Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Dk Slaa, Mbowe kupanda tena kizimbani leo?

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

MACHO na masikio ya waanachama, mashabiki na wapenzi wa Chadema, leo yataelekezwa tena mkoani Arusha ambako viongozi wakuu wa chama hicho, watapandishwa tena kizimbani kusikiliza kesi waliyofunguliwa baada ya maandamano ya Januari 5 mwaka huu. 
Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa, wabunge  watatu na watu wengine 24, walifunguliwa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi mkoani Arusha, wakituhumiwa kukusanyika bila kibali.

Kesi hiyo inatajwa huku Chadema wakiwa wameishatangaza kutokwenda mahakamani kuhudhuria kesi hiyo kama moja ya sharti la kumaliza mgogoro wa kisiasa mkoani Arusha.

Kufutwa kwa kesi hizo au Chadema kutohudhuria tena mahakamani,  ni moja kati ya masharti saba yaliyotolewa na chama hicho kwa serikali katika kulimaliza tatizo la mjini Arusha.

 Mara ya kwanza, viongozi hao walipanda kizimbani Januari 6 mwaka huu, siku moja tangu kufanyika kwa maandamano ambayo katika kuzimwa kwake na polisi yalisababisha maafa ikiwa ni pamoja na vifo vya watu watatu. 

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Zakaria Elisante, alimweleza hakimu mfawidhi Charles Magesa  kuwa, watuhumiwa hao, wote wametenda kosa moja la kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria.

Elisante alisema watuhumiwa hao, walivunja sheria namba 74 na 75 kifungu cha 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 na pia sheria ya polisi sura 45 kifungu cha 322  ambayo pia ilifanyika marekebisho mwaka 2002.

Hata hivyo, watuhumiwa wote walikana makosa hayo, ambapo mawakili watatu wa serikali waliokuwa wanaongozwa na  Elisante walisema hawana pingamizi la dhamana ya washitakiwa hao.

Washitakiwa hao, wanatetewa na Mawakili  Method Kimomogoro na Arbert Msando.

Katika mwendelezo wa kesi hiyo leo, viongozi hao wa Chadema wanatarajiwa kuunganishwa na watuhumiwa wengine ambao Januari 6, waliosomewa mashtaka wakiwa hospitali. Watuhumiwa hao ni mchumba wa Dk Slaa, Josephine Mushumbuzi, Kenedy Bundara, Juma Wambura na Richard Mtui.

Chadema walitoa kauli kwamba hawatakwenda mahakamani leo,  Januari 12 mwaka huu wakati wa kuaga miili ya watu wawili waliofariki kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano hayo.

"Kesi walizofunguliwa viongozi na wafuasi wa Chadema, zifutwe bila masharti na kuanzia sasa, viongozi hao, hawatahudhuria tena mahakamani kusikiliza kesi hizo za uongo," alisema mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alipokuwa akisoma tamko la chama hicho

Mbali na sharti hilo,  mengine ni kujiuzulu na kufunguliwa kesi za jinai kwa IGP Said Mwema na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha.

Mbowe alisema katika kuhakikisha masharti hayo yanafuatwa na madai kutekelezwa, chama hicho kimewaelekeza viongozi, wanachama na wafuasi wake nchini, kuandaa maandamano ya amani nchi nzima kwa ajili ya kulaani mauaji hayo.

"Chadema taifa itatuma maafisa wa ngazi za juu wa chama, wakiwemo Wabunge na Wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho kushiriki maandamano hayo kwa ngazi za mikoa na wilaya ili kuyaongezea nguvu na hamasa," alisema Mbowe na kuongeza: “Ni siku ambayo haitasahaulika katika historia ya Tanzania. Ni siku ya kihistoria.” 

Kwa mujibu wa Mbowe, masharti mengine katika kulipatia ufumbuzi suala hilo  ni kujiuzuuu pia kwa Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye na kufunguliwa mashtaka ya jinai na kufutwa kwa kesi zote zilizofunguliwa dhidi ya viongozi na wanachama wa Chadema kwa ajili ya kujihusisha na maandamano hayo.

Mbowe alifafanua kuwa kujiuzulu kwa IGP Mwema, Waziri Nahodha na RPC Andengenye kutapisha uchunguzi huru na wa kina wa matukio yote yaliyosababisha wananchi hawa kuuawa na mamia kujeruhiwa huku wengine kadhaa  wakikamatwa bila sababu. 

Mbowe pia alisema Chadema imetaka  matokeo ya uchaguzi wa umeya Arusha yafutwe na uchaguzi uitishwe mpya na kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kwa ajili ya kuchunguza vurugu za Arusha. 

“Damu iliyomwagwa Arusha inalilia haki, roho za wote waliotolewa mhanga na polisi zinahitaji haki ili ziweze kutulia na mizimu yao ipumzike. Wote walioumizwa na ujambazi wa polisi wanalilia fidia ya kuuguza maumivu yao ya kimwili, ya kiroho na ya mali zao zilizoharibiwa,” lilisema tamko hilo lililotumwa kwa vyombo vya habari muda mfupi kabla Mbowe hajalisoma akiwa Arusha.

Tamko hilo limeongeza “Sheria za nchi yetu zilizokanyagwa chini kana kwamba hazipo zinahitaji kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa ili iwe fundisho kwa wahalifu wengine wa aina hii.”  “Sisi sote tuliokusanyika hapa leo, na wale wote wanaotusikiliza na kutuangalia mahali popote nchini na hata nje, tuna jukumu la kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wale ambao tunaomboleza vifo vyao,” linaendelea tamko hilo.

Kwa mujibu wa Mbowe, Chadema ina jukumu la kuhakikisha haki inapatikana kwa wale wote walioumizwa kwa risasi na mabomu na virungu.  

“Tuna jukumu la kuhakikisha wale wote ambao waliharibiwa mali zao kwa sababu ya uhalifu huu wa polisi wanafidiwa kwa kiasi chote cha hasara waliyoipata na kwamba polisi hawarudii tena ujambazi wa aina hii dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia yoyote kwa kuwawajibisha wale wote walioshiriki,” alisema na kuongeza:  “Fidia stahili ilipwe kwa mujibu wa sheria husika za nchi kwa ndugu na jamaa wa waliouawa kutokana na polisi na walioumizwa kwa namna yoyote ile au kuharibiwa mali zao kutokana na vurugu hizo.”

Aliendelea “Tunasisitiza katika jambo hili kwamba viongozi, wanachama na wafuasi wetu wote waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka haya, hawatahudhuria mahakamani tena kuhusiana kesi iliyofunguliwa dhidi yao, hata kama kwa kufanya hivyo kutafanya wakamatwe na kurudishwa tena gerezani.” 

Mbowe alisema, kwa vile uchaguzi wa viongozi wa halmashauri ya Jiji la Arusha ndio chanzo cha mauaji ya wananchi na kwa kufahamu utaratibu haramu uliotumika kumpata Meya wa Jiji hilo, matokeo ya uchaguzi huo yafutwe na uchaguzi mpya uitishwe haraka.

Alisema haki ya vyama vya siasa na wananchi kufanya maandamano ya amani kama inavyotambuliwa na katiba ya Muungano wa Tanzania iheshimiwe na kutiliwa nguvu zaidi kwa kufuta vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi na ya Vyama vya Siasa vinavyoruhusu Jeshi la Polisi la Tanzania kuzuia na/au kusitisha maandamano ya amani. 

“Badala yake, sheria ziweke wazi wajibu wa Jeshi la Polisi la Tanzania kulinda maandamano ya amani na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na/au ya wananchi na sio kuruhusu au kukataza mikusanyiko hiyo,” alisema Mbowe. 

Mbowe aliitaka serikali kupitia mahakama, kuunda Tume huru ya uchunguzi ya kimahakama (Judicial Commission of Inquiry) itakayoundwa na majaji wa Mahakama ya Rufani nchini ili kufanya uchunguzi huru, wa kina na wa wazi wa matukio yote yaliyosababisha IGP Mwema kupiga marufuku maandamano ya amani na mkutano wa hadhara.

Alisema agizo hilo ndilo lililoambatana na Jeshi la Polisi kufanya vurugu na kusababisha mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia. 

“Tunapenda kusisitiza kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kwa sababu historia ya tume nyingine ambazo zimeundwa kwa utaratibu wa Rais kuteua watu anaowataka inaonyesha zimefanya kazi zao za uchunguzi mafichoni bila kushirikisha wadau wengine na bila wananchi kufahamu kitu kinachoendelea,” alisema Mbowe.

 Alisema mauaji ya Arusha yanathibitisha wazi mahitaji ya katiba mpya ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania na marekebisho ya dhati ya sheria nyingine za nchi ikiwa ni pamoja na ya Jeshi la polisi na ya vyama vya siasa. 

Hotuba hiyo ndefu ya Mbowe ilpangwa kwa utangulizi, siku ya historia, maandamano halali, jeshi la wahalifu, mauaji ya kupangwa, kisasi cha uchaguzi mkuu, haki lazima itendeke na mauaji ya Arusha na mahitaji ya katiba mpya.
Tags:

0 comments

Post a Comment