Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kauli ya Nahodha yamgeukia ‘kaa la moto’

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter WASOMI wamekosoa kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, kuhusu vurugu zilizotokea Arusha kuwa ni tatizo la kisiasa, linahitaji suluhisho la kisiasa. Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema vurugu hizo haziwezi kusuluhishwa kisiasa kwa sababu kilichofanyika ni ukiukaji wa haki za binadamu. 

Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abdallah Safari, alisema vurugu za Arusha hazikusababishwa na mambo ya siasa, kwani zilitokea baada ya uvamizi wa polisi kwenye maandamano ya amani ya Chadema. 

“Sikubaliani na kauli ya Waziri Nahodha kuwa vurugu hizo zisuluhishwe kisiasa. Hakuna suluhisho la kisiasa, kwa sababu vurugu hazikuwa za kisiasa, vurugu hizo zimesababishwa na polisi na tayari suala hilo liko mahakamani,” alisema na kuongeza: “Uhuru wa kuandamana ni haki ya kikatiba, polisi wanaarifiwa tu kuhusu hilo sio kuomba ruhusa, hivyo hawana nguvu kisheria za kuzuia maandamano.” Profesa Safari alisema inapofikia hatua ya polisi kuua raia, suluhisho la kisiasa haliwezi kuwepo, badala yake, suala hilo lishughulikiwe kisheria. 

Kwa upande wake, Profesa Chris Maina, ambaye pia ni Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisisitiza kuwa dola inapaswa kuhakikisha haki za kikatiba za raia zinatimizwa, ikiwamo kuandamana na kutoa maoni yao. “Suala la msingi hapa ni haki za binadamu kuzingatiwa, watu waheshimu haki za kikatiba,” alisema Profesa Maina. 

Hata hivyo, Mhadhiri mwingine chuoni hapo, Bashir Ali, aliunga mkono kauli ya Waziri Nahodha kuwa, vurugu hizo zinapaswa kusuluhishwa kisiasa, huku akipinga waziri huyo kugeuka msuluhishi suala linalohusu wizara yake.

 “Naunga mkono kauli hiyo, lakini Nahodha hatakiwi kusema hayo, Waziri Mkuu ndiye anayepaswa kulitolea tamko kwa sababu yeye (Waziri Mkuu) ndiye kiongozi wa shughuli za serikali,” alisema Ali. Ali alisema serikali inapaswa itoe kauli kuhusu sakata la umeya wa Arusha na suala la katiba mambo ambayo ndio malalamiko ya Chadema yaliyosababisha maandamano hayo.
Tags:

0 comments

Post a Comment