IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
HALI ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imezidi kuwa tete, baada Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuitisha kikao cha dharura cha wabunge wa chama hicho mjini Dodoma juzi kwa ajili ya kujadili na kukemea tabia ya kupakana matope wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba.
Habari za kuaminika ambazo Tanzania Daima Jumapili limezipata kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa zamani wa Bunge wa Pius Msekwa, zinasema kikao hicho kilitawaliwa na mjadala mkali wa baadhi ya wana CCM, hasa waliotangaza nia ya kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali.
“Ni kweli tulikutana wote chini ya Mwenyekiti wetu, Waziri Mkuu jana (Ijumaa) kujadiliana masuala mbalimbali, lakini moja ya ajenda kubwa iliyoonekana ni suala zima la mwenendo unaonyesha namna baadhi ya watu waliotangaza nia ya kugombea ubunge wanavyowapaka wabunge walioko madarakani matope.
“Wabunge wengi wamepinga utaratibu ambao umeanza kutumika kuruhusu watu kupita kwenye majimbo na kuanza kunadi sera zao kabla ya tarehe ya kampeni kufika, hawa wameonekana wazi kabisa wameanza kupiga kampeni hadharani.
Chanzo hicho kilisema watu hao wameanza kupita maeneo mbalimbali ikiwemo misikitini, makanisa na kwenye mikusanyiko ya watu huku wakitoa misaada mbalimbali kama fedha, nguo, vifaa vya michezo na ahadi mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zinakuwa na lengo la kujipigia debe.
Kiliongeza kuwa malalamiko hayo yalimfanya Waziri Mkuu kukemea vikali tabia hiyo ambayo si tu inakiaibisha chama bali inajenga uhusiano mbaya miongoni mwa wanachama ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa na uhusiano mbaya kiasi cha kukifanya chama kuunda kamati ya kutafuta chanzo cha kutoelewana na kuangalia namna bora ya kusuluhishana.
“Pinda ameagiza wanachama wote ambao wameanza mchezo huo wafuatiliwe, na majina yao yawasilishwe kwenye mamlaka husika ili wachukuliwe hatua za kinidhamu; lakini pia wasiteuliwe wakati wa mchakato wa kugombea ubunge,” kilisema chanzo kingine.
Tanzania Daima Jumapili ilidokezwa kuwa Waziri Mkuu ameagiza zichukuliwe hatua kwa watumishi wote wa serikali ambao wametangaza nia ya kugombea ubunge kuwa kwa kufanya hivyo wamekiuka sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Chanzo kingine kimedokeza kuwa Waziri Pinda alisema kuna zaidi ya wakuu wa mikoa 10 na wakuu wa wilaya wapatao 30 wametangaza nia ya kugombe ubunge katika uchaguzi mkuu ujao huku wengine wakitumia nafasi zao kufanya kampeni na kuwachafua wenzao.
“Alituambia kuwa watumishi wa serikali waliotangaza nia ya kugombea ubunge wakiwemo ma-RC na ma-DC, wanapaswa kuchukua likizo ya bila malipo ili wakatumikie siasa hadi uchaguzi mkuu utakapomalizika,” kilisema chanzo hicho.
Habari zaidi zinasema kuwa ameonya viongozi hao ambao wamekuwa wakitumia posho za serikali na magari kwenda majimboni kwa ajili ya kuweka mikakati mbalimbali ya kampeni huku wakitumia fedha za walipa kodi kwa ajili ya masilahi binafsi jambo ambalo halikubaliki na ni kinyume na sheria za utumishi wa umma.
Pinda alikwenda mbali zaidi kuwa watendaji hao wapo hatarini kupoteza kazi zao kama hawatajirekebisha kwa kuwa tayari baadhi ya majina yao yameshatajwa kwenye ngazi za juu za uongozi serikalini.
Chanzo hicho kilisema, idadi kubwa ya wabunge waliohudhuria mkutano huo waliishambulia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa imekuwa chanzo kikubwa cha kuwalinda baadhi ya vigogo wanaopita majimbo na kutoa misaada bila kuogopa kukamatwa.
“Wabunge wengi wameilalamikia TAKUKURU mno kuwa imekuwa chanzo cha kuhifadhi vigogo ambao wameanza kupita majimboni na kugawa misaada, tunaamini kwa vile wengi wao ni watumishi wa serikali inaona aibu kuwakamata,” kilisema chanzo chetu.
Kutokana na hali hiyo, maafisa wa TAKUKURU wameagizwa mara moja kusoma na kuelewa Sheria ya Gharama za Uchaguzi waielewe vyema badala ya kukurupuka na kukamata wanasiasa hovyo.
“Unajua imeonekana TAKUKURU imeanza kamatakamata kila sehemu kwenye majimbo mbalimbali… hata kwa wabunge ambao kisheria bado wako madarakani kwa mujibu wa sheria hadi Bunge litakapovunjwa… wametakiwa wakasome vizuri sheria hii.
“…Unaelewa kuwa sisi wabunge tuliahidi mambo mengi mwaka 2005, sasa unapokwenda kwa wapiga kura kutoa misaada uliyoahidi unaonekana kama unatoa rushwa jambo ambalo si cha kweli,” alisema mmoja mbunge mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Hoja nyingine iliyojadiliwa kwenye kikao hicho, ni namna ya kifungu namba 7 (c) ambacho kiko kwenye Sheria ya Gharama za Uchaguzi kinavyoelezea muundo wa timu za wagombea kuanzia ngazi ya udiwani na ubunge zinavyotakiwa kuwa chini ya viongozi wa serikali.
“Imeonekana wazi kwamba kwenye muundo wa timu za wagombea kuna kasoro za usimamizi… sasa imeshauria maafisa ya serikali kuanzia ngazi ya kata wajumuishwe kwenye timu hizo.
Mkutano huo wa CCM unafanyika huku kukiwa na wingu zito wa namna mgogoro uliozuka baina ya makundi yanayohasimiana ndani ya chama hicho ambalo limechangiwa kwa kiasi kubwa na tuhuma za ufisadi utakavyosuluhishwa na kamati iliyoundwa na Halimashauri Kuu ya CCM (NEC) chini ya uenyekiti wa Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
CCM inadaiwa kugawanyika katika makundi mawili ambapo moja linadaiwa kuwa katika upande wa Spika wa Bunge Samuel Sitta ambaye anasemekana kuwa mstari wa mbele kutaka vigogo wa ufisadi washughulikiwe ndani na nje ya chama huku kundi la pili linalodaiwa kuongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa likidaiwa kupingana na lile la Sitta kwa madai kuwa ni vema sheria zikachukua mkondo wake badala ya watu kusingizia au kuelekezeana tuhuma kwa lengo la kuchafuana.
Makundi hayo mawili yalijipambanua baada kuibuka kwa kashfa ya kuzalisha umeme wa dharura kupitia kampuni ya Richmond, kashfa iliyomsababishia Lowassa na mawaziri wawili, Nazir Karamagi (Nishati na Madini) na Ibrahimu Msabaha kuachia nyadhifa zao baada ya kuguswa na kamati teule ya Bunge iliyokuwa chini ya uenyekiti wa mbunge wa Kyela Dk. Harisson Mwakyembe.
You Are Here: Home - - CCM kwafukuta • TAMAA YA UBUNGE KUFUKUZISHA WAKUU WA MIKOA 10, WAKUU WA WILAYA 30
0 comments