Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Serikali yatangaza eneo la Sterling kuwa Hifadhi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAZIRI wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kulitangaza eneo la Sterling lililogundulika kuwa na rasilimali nyingi ya maji chini ya ardhi kuwa eneo la Hifadhi.

Agizo hilo la Profesa Mwandosya alilitoa juzi katika mji wa Same baada ya kuelezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Lister Kongola kuwa eneo hilo limegundulika kuwa na hazina ya maji.

Kongola  alisema eneo hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba kati ya 15 na 20 linapaswa kuhifadhiwa.

Mkurugenzi huyo msaidizi alisema utafiti wa kitaalamu umebainisha kuwa visima hivyo viwili vinavyochimbwa vina uwezo wa kutoa maji yenye ujazo wa mita kati ya 50-60 na eneo hilo ni mkombozi wa tatizo la maji Mji wa Same.

Baada ya kupokea maelezo hayo na baadaye kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uwanja wa Kwasakwasa, Profesa Mwandosya alisema kuwapo kwa eneo la Sterling ni Mungu ameipendelea Same.

Waziri Mwandosya aliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha eneo hilo ambalo baadhi ya wananchi walipimiwa viwanja na kuanza ujenzi, halivamiwi na maeneo ambayo hayajajengwa hayajengwi tena.


“Hivi ni lazima hawa watu wakajenge juu ya eneo lenye chanzo cha maji?, wapimieni wananchi maeneo mengine lile liwe eneo la hifadhi na kwa hili lenye maslahi ya wengi naomba watu wachache watusamehe”alisisitiza waziri.

Profesa Mwandosya aliitaka Halmashauri hiyo ya Same kuanzisha mchakato wa kisheria wa kulitangaza eneo hilo kuwa hifadhi kwa kutumia sheria ndogo za Halmashauri na wakikwamba wawasiliane na wizara kwa msaada zaidi.

Awali akitoa taarifa ya Halmashauri kwa waziri, Mhandisi wa wilaya hiyo, Fimbo Mtango alisema ingawa mahitaji ya maji katika mji wa Same ni meta za ujazo 4,500 kwa siku, kwa sasa upatikanaji wake ni meta za ujazo 750 tu.

Kutokana na kushuka huko kwa uzalishaji wa maji, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Same(Sauwsa) yameshuka kutoka Sh12 milioni kwa mwezi hadi kufikia Sh9 milioni.
Tags:

0 comments

Post a Comment