IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kitawasha moto wa madai ya kutaka Katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wote.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano katika mahojiano maalum, Dk. Slaa alisema mabadiliko ya Katiba wakati huu ni ya lazima na kwamba chama chake kimejipanga kuuelimisha umma kudai mabadiliko hayo.
Dk. Slaa ambaye alikuwa mgombea urais wa CHADEMA na kutoa upinzani mkali kwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, na kuambulia ushindi mwembamba, alisema hivi sasa chama chake kinaweka mikakati ya harakati hizo kwa kuwashirikisha wataalam wake wa ndani na nje ya chama.
“CHADEMA ni chama makini, si chama kinachofanya mambo kwa kukurupuka. Tunaandaa mkakati wa mwaka 2011-2015. Ifikapo Januari mwakani, tutapeleka mkakati huo kwenye vikao vya bodi, Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Baraza Kuu baada ya hapo tutaenda kwa wananchi na kuwasha moto nchi nzima kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kudai Katiba mpya,” alisema Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, CHADEMA inatambua kuwa suala la mabadiliko ya Katiba ni kilio cha Watanzania wengi, hivyo iko tayari kushirikiana na vyama, taasisi na watu binafsi ili kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya.
Wakati wa mikutano yake ya kampeni, Dk. Slaa katika mambo 15 ya vipaumbele vyake, aliahidi kufanya mabadiliko makubwa ya Katiba ndani ya siku 100 za kwanza endapo chama chake kingeingia madarakani.
Alikuwa akitoa ahadi hiyo kila mahali alipofika kuomba kura za kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Kasi ya CHADEMA kutaka mabadiliko ya Katiba, imechagizwa zaidi na matokeo ya uchaguzi mkuu ambapo mgombea wake, Dk. Slaa anaamini kushindwa kwake kumetokana na mfumo mbovu wa vyombo vinavyosimamia uchaguzi yaani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inayodaiwa kukibeba chama tawala.
Kuhusu kumtabua au kutomtambua Rais Kikwete, Dk. Slaa alisema Kamati Kuu ilipokea taarifa ya matokea ya urais; akayajadili na kukubaliana kuwa matokeo yaliyompa ushindi Rais Kikwete yalichakachuliwa kutokana na mfumo mbovu wa Katiba.
Alisema kutokana na sababu hizo, CHADEMA imependekeza kuundwa kwa kamati huru itakayochunguza matokeo hayo na kutoa taarifa itakayolenga kuweka wazi juu ya kila kitu kilichojiri kwa manufaa ya taifa.
“Ushahidi wa matokeo kutoka katika vituo kutofautiana na yale ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi; karatasi za matokea kufutwa ni vielelezo tosha kuwa matokea hayo yalichezewa,”alisema Dk. Slaa.
“Kisheria Tanzania ina Rais na sisi CHADEMA tunasema nchi hii ina Rais, lakini njia iliyotumika kumpata Rais huyo si halali na hilo ndilo lililosababisha wabunge wa CHADEMA kutoka nje siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Bunge,” alisema Dk. Slaa.
Wakati kasi ya kutaka mabadiliko ya Katiba ikiwa juu, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alitoa kauli iliyoibua mjadala kuwa serikali haiwezi kufanya mabadiliko hayo kwa madai kuwa haina fedha.
Hata hivyo kauli hiyo ilipingwa na wengi wakiwemo baadhi ya majaji na viongozi waandamizi wastaafu.
Moja wa majaji hao ni Amir Manento na Jaji Mkuu Augustine Ramadhan; lakini pia Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu wake, Frederic Sumaye, viongozi wa dini, wasomi na wanazuoni mbalimbali, wanaharakati, na wengineo wengi wanaunga mkono hoja ya kuandikwa Katiba mpya.
You Are Here: Home - - Slaa: Tutawasha moto • CHADEMA YAANDAA MKAKATI MZITO KUDAI KATIBA MPYA
0 comments