Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sumaye: Ufisadi janga la kitaifa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
AONYA HATARI YA MATABAKA, AHAMASISHA VIJANA NCHINI KUPAMBANA

WAZIRI Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Fredrick Sumaye, amewataka vijana kuwa na uzalendo wenye faida kwa kuhakikisha wanapiga vita rushwa na ufisadi ulio katika jamii kwa kile alichokieleza kuwa “ndio janga kubwa linalorudisha nyuma maendeleo ya taifa”.
Sumaye alitoa hamasa hiyo katika mahafali ya kidato cha sita ya Shule ya Sekondari Pugu jijini Dar es Salaam akisisitiza kwamba rushwa na ufisadi vilivyotamalaki katika jamii ni matunda ya ubinafsi wa watu wanaopenda kujilimbikizia mali kwa manufaa yao.
Kwa hiyo, aliwataka vijana kutokuwa wabinafsi na badala yake wajenge maadili mema ili kuwa na taifa la kizalendo ambalo wananchi wake hawapendi rushwa na ufisadi.
Akionekana kuzungumza kwa tahadhari kubwa Sumaye alionya kuwa ufisadi na rushwa katika nchi hujenga matabaka mawili: moja ni la wananchi wengi wasionacho na tabaka la pili ni la wachache walionacho ambalo limekuwa likiwanyima haki na fursa walio wengi katika kupata huduma za jamii.
Alisema utajiri wa nchi ukijikusanya kwa wachache ni hatari kwa taifa kwani kundi hilo kubwa la wanyonge linaweza kuingia katika mgogoro mkubwa wa kudai haki yake.
“Ufisadi na rushwa ni janga katika nchi zinazoendelea ndio maana haziwezi kuondokana na umaskini kwa sababu ndani yake kuna tabaka la wachache linalonyonya nguvu ya wenzao walio wengi,” alisema.
Alisisitiza ni lazima ukuaji wa uchumi uonekane katika mabadiliko chanya kitaifa kwa kuwa na vijana wazalendo wanaojali maslahi ya nchi yao.
Aliendelea kusema vijana wanatakiwa kujitoa kwa jamii katika kufanya kazi kwa ajili ya kusaidia wanyonge katika kupata huduma mbalimbali za kijamii.
Alisema umaskini, ufisadi, magonjwa kama ukimwi na rushwa ni matatizo yanayowakumba vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa katika uzalishaji.
“Naamini kuwa elimu ni karakana ya maisha kwa kujipanga katika maisha ya baadaye hivyo kupanga kufanya ufisadi na rushwa si matarajio ya shule. Elimu yenu mliyoipata muitumie katika ujenzi wa taifa….msipofanya hivyo mtakuwa wasaliti,” alisema.
Nchi zenye maendeleo ziliweka misingi bora katika masomo ya sayansi hivyo ni vyema vijana kuongeza juhudi katika masomo hayo.
“Naamini kuwa ni vizuri kuwa na umuhimu lakini ni muhimu zaidi kuwa vizuri,” alimalizia Sumaye.
Tags:

0 comments

Post a Comment