Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mwanafunzi ajiua kwa kufukuzwa shule

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

•  ALIKUNYWA DAWA YA KUOSHEA MIFUGO


MWANAFUNZI mmoja wa Shule ya Sekondari Chamriho, iliyoko wilayani Bunda, mkoani Mara, Sira Giabe, amefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kunywa sumu baada ya kufukuzwa shule.
Giabe, ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne, alifukuzwa shuleni hapo kwa sababu ya utoro uliokithiri.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Robert Boaz, alisema kuwa alikunywa sumu Februari 9, mwaka huu.
Kamanda Boaz alisema baada ya mwanafunzi huyo kunywa sumu hiyo, alipelekwa katika zahanati ya Kijiji cha Mugeta, ambapo hali yake iliendelea kuwa mbaya, hivyo kulazimika kuhamishiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda kwa matibabu zaidi.
Alibainisha kuwa mwanafunzi huyo alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi akiwa amelazwa katika hospitali hiyo na upelelezi kuhusu tukio hilo bado unaendelea.
Daktari kiongozi wa Hospitali ya Bunda, Dk. Mathias Baruya, alithibitisha kifo cha mwanafunzi huyo, kwa kusema kuwa alikuwa amekunywa sumu aina ya Dip, ambayo hutumika kuogeshea mifugo.
Taarifa zaidi zinabainisha kuwa marehemu Giabe alichukua uamuzi wa kukatisha maisha yake kwa kunywa sumu baada ya kufukuzwa shuleni na mkuu wa shule hiyo, aitwaye Sassi Mugeta.
Kwa mujibu wa taarifa za watu walio karibu na marehemu huyo, zinadai kuwa tangu shule hiyo ilipofuguliwa Januari 10, mwaka huu, mwanafunzi huyo hakuwahi kuripoti shuleni hapo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyang’aranga alikokuwa anaishi mwanafunzi huyo, Soro Mabembere na diwani wa kata hiyo, Daniel Majani, walisema kuwa baada ya mwanafunzi huyo kufukuzwa shuleni, alifika nyumbani kwao na kuamua kunywa sumu hiyo.
“Baba yake mzazi aliniambia kuwa mtoto wake baada ya kwenda shuleni, mwalimu huyo alimfukuza kwa madai kuwa alikuwa mtoro, kwani tangu shule ilipofunguliwa hakuripoti.
“Sisi tulishangaa sana kufukuzwa kwa mtoto huyo, kwa sababu siku zilikuwa chache sana,” alisema Majani.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Chamriho, Sassi Mugeta, alipopigiwa simu kuzungumzia tukio hilo alitaka afuatwe shuleni na si vinginevyo.
Tags:

0 comments

Post a Comment