IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Rage amesema wamechoshwa na tabia ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri kuhusu kuchelewa mara kwa mara kuripoti mara aendapo kwao Zambia.
Akizungumza kwa simu jana kutoka Tabora, Rage alisema kocha huyo anaporuhusiwa kwenda kwao Zambia anakuwa msumbufu kurudi Dar es Salaam kuendelea na kazi yake.
“Hali hii si kwa uongozi wangu, bali hata awamu nyingine zilizopita amekuwa hivi, inasikitisha sana kwamba wakati mwingine timu inamhitaji lakini hajali hilo. “Nimemuandikia barua kumtaka ajieleze kwa nini tusivunje mkataba wake, maana inaonekana hayupo tayari kuitumikia Simba. “Pia nimeshampa kazi mwanasheria mmoja aupitie mkataba wake na Simba tuone kama tunaweza kuuvunja, kwani tumechoshwa kila siku na hii tabia yake,” alisema Rage.
Aliwaomba mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi kwani kocha Syllersaid Mziray ambaye amechukuliwa kama kocha wa viungo ana historia nzuri ya ufundishaji.
“Nimefanya kazi na Mziray wakati nikiwa FAT (Chama cha Soka Tanzania sasa TFF), amefanya mambo mengi mazuri, hivyo ile pia ni lulu ambayo Simba tumeipata. “Hatuwezi kuendelea kumvumilia kocha ambaye kila siku anatoa sababu zisizo kuwa na msingi,” alisema Rage na kuongeza kuwa mara kwa mara wanapowasiliana na Phiri amekuwa akiwaeleza atakuja kesho.
Phiri alienda kwao Zambia kwa mapumziko baada ya kumalizika michuano ya Kombe la Kagame Mei mwaka huu mjini Kigali, Rwanda.
Lakini karibu wiki mbili sasa klabu ya Simba imeanza mazoezi kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Agosti 21 pamoja na mchezo dhidi ya Yanga kuwania Ngao ya Jamii utakaofanyika Agosti 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bado kocha huyo hajawasili nchini.
Viongozi wa Simba mara kwa mara wanapoulizwa kuhusu ujio wa Phiri husema kuwa amewaeleza atakuja ‘kesho’, ingawa hakuna mafanikio yoyote.
Juzi Phiri alikaririwa na gazeti moja la michezo hapa nchini akisema kuwa ana matatizo binafsi ambayo hayahusiani na Simba na kuwa pindi yakimalizika atakuja Dar es Salaam kujiunga na timu hiyo.
Simba ililazimika kucheza na Yanga Aprili 18 mwaka huu katika mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilioshinda mabao 4-3 bila kuwa na Phiri ambaye alienda kwao Zambia na kuchelewa kurudi.
Wakati huo huo, Rage alisema timu hiyo ilitarajiwa kuondoka jana jioni kwenda Zanzibar kuweka kambi kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Alisema kambi hiyo ni maandalizi kwa ajili ya mchezo huo ambao wameuchukulia uzito wa aina yake.
You Are Here: Home - HABARI ZA MICHEZO - Simba wamchoka Phiri
0 comments