IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
RAIS Jakaya Kikwete yupo kwenye hatua za mwisho kuunda serikali yake, ambayo wachambuzi wa mambo wanaeleza kwamba huenda ikawa na mabadiliko makubwa kuondoka kasoro zilizojitokeza miaka mitano iliyopita.
Mtihani mkubwa ambao unamkabiri Rais Kikwete katika kuunda serikali yake ni kumpata Waziri Mkuu ambaye atamsaidia kuongoza nchi katika kipindi chake cha mwisho cha miaka mitano ijayo.
Kwa mujibu wa shughuli za bunge, jina la Waziri Mkuu aliyeteuliwa na Rais litawasilishwa bungeni, kesho kutwa kwa ajili ya kuthibitishwa na wabunge kwa kupigiwa kura.
Wanaotajwa kwamba huenda wakaukwaa uwaziri mkuu katika ngwe hii ya pili ya Rais Kikwete ni pamoja na Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Mizengo Pinda.
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa nchini wanasema kuwa Pinda anaweza kurejeshwa katika kiti hicho kutokana na rekodi yake ya uadilifu, kutokuwa katika makundi na kutohusika katika kashfa ya aina yoyote.
Pinda maarufu kama mtoto wa mkulima, amejipatia umaarufu kutokana na kutokuwa Waziri Mkuu anayependa matumizi mabaya ya fedha za umma, ikiwamo hatua yake ya kuzuia semina na safari za mara kwa mara za viongozi wa seriali nje ya nchi.
Mwingine ambaye anatajwa kuwa huenda akaupata uwaziri mkuu ni Spika aliyemaliza muda wake, Samwel Sitta.
Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki, mkoani Tabora anatajwa kuwa anaweza kuupata uwaziri mkuu ikiwa ni njia ya Rais Kikwete kumfariji baada ya Kamati kuu ya CCM kumwengua kuwania uspika.
Lakini pia inaelezwa kuwa ni njia mojawapo ya kuupoza umma ambao umeonyesha kusikitika kwa kunyimwa nafasi ya Bunge, ili kurejeshea serikali yake imani kwa wananchi.
Sitta anakumbukwa chini kwa kuliendesha Bunge kwa kiwango cha hali ya juu na kuruhusu mijadala wazi na kuchangia kuibuka kwa kashfa ya Richmond ambayo ilitikisa serikali baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu kwa kuwajibika na pamoja n mawaziri wawili walioiongoza Wizara ya Madini na Nishari kwa nyakati tofauti wakati wa mchakato kwa kuipitisha zabuni iliyoipa ushindi tata kwa Richmond.
Mijadala mingine ambayo ilitika nchi iliyojadiliwa bungeni ni wizi wa fedha za Mfuko wa Madeni ya Nje katika Benki Kuu (EPA) na mikataba mibaya katika sekta ya madini.
Habari kutoka Dodoma ambako kikao cha bunge kinaendelea zinaeleza kuwa gumzo kubwa sasa ni nani atateuliwa kuwa waziri mkuu.
Mtu mwingine ambaye anatajwa kuwa huenda akapewa nafasi hiyo kubwa ya utendaji wa serikali ni aliyekuwa Waziri wa Mifungo na Uvuvi, Dk John Magufuli ambaye anaheshimika kutokana na utendaji wake makini.
Magufuli ambaye ni Mbunge wa Chato mkoani Kagera ana rekodi nzuri ya kufanya vizuri katika wizara zote alizopangiwa na hana kashfa wala makundi ndani ya CCM.
Habari kutoka ndani ya serikali, zinaeleza kuwa pia Rais Kikwete anaelezwa huenda akafanya mabadiliko makubwa katika baraza lake la mawaziri ikiwamo kuunda baraza dogo la mawaziri ili kupunguza matumizi ya serikali na kuelekeza fedha nyingi kwenye shughuli za maendeleo.
Katika serikali iliyopita, Baraza la Mawaziri lilikuwa na mawaziri 27 pamoja na manaibu mawaziri 21.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa watu waliokaribu na washauri wa Rais Kikwete zinasema safari hii amekusudia kuunganisha baadhi ya wizara na kuunda zisizozidi 20.
Mkakati huo umeelezwa kwamba utafanywa ama kwa kuunganisha wizara au kuvunja na idara zake kuziweka chini ya wizara nyingine zinazolingana nazo kiutendaji.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Rais Kikwete alijaribu kupangua baadhi ya wizara na kuhamisha baadhi ya idara kwa lengo la kuchochea ufanisi.
Miongoni mwa marekebisho aliyoyafanya kuisambaratisha iliyokuwa wizara ya Kilimo na Mifugo na kuzaa tatu, kilimo, chakula na ushirika, maji na umwagiliaji na maendeleo ya mifugo na uvuvi.
Rais Kikwete alifuta wizara mipango na Uchumi ambapo idara zilizokuwa zinahusiana na uchumi zilipelekwa kuwa chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ikawekwa chini ya ofisi yake.
Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya juu pia ilisambaratishwa na Idara za Elimu ya juu kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi huku Teknolojia ikiunganishwa na Mawasiliano.
You Are Here: Home - - Homa ya Waziri Mkuu yapanda Pinda, Sitta, Magufuli watajwa uwaziri mkuu
0 comments