IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Maspika wastaafu wa Bunge la Tanzania Pius Msekwa na Samwel Sitta wakipeana mikono nje ya Bunge baada yaa kumaliza jukumu la kumchagua spika mpya mjini Dodoma
UTEUZI wa Anna Makinda kuwa spika wa Bunge la kumi umepokewa kwa hisia tofuati huku wabunge, wananchi na taasisi kadhaa zimemtaka kutokubali kutumiwa na kikundi cha watu kwa maslahi binafsi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema Makinda anatakiwa kuwa imara na makini katika utendaji wake, kwani atakumbana na changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe(Chadema) alisema Makinda ana uwezo mkubwa kuliongoza bunge, lakini anatakiwa kuendeleza mazuri ya bunge lililopita na kuweka ushabiki wa vyama pembeni ili aweze kuwatendea haki wabunge wote.
Mbowe ambaye ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni alitaja moja ya changamoto za Bunge hilo kuwa ni mwendelezo wa vita ya mafisadi kutoka kwa wapinzani.
Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda alisema hana shaka na uwezo, utendaji wa Makinda isipokuwa anatakiwa kufuata nyayo za mtangulizi wake, Samuel Sitta.
“Huyu mama ni mzuri sana, lakini najua asipokuwa makini lazima CCM wataingilia utendaji wake. Jambo hilo litaharibu kabisa na kuondoa mwelekeo wa sura ya bunge, hivyo ninamtaka asimame imara katika hilo kama alivyokuwa mtangulizi wake,” alisema Shibuda.
Mbunge wa Mkanyageni kwa tiketi ya CUF, Habibu Mnyaa alimtaka Spika huyo kufanya kazi kwa nguvu zote ili aweze kufuta minong’ong’o kuwa alichaguliwa kwa hila na shinikizo la wakubwa wa CCM.
“Namshauri aendeleze mema na mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake kwani kuna ming’ong’ono kutoka kwa baadhi ya watu wanaodai kuwa ameingia kwa kazi maalumu hivyo afanye kazi ili aweze kuziba mapengo hayo,” alisema Manyaa.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Mafulila (NCCR-Mageuzi) alimtahadharisha spika huyo kuwa lazima atakutana na changamoto za vijana ambao kwa sehemu kubwa wanahitaji mageuzi.
Kafulila alimtaka Spika kuondoa u-CCM ndani ya vikao vya bunge ili aweze kutenda haki kwa watu wote na akamtaka afuate nyayo za mtangulizi wake ambaye alijenga heshima kubwa ndani ya bunge na nchi kwa ujumla.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema hataki kuamini kwamba Makinda anaweza kutumiwa na chama chake kuminya uhuru wa wabunge na kukiuka maslahi ya umma na kwamba, ikiwa hivyo wananchi hawataruhusu.
“Naamini CCM haiwezi kumburuza Makinda na kama ikifikia hali hiyo, Watanzania tuko macho hatudanganyiki tena hivi sasa. Lakini haiwezekani kuburuzwa kwa sababu anaongozwa na kanuni za bunge na sio za CCM,” alisema Dk Bana.
Alisema hana wasiwasi na Makinda na kwamba, Watanzania wamepata Spika mzuri kwa sababu ana uzoefu, busara na hekima katika utendaji wake na kwamba ni mtu wa kanuni.
“Hofu yangu ni kwamba, sina uhakika kama Makinda ana uwezo wa kutosha kuhimili mikiki ya Bunge la vyama vingi, lakini kiuzoefu, busara na hekima tumepata Spika,” alisema Dk Bana.
Alisema tatizo lililomwangusha Sitta ni kwamba, alijitambulisha wazi kuwa yumo katika kambi ya wabunge wa CCM, wanaoendesha mapambano dhidi ya wabunge wenzao wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali.
Alisema ingawa hilo haliko wazi lakini kila Spika anakuwa mtiifu na makini kwa chama na serikali ya chama chake, jambo ambalo Spika Sitta alionekana kulikiuka.
“Hili lilimwondolea sifa ya mamlaka ya kimaadili l Sitta kuwa Spika, kwa sababu hakuwa tena spika wa wabunge wote bali alikuwa wa kundi la wabunge wapambanaji,” alisema Dk Bana.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) Dar es Salaam Profesa Mwesiga Baregu alisema: “Hofu yangu na Watanzania wengi ni uwezo wake wa kiutendaji na kukabiliana na shinikizo la CCM la kuzima mijadala ambayo wananchi watakaohoji maswali mazito kuhusu uwajibikaji wa serikali".
Hata hivyo, Profesa Baregu alielezea masikitiko yake kwa kitendo cha mchakato wa uteuzi wa mgombea wa Uspika uliofanywa na CCM ambao ulimtupa nje Spika aliyemaliza muda wake Samuel Sitta.
“Spika Sitta alichangamsha bunge na kuwaruhusu Watanzania kujenga ujasiri wa kuhoji masuala mazito kuhusu uwajibikaji na uadilifu wa serikali,” alisema Profesa Baregu na kuongeza:
“Kitendo chake cha kuruhusu mijadala bungeni kilisaidia sana kuongeza na kunyanyua sauti ya upinzani bungeni, hadi leo hii tunashuhudia idadi kubwa ya wabunge kutoka vyama vya upinzani.”
Kwa upande wake, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimempongeza spika huyo mpya na wanawake wengine waliochaguliwa kuwa wabunge na kuwaasa kuwa wawe wabunifu, waadilifu na jasiri katika kulitumikia Taifa.
Makinda alichaguliwa jana na bunge kushika nafasi ya Spika wakati ambapo bunge la wakati huu limeongeza nafasi za wabunge wa viti maalumu kutoka 75 hadi 104.
Hii ni mara ya kwanza mwanamke kuchaguliwa kuongoza bunge ambalo ni moja ya mihimili mitatu ya dola. Mihimili mingine ni Serikali na Mahakama.
Mkurugenzi mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya alisema jana katika taarifa yake kuwa viongozi wanawake waliochaguliwa, wanatakiwa kujiwekea malengo ya kuwatumika kwa bidii wananachi wote.
Nkya alisema, Makinda ni mwanamke mwenye busara, msimamo thabiti, hekima na ujasiri na kuwa atatoa uongozi mpya wenye mtazamo wa kijinsia unaojali zaidi maslahi ya Taifa na wanachi kwa ujumla.
“Tuna imani kuwa bunge hili jipya chini ya uongozi wa mwanamke litaonyesha mfano kwa vitendo kwamba katika mfumo wa vyama vyingi vya siasa inawezekana kuweka mbele maslahi ya wananchi na taifa kuliko maslahi ya vyama vya siasa au viongozi,” alisema Nkya na kuongeza:
“Spika huyo atajenga mazingira mazuri yatakayoliwezesha bunge hilo kufanikisha taifa na kupata katiba mpya ambayo pamoja na mambo mengine, itachochea uwajibikaji wa viongozi katika ngazi mbalimbali.”
Habari hii imeandaliwa na habel Chidawali, Dodoma, Salim Said na Minael Msuya, Dar
You Are Here: Home - - Wadau wamchorea ramani Makinda
0 comments