Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda mara baada ya kuapishwa bungeni jana |
SPIKA wa Bunge, Anna Makinda, amewaonya wabunge kuwa hatakubali Bunge liendeshwe kwa hoja za watu au kundi fulani la watu kutoka nje, ambao wana masilahi binafsi, bali litaendeshwa kwa kufuata matakwa ya wananchi.
Kauli hiyo ameitoa jana bungeni wakati akitoa shukurani za kuchaguliwa kukalia kiti hicho baada ya kumbwaga mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando, ambaye alipata kura 53 dhidi ya 265 za Makinda.
Makinda ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuwa Spika wa nane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, alisema Bunge halitatumiwa na mtu, kundi la watu fulani walio ndani au nje ya Bunge kupitisha hoja zao kwa masilahi binafsi.
Alibainisha kuwa ni vema wabunge wakalifanya Bunge kuwa sehemu ya kujadili matatizo na matakwa ya wananchi waliowapa ridhaa ya kuwawakilisha kupitia masanduku ya kura.
“Sitakubali wabunge walifanye Bunge liwe sehemu ya kujadili hoja za watu fulani kutoka nje ya Bunge, nataka Bunge liwe moja na imara kwa faida ya Watanzania wote,” alisema.
Makinda alibainisha kuwa Spika aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta, alifanya kazi nzuri na yeye ataendeleza mazuri yote yaliyopatikana katika uongozi wake, ikiwamo mabadiliko ya kanuni ambazo zimechangia kukua kwa demokrasia miongoni mwa wabunge kwa kuwa huru kutoa mawazo yao.
Aliongeza kuwa wakati wa utawala wa Sitta, alikuwa na kaulimbiu ya ‘Kasi na Viwango’ lakini yeye amekuja na kauli mbiu ya ‘Bunge moja, imara na uwakilishi wa kweli wa wananchi.’
Onyo la Makinda kuwa Bunge halitakuwa sehemu ya kupokea na kujadili hoja za mtu au kundi la watu fulani, imesababishwa na malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya wabunge kwenye Bunge lililopita kuwa baadhi ya wabunge walikuwa wakitumiwa na makundi fulani ya watu wenye nguvu kiuchumi na ushawishi wa siasa za nchini.
Malalamiko hayo pia yalikuwa yakimtuhumu Spika wa wakati huo Sitta, kukubaliana na hoja hizo zilizokuwa zikidaiwa kulenga kuwavunjia heshima watu fulani.
Tanzania Daima ilidokezwa na baadhi ya wabunge kuwa Makinda atakuwa na wakati mgumu wa kuhimili vishindo vya upinzani pamoja na makundi yanayokinzana ndani ya CCM, ambayo yalichochewa kwa kiasi kikubwa tangu kuibuliwa kwa kashfa mbalimbali za ufisadi.
Wabunge hao walisema kauli hiyo ya Makinda kuwa Bunge halitatumika kujadili hoja zinazochochewa na watu kutoka nje kwa masilahi binafsi, inaweza isiwe ya vitendo iwapo juhudi za makusudi hazitafanywa kuyadhibiti makundi ya Wana CCM yanayokinzana.
Wakati huo huo, Spika wa Bunge aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta, alishangiliwa sana alipokuwa akienda kuapishwa na Spika Makinda, ambaye alikuwa naibu spika wakati wa utawala wake.
0 comments