Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Vigogo TLP wapingana vikumbo kumrithi Mrema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
VIGOGO kadhaa wa TLP, akiwemo aliyewahi kuwa mbunge kupitia chama hicho ambaye sasa ni kada wa CCM, Thomas Ngawaiya wanatajwa kuanza kupigana vikumbo kwa ajili ya kumrithi Mwenyekiti wa chama hicho, Agostine Mrema ambaye anadaiwa anajiandaa kustaafu.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na katibu Mkuu wa TLP, Hamad Tao zimeeleza kuwa Mrema atastaafu kuwa mwenyekiti wa chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Nafasi hiyo, sasa imeanza kupigiwa chapuo na watu watano ambao pamoja na Ngawaiya, Mugahywa Mutamwega na Macmilian Lyimo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Hamad Tao alisema; “Kuna uvumi kwamba Mrema anaweza akaachia nafasi hiyo kabla ya muda wake, lakini anapaswa kustaafu rasmi 2014."

Mrema aliliambia Mwananchi jana kuwa bado ni Mwenyekiti wa TLP hadi mwaka 2014 na kwamba hayo ni maneno ya watu wenye uchu wa madaraka.

“TLP mimi ndio Mwenyekiti, hao wenye uchu wafanye kazi zionekane ili hata nikitaka kustaafu nijue nani namshika mkono ambaye atakijenga chama,”alisema Mrema.

Alisema kisheria mwenyekiti wa chama anatakiwa awe mbunge kwa sababu anapokuwa bungeni ataweza kusimamia sera na hoja zake.

Mrema ambaye ni Mbunge wa jimbo la Vunjo, alisema kwa sasa anaweza kubeba kofia zote mbili kwani habebi kazi mgongoni bali anagawa kazi kwa watu.

Alisema mbali ya kuwa mwenyekiti wa chama taifa, pia ni mwenyekiti wa vikao, kamati kuu, halmashauri kuu, mkutano mkuu na sekretarieti.

“Nastaafu nimuachie nani kwasababu pale makao makuu ukitoka huwezi ukamuacha mtu aende kuwapeleka Kariakoo na Jangwani nitamkabidhi mtu mwenye uwezo wa kukijenga chama,”alisema.

Akizungumzia kutajwa kutaka kumrithi Mrema, Ngawaiya alisema taarifa hizo si za kweli kwa sababu yeye hawezi kutoka CCM kwa kuwa ana vyeo vingi.

Alitaja vyeo hivyo kuwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC), Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa.

“CCM wamenipa vyeo vya kutosha na ni chama tawala, nitakuwa sieleweki kama nitaamua kuhama,”alisema Ngawaiya.
Tags:

0 comments

Post a Comment