Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kenya yaboronga soko la EAC

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

BIDHAA za Kenya zenye thamani ya Sh30 bilioni zitazuiwa kuingia nchini kuanzia mwezi Machi mwaka huu baada ya  kukosa viwango vya ubora vinavyokubalika katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), zimeeleza kwamba Kenya inatumia alama mbili za viwango vya ubora jambo ambalo ni kinyume na makubaliano ya Jumuiya hiyo.

Gazeti la Business Daily linalochapishwa nchini Kenya jana lilimkariri Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini humo, Patick Obath akisema  bidhaa hizo, hazitaruhusiwa kuingia nchini baada ya Machi.

“Tutashindwa kushindanisha bidhaa zetu nchini Tanzania kama hatutafikia uamuzi wa kutumia alama moja ya ubora,” alisema Obath katika gazeti hilo.

Taarifa zimeeleza kuwa Kenya sasa inatumia alama mbili za ubora; Diamond na Standard.  “Kuanzia Machi, mwaka huu bidhaa zenye thamani ya Sh 30 bilioni, huenda kikazuiliwa kuingia Tanzania, kutokana na matumizi ya alama hizo,” alisema Obath.

Lakini Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limeishauri Kenya kuharakisha kufikia viwango vinavyokubalika kabla ya muda huo ili isipoteze soko lake.  Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa TBS, Daudi Mbaga, alisema nchi hiyo iharakishe kufanya uamuzi wa kutumia alama moja ya viwango vya ubora kama ilivyokubalika katika jumuiya hiyo. 

Alisema kuanzia sasa hadi Machi mwaka huu, nchi hiyo imeombwa kuchagua alama moja ya viwango vya ubora kama inataka kuendelea kuuza bidhaa zake nchini.

“ Nchi zote mwanachama zilishakubaliana kutumia alama moja ya ubora. Tanzania tuna alama moja, Uganda pia wana alama moja, lakini wenzetu Kenya, wana alama mbili za ubora,”alisema.

Alisema mpango huo, wa nchi kuwa na alama moja ya ubora, umelenga kuzifanya nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na alama moja ya ubora katika siku za usoni.  “ Lakini tunadhani kwamba hadi Machi mwaka huu, Kenya itakuwa imefanya maamuzi ya kutumia alama moja. Hatupendi tufikie katika hatua ya kuzuia bidhaa za nchi hiyo,”alisema.

Kenya inauza Tanzania bidhaa mbalimbali, lakini hasa bidhaa za saruji, mafuta ya kupikia, sukari na unga wa ngano.  Gazeti hili pia limeukariri uongozi wa Shirika la East African Portland Cement la Kenya, ukisema iwapo suluhu hiyo haitapatikana, Sh 43 milioni za Kenya zinaweza kupotea ambazo mwaka jana zilipatikana kwa kuuza saruji hapa nchini. 

“Bado tunafikiria ni alama gani ya ubora tutumie kwenye bidhaa yetu na ni vipi itaathiri mauzo ya bidhaa yetu,” alisema Meneja Mauzo ya Nje, Abraham Kiprotich.

Kwa mujibu wa ofisi ya Takwimu ya Kenya, katika kipindi cha mwaka jana, mauzo ya bidhaa zake Tanzania yalikua hadi kufikia Sh30 bilioni.  

Tags:

0 comments

Post a Comment