Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Maaskofu wamkataa meya wa CCM Arusha

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MAASKOFU wa makanisa ya Kikristo mkoani Arusha, wametoa tamko la pamoja la kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha aliyeteuliwa na CCM na kuweka bayana kwamba "hawatampa ushirikiano".Walitoa tamko hilo jana wakati wakilaani hatua ya polisi mkoani Arusha, kutumia nguvu kupita kiasi katika kuvunja maandamano ya amani ya Chadema na hivyo kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 20.

Akisoma tamko la umoja wa viongozi wa dini ya kikristo mkoani Arusha, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu alisema Jeshi la Polisi ndilo lilikuwa chanzo cha vurugu hizo.

Tamko la maaskofu hao limekuja siku moja tu tangu Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha atoe tamko kwamba vurugu zilizotokea Arusha ni tatizo la kisiasa ambalo pia litapaswa kushughulikiwa kisiasa.

 “Wote tunapaswa kulinda amani yetu. Tunapaswa kutuliza hali ya Arusha. Kilichotokea Arusha ni mgogoro wa kisiasa, tutautatua pia kisiasa,” alisema Nahodha alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, juzi jijini Dar es Salaam.

Kuhusu uwezekano wa kutengua matokeo ya umeya Arusha, suala ambalo pia Chadema wanalilalamikia, Naodha alisema “Sina uhakika kama tatizo la msingi lililopo Arusha linatokana na Umeya. Lakini katika mazungumzo tukibaini kuwa hilo ndiyo tatizo basi tutalifanyia kazi.”

Lakini jana Askofu Lebulu alisema, "Sisi kama viongozi wa dini hatuwezi kushirikiana na mtu ambaye hakushinda kihalali, kuna mtu alipiga kura si diwani wa Arusha, Chadema hawakushirikishwa na pia taratibu na kanuni za uchaguzi huo zilikiukwa".

Maskofu hao walisema chanzo cha vurugu hizo ni hila zilizofanywa na baadhi ya watu ili kumsimika Meya wa jiji la Arusha, Gaudence Lyimo wa CCM. 
   
Kwa mujibu wa malalamiko ya Chadema, mbunge ambaye hakustahili kupiga kura ni wa viti maalum CCM Mkoa wa Tanga na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda ambaye alipiga kura kama diwani wa Arusha.

Katika tamko lao, maaskofu hao walieleza kuwa kama Serikali inataka kutunza amani inatakiwa kuhakikisha haki inatendeka kwani haki na amani ni vitu visovyotenganishwa.
 
"Serikali ina wajibu na dhamana ya kutunza watu wake, hatukubaliani na mtu yoyote ambaye anaamua kutekeleza mauaji kwa wengine," alisema Leburu.
 
Hata hivyo, maaskofu hao, walitoa wito kwa vyama vya siasa kukubali kushindwa na kukosolewa, lakini wakasisitiza kuwa wito huo hauna maana kwamba wakae kimya pale wanapotendewa vibaya.
 
Maaskofu hao pia waliigeukia Chadema wakisema haiwezi kukwepa kuwa sehemu ya chanzo cha vurugu hizo kwa sababu ilikuwa na uwezo wa kuwazuia wafuasi wake kutoandamana ili kutii amri iliyotolewa na polisi.

"Lakini pia Chadema walitakiwa kufanya kila jitihada kuwajulisha wafuasi wake kutoandamana licha ya kuzuiwa kufanya maandamano hayo muda mfupi kabla ya kuanza," alisema Askofu Lebulu.

Kutokana na vurugu hizo, Maaskofu hao walisema Serikali inapaswa kushughulikia mgogoro wa Arusha kwa hekima, busara na uwazi kwani ni dhahiri kuwa taratibu za kumchagua Meya zilikiukwa.
 
Askofu Lebulu pia alisema Serikali inapaswa kuchukua tukio la Arusha kama jambo la kitaifa na kufanya jitihada za kulishughulikia haraka na kwa amani.
 
Naye, Askofu Thomas Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Arusha, alisema kutokana na polisi kutumia nguvu kubwa, hawatasitisha mahusiano yao na Serikali pamoja na  polisi kwa sababu kufanya hivyo ni kujitenga na majukumu.
 
"Ushirikiano wetu hauwezi kukatishwa na vurugu hizi kwani huwezi kutatua tatizo kwa kulikwepa," alisema Askofu Laizer.
 
Katika kikao hicho, pia walihudhulia Askofu Martin Shao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, na maaskofu wa makanisa na Kipentekoste ya mkoani Arusha.
 
Wakati huo huo, Meya  anayelalamikiwa Gaudence Lyimo amesema hafikirii kujiuzulu katika nafasi hiyo kwani amechaguliwa kihalali na kwa kufuata taratibu.
 
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Lyimo alisema kitendo cha Chadema kuandamana na watu kufariki kutokana na mgogoro wa yeye kuchaguliwa hakuwezi kumsukuma ajiuzulu.
 
"Mimi kwa nini nijiuzulu? Nimechaguliwa na madiwani kwa kufuata sheria na hao waliandamana  mimi siwezi kuwazungumzia kuwa waliandamana kwa ajili yangu," alisema Lyimo.
 
Wafuasi wa Chadema, wakiwepo wabunge na viongozi wa Kitaifa, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa walifanya maandamano Alhamisi iliyopita licha ya kuzuiwa na polisi makao makuu wakati ambapo yalikuwa yamepewa kibali na Polisi mkoa wa Arusha.
 
Katika maandamano hayo, watu watatu wamefariki ambao ni Denis Shirima (25), Mwita Marwa (24) na Ismail Omar (40) huku wengine zaidi ya 20 wakijeruhiwa 16 kwa kupigwa risasi.
Tags:

0 comments

Post a Comment