IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amekiri kupata taarifa za tuhuma zinazowahusisha maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini kuwahonga baadhi ya wabunge katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa lengo la kutaka urahisi wa kupitishwa kwa bajeti yake.Pinda aliliambia Mwananchi kwa simu jana kuwa “……niseme kwamba jambo hilo nimesikia likizungumzwa, zungumzwa pale bungeni, lakini si kwamba lililetwa rasmi kwangu kwa maana ya kulishughulikia”.
Jana gazeti hili lilichapisha habari kuhusu tuhuma dhidi ya maofisa hao, huku kukiwa na taarifa za Waziri Mkuu, Pinda kufikishiwa taarifa hizo na kuahidi kwamba angelishughulikia baada ya kuwa amewasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Waziri Ngeleja alipohojiwa juzi kuhusiana na tuhuma hizo, hakukubali wala kukanusha na badala yake alisisitiza kwamba anayeweza kuzizungumzia ni mwenyekiti wa kamati akimaanisha January.
Mwingine ambaye alitajwa kuarifiwa kuhusu wabunge hao kuhongwa ni Spika wa Bunge, Anne Makinda na kwamba kamati ya uongozi ya bunge anayoiongoza pia ilikuwa imeishapewa taarifa husika.
Hata hivyo Makinda aliliambia Mwananchi juzi kwamba hakuwa na taarifa za tuhuma hizo. "Mimi ndiyo nazisikia kutoka kwako, pengine kama zimeletwa kwa barua sijaiona, lakini sifahamu kitu kama hicho," alisema Makinda alipozungumza kwa simu na Mwananchi.
Habari zilizolifikia Mwananchi zilidai kwamba, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, January Makamba ndiye aliyewashtaki wajumbe wa kamati yake kwa Spika huku akiwachongea watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini kwa Pinda kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Lakini jana Pinda alisema, tuhuma kwamba baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walihongwa alizisikia na kwamba suala hilo ni kama liliachwa mikononi mwa kamati za bunge na uongozi wa bunge kwa ujumla ili liweze kushughulikiwa.
“Jambo kubwa ni kwamba hizi tuhuma zinapotolewa mara nyingi huwa kama rumors (uvumi) hivi na mimi kama Waziri Mkuu ni vigumu kushughulikia uvumi, inapofikia hapo unawaachia kwanza wahusika walishughulikie,” alisema Pinda.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, mbali na kusikia jambo hilo likizungumzwa katika vikao bungeni (japokuwa hakutaja vikao hivyo) hakuna taarifa rasmi wala malalamiko ambayo amekwishapelekewa ili ayashughulikie katika nafasi yake.
“Sina taarifa yoyote ya maandishi, maana ili niweze kuact (kuchukua hatua) lazima kuwepo na malalamiko rasmi, kwamba mtu analalamikia jambo hilo halafu mimi nalifanyia kazi, lakini katika mazingira ya sasa hakuna taarifa yoyote zaidi ya maelezo hayo niliyokupa,”alisema Pinda.
Hata hivyo Waziri Mkuu huyo alisema pale malalamiko ya rushwa yanapokuwa na ukweli ndani yake suala la msingi ni kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
Alipoulizwa kwamba hatua ya maofisa kutoa rushwa kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini huenda imetokana na woga wa kukwama kwa bajeti yao, Pinda alijibu:
“Hiyo haiwezi kuwa excuse (utetezi) kwani rushwa ni rushwa tu, ndiyo maana mimi nasema kwamba kama kuna ushahidi upo basi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika na vyombo vya kuchukua hatua vipo.
Kashfa hiyo imeikumba wizara hiyo katika kipindi kigumu ambacho nchi iko gizani huku watendaji wake wakilaumiwa kutokana na uhaba wa nishati ya umeme, huku Waziri Ngeleja akitangaza hali hiyo kuwa ni “janga la kitaifa”.
Kwa ujumla wabunge wengi wamekuwa wakieleza wazi kutofurahishwa na kile wanachodai kwamba ni ulegevu katika wizara hiyo na kuna taarifa kwamba huenda Waziri Ngeleja akapata wakati mgumu atakapowasilisha bajeti ya wizara yake bungeni.
Wizara ya Nishati na Madini inatarajiwa kuwasilisha makadirio ya matumizi bungeni Agost 19 na bajeti hiyo itajadiliwa na kuhitimishwa Agosti 20, mwaka huu.
Miongoni mwa mambo ambayo yamepata upinzani kutoka ndani ya Kamati ya Nishati na Madini pamoja na wabunge wengine wa CCM ni mapendekezo ya wizara hiyo kutaka kujenga makao yake makuu jijini Dar es Salaam kinyume cha ilani ya CCM ambayo inaweka wazi kwamba hakutakuwa na ujenzi wa makao makuu ya wizara jijini humo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Rushwa kwa mafungu
Habari ambazo Mwananchi lilizaipata jana zinadai kuwa, si wabunge wote ambao ni wajumbe wa walipewa fedha hizo za hongo na kwamba kulikuwa na walengwa ambao walitakiwa kudhibiti kile kilichoelezwa kuwa ni ‘kasi’ ya mwenyekiti, January.
Mmoja wa maofisa wa bunge (jina tunalihifadhi) alidai kuwa mpango wa kufikisha bahasha za hongo kwa baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo uliandaliwa kwa siri, hasa baada ya kubaini kwamba January alikuwa na msimamo wa kutaka maelezo ya wizara kabla kamati yake kubariki mapendekezo ya bajeti ya wizara.
Habari zaidi zinasema hicho ndicho chanzo cha mwenyekiti huyo ambaye ni mbunge wa Bumbuli, kuitisha kikao cha kamati yake na kugeuka mbogo, kiasi cha kutishia kuachia wadhifa wake.
Katika mahojiano juzi na Mwananchi, January hakutaka kusema chochote kuhusu sakata hilo na hata jana alipohojiwa tena alisema kwa kifupi; “…mimi niko Kigoma kikazi, lakini pia si mmeishaandika kuhusu hayo mambo, sasa mnataka niseme nini tena, mimi nadhani inatosha?”.
Mpashaji habari wetu juzi alisema, "Yule kijana (January) alikasirika sana, alichukizwa kweli kweli na hali hiyo kwa sababu ni kama wajumbe waliopokea hizo bahasha walikuwa wakimzunguka kwani tayari walikuwa wanajua nini wanachopaswa kufanya ili kuziokoa sekta za nishati na madini,"kilieleza chanzo hicho.
Kadhalika suala hilo la hongo inadaiwa kwamba lilijadiliwa katika kikao cha pamoja baina ya wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, ambapo Waziri Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima waliomba radhi kutokana na tukio hilo, hivyo kamati hiyo kuagiza maofisa wa wizara waliohusika wachukuliwe hatua.
Ole Sendeka anena
Mbunge wa Simanjiro (CCM) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, Christopher Ole Sendeka alisema iwapo kuna fedha ambazo zipo kwa ajili ya kujaribu kuwashawishi wabunge wasifanye uamuzi wa haki ni hatari kwa mustakabali wa nchi.
“Mimi sikuwepo kwenye vikao hivyo, maana nililaziika kuwepo jimboni kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali, hivyo sifahamu chochote kuhusu suala hilo,” alisema Ole Sendeka na kuongeza:
“Lakini kama kuna fedha zipo tu zinaelea mahali, zikisubiri kuwashawishi wabunge wapindishe uamuzi wao, sasa ni kwa maslahi ya nani? Mimi nadhani hali hii ni hatari haipaswi kuachwa iendelee hivihivi”.
Alisema iwapo kuna ukweli kwamba baadhi ya wabunge wanahongwa, basi anayewahonga ana ajenda binafsi na kwamba upo uwezekano bajeti inayolazimishwa kupitishwa kwa rushwa imebeba maslahi ya mtu huyo.
“Bajeti ni ya serikali, akitokea mtu anataka kutoa hongo ili bajeti ipite kiualini basi huyo lazima ana maslahi yake, na hapa mimi ndipo nasema lazima wabunge na wajumbe wa kamati zetu hizi tuwe imara, vinginevyo tutajikuta tunapitisha bajeti zinazolinda maslahi ya wachache,”alisisitiza mbunge huyo.
You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA LEO - Pinda azungumzia kashfa Wizara ya Ngeleja
0 comments