IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MAWAZIRI wawili jana waliungana na wadau mbalimbali wa sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji wadogo, kupinga muswada wa sheria mpya ya madini na hivyo kumuweka kiti moto Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Tofauti na utamaduni wa siku zote wa uwajibikaji wa pamoja, Stephen Wassira, ambaye ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, na Ezekiel Maige, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, waliungana na wengine kukosoa muswada huo wakisema umejaa mapungufu makubwa na unalenga kunufaisha wachimbaji wakubwa na kuacha wadogo.
Mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali, Andrew Chenge ambaye ni mbunge wa Bariadi Magharibi, pia alikuwa ni mmoja wa watu walioshiriki mkutano wa siku moja baina ya wadau wa madini na wabunge, akitaka muswada huo ujadiliwe upya kabla ya kuwasilishwa bungeni.
Muswada huo ulitakiwa ujadiliwe leo na kupitishwa baada ya habari kueleza kuwa Rais Jakaya Kikwete alitoa hati ya dharura ya kuharakishwa kwa taratibu za kuupitisha, lakini hata kabla ya kuingia bungeni mambo yanaonekana kuwa magumu na huenda ratiba ikabadilishwa ili ujadiliwe baadaye.
Tayari Bunge limeshakataa miswada miwili iliyowasilishwa na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na ule ulirejeshwa mwaka jana wa Sheria ya Baraza la Usalama wa Taifa uliowasilishwa na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), huku Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyopitishwa mapema mwaka huu ikitarajiwa kujadiliwa upya na mkutano huu.
Dalili za mkutano huo wa wadau wa madini na wabunge kuonekana kuwa mbaya kwa Ngeleja zilianza kujitokeza wakati Waziri Maige alipokuwa wa kwanza kuchangia aliposema kuwa muswada huo unaonekana wazi kumnufaisha zaidi mchimbaji mkubwa na kumuacha mdogo.
Sehemu mojawapo ya muswada inaeleza mchimbaji mdogo haruhisiwi kupata leseni ya kufanya utafiti, zaidi ya leseni ya kuendesha uchimbaji tu huku mchimbaji mkubwa akipewa miaka mitano kufanya utafiti kabla ya kuanza rasmi kuchimba madini.
Katika maana nyingine, alisema, mchimbaji mdogo atapaswa kulipa kodi mara tu anapoanza kazi ya kuchimba madini wakati mkubwa anaachwa kuendesha shughuli za madini kwa miaka mitano bila ya kulipa kodi, kitu ambacho wadau wa madini, walisema hakifai.
"Muswada huu haufai kwa sababu hauna sehemu yoyote inayoonyesha kuwa itamsaidia mchimbaji mdogo. Kibaya zaidi waziri amejipa madaraka makubwa ya kuamua moja kwa moja mambo mengi dhidi ya madini, kitu ambacho si sahihi," alisema Amani Mnginda wa asasi inayofuatatilia masuala ya sera, Policy Forum.
Kauli ya Mnginda iliungwa mkono na Waziri Wassira ambaye alishauri sheria ilenge kuangalia nani anapata nini.
Wassira alitoa mfano kwamba wakati fulani alikuwa kwenye mkutano wa uchumi nchini Uswisi ambako alikutana na waziri wa madini wa Sweden na kumuuliza wanafanya nini ili kuhakikisha nchi inanufaika.
"Alinijibu kwa kifupi kwamba kipaumbele chao ni wawekezaji wa ndani," alisema Wassira.
"Wazungu ambao ndio wenye kumiliki biashara ya madini siwaoniĆ¢€¦ namuona hapa (mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini, Amin) Mpungwe Ć¢€¦aaah huyu ni mwenzangu mimi tu, kuna wenyewe, wako wapi?
"Ninachotaka kusema ni kwamba, tuangalie namna ya kunufaika na madini yetu. Hata wenzetu wa Afrika Kusini wana maendeleo; wamejenga barabara za juu kwa juu kwa sababu wametumia vizuri madini yao. Kama hatutakuwa makini Watanzania tutabakia na mashimo tu.
Wassira alisema inasikitisha kwamba baadhi wa wawekezaji wa kigeni wamekuwa wakinunua mbogamboga na hata maji ya kunywa kutoka Ulaya, hivyo kuwakosesha mapato Watanzania ambao wangeweza kuuza mazao yao kwao.
Katibu wa Chama cha Wachimbaji Madini wa Wilaya ya Ulanga, Christoms Msakamba alisema muswada huo unapaswa kujadiliwa na wadau kabla ya kuwasilishwa bungeni, akisema una kasoro nyingi.
"Baadhi ya kasoro hizo ni mfumo wa utoaji leseni ambao kimsingi unaonyesha kuendelea kumnyonya mchimbaji mdogo hasa kwa kutompatia unafuu wowote, huku mchimbaji mkubwa akipatiwa nafasi ya kuendesha tafiti kwa zaidi ya miaka mitano bila kutakiwa kulipa kodi," alisema.
Msakamba pia alilalamikia muswada kupendekeza nafasi ya naibu kamishna wa madini iondolewe, na kuongeza kwamba hiyo itachangia usumbufu kwa wadau wa madai hasa katika utoaji wa leseni.
"Sasa hivi pekee kuna maombi zaidi ya 5,000 ya leseni hayajafanyiwa kazi pale wizarani. Tukisema tuondoe nafasi ya kamishna msaidizi, maana yake ni kuongeza hali mbaya ya utendaji," alisisitiza.
Waziri Ngeleja alisema kuwa wizara yake itafanyia kazi maoni hayo.
Kwa sasa Sheria ya Madini inayotumika nchini ni ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwa inanufaisha zaidi wageni hasa katika suala la mrabaha wa asilimia tatu kwa wakia.
Alipoingia madarakani Rais Jakaya Kikwete aliahidi kupitia upya sheria ya madini na kuifanyia marekebisho na tayari hadi sasa mikataba ya madini ilikwishapitiwa na Tume ya Jaji Mark Bomani na kupendekeza hatua za kuchukua.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuhakikisha asilimia 60 ya fedha za mauzo ya dhahabu zinawekezwa kwenye mabenki ya nchini ili kuongeza thamani ya shilingi na kukuza uchumi wa nchi.
You Are Here: Home - - Mawaziri wawili wamgeuka Ngeleja muswada wa madini
0 comments