IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Spika mpya wa Bunge, Anna Makinda akiongozwa na Askari wa bunge kuingia bungeni mjini Dodoma jana baada ya kuchaguliwa na wabunge wengi kushika wadhifa huo. Picha na Edwin Mjwahuzi
BAADA ya wabunge kumchagua kwa kishindo Anna Makinda kuwa Spika wa Bunge la kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta amemtaka kuwa makini kwa kuhakikisha kwamba, chombo hicho cha kutunga sheria hakipotezi mwelekeo kutoka mahali kilipofikia kidemokrasia.
Makinda ambaye ni mbunge wa Njombe Kusini, alichaguliwa jana kwa kura 265 ambazo ni sawa na asilimia 74.2 ya kura zote zilizopigwa (327), huku mpinzani wake Mabere Marando akiambuliwa 53 (asilimia 16.2) na kura tisa ziliharibika.
Baada ya matokeo hayo, Spika Makinda aliwashukuru wabunge kwa kumchagua kwa kura nyingi ambazo alisema anaamini zimeonyesha kuwa wabunge wengi wamemkubali. Aliahidi kuwa atafanya kazi ya uspika kwa kuzingatia misingi na kanuni za bunge.
“Nitajitahidi kuzielewa kanuni za bunge pamoja na ninyi waheshimiwa wabunge, hivyo naomba mzisome na kuzielewa vema sheria za Bunge letu tukufu ili kusiwe na mgongano wa kimaslahi,” alisema Makinda.
Spika huyo alisema atajitahidi kulifanya bunge liwe moja, bora, imara na liwe la watu wote kwa kuanzisha utaratibu wa vipindi katika vyombo vya habari ikiwemo radio ambavyo vitawawezesha wananchi kuzielewa kanuni za Bunge.
Aliwaonya wabunge kwamba hatakiwi kupeleka ndani ya bungeni hoja zenye maslahi binafsi au kwa kutumiwa na mtu au vikundi vya watu na kusisitiza kuwa wapeleke bungeni hoja zinazotoka katika majimboni yao.
"Kitakachozingatiwa humu bungeni ni sheria, kanuni na taratibu hatuwezi kuingiza bungeni mambo yanayobeba maslahi ya watu fulani au vikundi, hivyo msome na mzielewe kanuni za Bunge," alisisistiza.
Akitoa mchango wake kuhusiana na kuchaguliwa kwa Makinda, Sitta ambaye alijizolea umaarufu kwa kuliongoza Bunge lililopata umaarufu kutokana na kuruhusu mijadala ya wazi, alimtaka spika huyo kutoyumbishwa katika kipindi chote cha uongozi wake.
Alibainisha kuwa hivi sasa wananchi wameelevu zaidi kwani wanafuatilia kwa umakini masuala ya Bunge, hivyo wanahitaji kuona vitu vizuri na haki ikitendeka ndani ya chombo hichi. Alishauri kuwa viwango na msimamo waliokuwa wameufikia katika Bunge la Tisa unafaa kuendelezwa.
Sitta alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nje ya Viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Alisema hana shaka na uwezo wa Makinda, lakini alibainisha kuwa Bunge la Kumi lina changamoto kubwa kuliko mabunge yote yaliyotangulia katika historia ya Tanzania.
“Mimi nadhani ataweza kumudu vema kazi hiyo, ila ninamtahadharisha kuwa asiwe na msimamo wa kuyumbishwa na wala asiwe na upendeleo na ikibidi, afuate nyayo zangu naamini kuwa bunge litakuwa na heshima kubwa,” alisema Sitta.
Mbunge huyo wa Urambo Mashariki alisema Bunge la Kumi lina wasomi wengi ambao wengi wao ni vijana na hivyo ni bunge bora kuliko yaliyotangulia.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo litakuwa na mijadala mizito yenye changamoto nyingi linalomlazimu Makinda kuwa makini zaidi katika majukumu yake.
Akizungnza kwenye ukumbi wa Spika baada ya kuanza rasmi kazi hiyo, Makinda alisema hatatumia nafasi hiyo kumsafisha mtu yeyote anayetaka kugombea urais kama watu wanavyodai.
Pia alisema kuwa hajawekwa kwenye uspika na mafisadi, ila alisimama mwenyewe kwa kuwa aliamua kugombea nafasi hiyo.
"Kuwa spika ni ratiba ya maisha yangu, ni kitu ambacho nilikuwa nakifikiria na mimi ni mtu wa kufuata taratibu. Kwanza sijui kama kuna mafisadi kwa kuwa fisadi ni mwanaume anayeiba mke wa mtu," alisema Makinda.
Kuhusu uendeshaji wake wa bunge alisema kuwa hatakubaliana na hoja za kukomoana bali atahitaji hoja zilizofanyiwa utafiti ili maamuzi yanapotolewa yaweze kuleta tija.
Alisema siasa si za kuzua maneno tu lazima hoja ziwe za kitafiti na ni lazima wabunge wawe na uwezo wa kuibua mambo ili kazi iwe nzito.
"Nasikitika kuwa bunge lililopita lilikuwa na hoja nzito moja tu ya Richmond, zilitakiwa ziwe zaidi ya kumi kama hizo ili bunge liwe na nguvu zaidi,"alisema Spika huyo ambaye katika bunge lililopita alikuwa Naibu Spika akimsaidia Sitta.
Makinda alisema katika bunge hili atatoa kipaumbele kwa huduma za wabunge na wafanyakazi wa bunge kuwa bora zaidi na kutoa elimu kwa wabunge iliwaweze kuzielewa kanuni vizuri.
You Are Here: Home - - Sitta ampa changamoto Makinda
0 comments