika viwanja vya Shule ya Mkendo mjini Musoma, Nyerere alisema mmiliki wa kiwanda hicho ameonekana kushindwa kusimamia uzalishaji, badala yake kiwanda hicho amekigeuza kuwa ghala la kuhifadhia vitu, hivyo anapaswa aondoke haraka vinginevyo ataondolewa kwa nguvu ya umma.
Alisema kutokana na kusuasua kwa uzalishaji huo, awali mwekezaji huyo alianza kutiririsha uchafu wenye kemikali yenye sumu, jambo ambalo lilimlazimu mbunge huyo kuagiza kufungwa kwa kiwanda hicho.
“Natoa siku 30 kwa huyu mwekezaji wa kiwanda cha nguo cha Mutex awe ameondoka iwapo atashindwa kuanza uzalishaji huo. Kwa hili nataka nikitoka bungeni Aprili nikute huyu jamaa mwekezaji ameondoka…vinginevyo tutamng’oa,” alisema mbunge Nyerere ambapo kauli yake iliungwa mkono na maelfu ya watu waliohuduria maandamano makubwa yaliyoitishwa na CHADEMA.
Kuhusu mtumishi wa Manispaa kujimilikisha bustani ya umma kisha kuweka biashara ya baa, Nyerere alisema kamwe hawezi kuvumilia mali za umma kuporwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao.
“Huyu mtumishi ameweka baa kwenye bustani yetu, nasema nikirudi bungeni awe ameondoka, la sivyo hatua za kisheria zitachukuwa,” alisema.
Mbunge huyo wa Musoma aliyekuwa akiongea kwa umakini mkubwa aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuunganisha nguvu zao kwa pamoja katika kuijenga Musoma mpya, na kwamba CHADEMA inahitaji kuona rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi wenyewe na si baadhi ya watu.
0 comments