Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sitta avunja ukimya • ASEMA MAKINDA NI MCHAPA KAZI, ANAWEZA

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter Maspika wastaafu wa Bunge la Tanzania Pius Msekwa na Samwel Sitta wakipeana mikono nje ya Bunge baada yaa kumaliza jukumu la kumchagua spika 
ALIYEKUWA Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, ametuliza joto na uvumi ulioanza kuenea kuwa amekimbia vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya jina lake kuenguliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kutetea nafasi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sitta alivunja ukimya baada ya kusema katika siasa kuna mambo mengi, hivyo ni vema mwanasiasa ajiandae kwa lolote litakalomtokea.

Alisema chama kina maamuzi yake katika kuteua majina ya watu kuwania nafasi mbalimbali, hivyo hakuna sababu ya kuanza kumjadili yeye wakati anayekalia kiti hicho ni mtu mwingine.

Kuhusu kuchaguliwa kwa Makinda, Sitta alisema ana imani na Spika huyo kutokana na utendaji kazi wake, kwani amewahi kufanya naye kazi akiwa Naibu Spika mbapo alionyesha uwezo mkubwa.

Alisema uwepo wa wapinzani wengi bungeni kuliko kipindi chochote hakuwezi kuleta ugumu kiutendaji kutokana na kuwepo kwa kanuni za Bunge ambazo ndiyo muongozo wa shughuli zote za Bunge.

“Kwa uzoefu alionao Makinda, nina imani ataweza kuliendesha Bunge kwa umahiri mkubwa, hasa katika kipindi hiki chenye vijana wengi,” alisema Sitta.

Alimpongza Makinda kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo kubwa katika mhimili mmoja wapo wa nchi na hilo linaonyesha kuwa wanawake wanaweza kuongoza kama wakipewa nafasi.

“Sina wasiwasi na utendaji wake, najua atakabiliana na changamoto kubwa lakini kwa uimara wake tutafika sehemu nzuri bila kujali itikadi za vyama,” alisema Sitta.

Sitta juzi hakuwepo kwenye mkutano wa kamati ya wabunge wote wa CCM, ambao ulifanya uchaguzi kwa wagombea watatu waliokuwa wakiwania nafasi ya uspika.

Kutoonekana kwa Sitta, katika uchaguzi huo, kulizusha uvumi mkubwa kuwa mbunge huyo wa Urambo Mashariki ana mpango wa kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Uvumi huo ulishamiri zaidi juzi pale Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri wa CHADEMA, John Mrema, alipowataka waandishi wa habari wafanye utafiti kujua alipo Sitta, badala ya kukurupukia mambo.
Tags:

0 comments

Post a Comment