Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Viongozi wa dini wapinga muswada

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter * Zitto aunga mkono, kuwashawishi wabunge waukatae

Na Frederick Katulanda, Dodoma

WAKATI serikali inatarajiwa kuwasilisha muswada wa Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010, viongozi wa dini ya Kikristo na Kiisalamu wamejiandaa kuupinga muswada huo na kuwashawishi wabunge kuukataa.

Viongozi dini ya ambao tayari wapo mjini Dodoma ni kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (Tec) pamoja na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili viongozi hao, walisema muswada huo ni kiini macho na kwamba, hauna dhamira ya dhati kuwawezesha Watanzania kunufaika na madini ambayo wametunukiwa na Mungu.

Afisa Mawasilino na Habari wa Jumuiya ya Kikrsto Tanzania (CCT), Mchungaji John Magafu akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini jana, alisema muswada huo hauna maslahi kwa taifa na kwamba, unakimbizwa haraka bungeni ili upitishwe ili kuwafurahisha wawekezaji hao.

“Sisi tunapinga kupelekwa muswada huu kwa haraka namna hiyo bungeni. Haraka ya nini wakati nchi hii ni yetu sote, tunataka tupatiwe muda wa kuchambua zaidi na kushirikisha watanzania wote.

"Madini ni mali ya watanzania wote tunataka muswada huu uendelee kujadiliwa zaidi ili uborehswe na kuwa wenye manufaa kwa taifa,” alisisitiza mchungaji Magafu.

Kuhusu upungufu uliyopo katika muswada huo, Mchungaji Magafu alisema ingawa muswada huo umeongeza tozo la mrahaba kutoka ailimia 3 hadi asilimia 4 kwa dhahabu, bado hauonyeshi kuwanufaisha wananchi wa maeneo yanayotoka madini hayo.

“Sheria hii ukiiangalia juu juu unaweza kusema nzuri, lakini haina uzuri wowote kwa vile katika mabadiliko hayo kuna upendeleo.

"Kwa mfano, ongezeko la mrahaba kampuni mpya ndizo zitakazotozwa na kuziacha zilizopo," alisema Magafu na kuhoji:

"Karibu eneo kubwa la madini limeishatolewa kwa wawekezaji, hao wapya watawekeza wapi ili tupate faida”.

Mbali ya viongozi wa dini, habari zaidi zimeeleza wabunge wengi wamejiandaa kuupinga muswada huo jambo ambalo lilimshitua Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye Ijumaa iliyopita alizungumza na waandishi wa habari kuutetea muswada huo.

Ngeleja alisema muswada anaokusudia kuuwasilisha bungeni wiki ijayo umezingatia mabadiliko makubwa katika maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwenye sera ya madini ya mwaka 1997 pamoja na sheria ya madini ya mwaka 1998.

Hata hivyo, Magafu alidai hata madini ya 'uranium' yatalayoanza kuchimbwa katika maeneo mbalimbali, tayari nayo yameshamilikiwa na kampuni zilizopo, hivyo uwezekano wa taifa kunufaina na madini hayo unabakia kuwa ndoto.

Alisema: “Eneo lingine ambalo halikuzingatiwa katika muswada huo ni namna ya kufanya tathmini ya athari za kimazingira. Katika sheria hii inaelezwa kuwa mgodi ndiyo utaajiri kampuni ya kufanya hivyo jambo ambalo viongozi wa dini tunapinga. Tunataka iwe chini ya taasisi huru ili waweze kubanwa wawekezaji hawa”.

Alitoa mfano akisema Mgodi wa North Mara wakati ilipotokea athari ya maji machafu, tathmini iliyofanywa na mgodi huo ilionyesha hakukuwa na athari za kimazingira hii ni inatokana aliyeifanya alikuwa wakilipwa na kampuni ya Barrick jambo ambalo lisingekuwa rahisi kujimaliza wenyewe.

Mchunaji Magafu alisema kutokana na mapungufu hayo tayari viongozi wa dini wameunda jopo la wanasheria ambao wanauchambua muswada huo kwa kina ikiwa ni pamoja na kuuandaa kwa lugha ya Kiswahili ili uweze kusomwa na watu wote.

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akizungumia muswada huo alisema anajiandaa kuupinga vikali iwapo utaletwa ukiwa hauna mapendekezo muhimu ya kuwanufaisha wananchi.

Alisema katika kuhakikisha unakuwa na nguvu ya pamoja atawashirikisha wabunge wote wanaotoka katika maeneo ya madini, ili kuwaomba waungane kwa maslahi ya taifa kuwa kitu kimoja kuupinga muswada huo, mpaka hapo serikali itakapokubali kuacha fedha za mrahaba katika wilaya inayochimbwa madini hayo.

Alisema katika mapendekezo ya kamati ya Jaji Mark Bomani walishauri kwamba, katika kuwashirikisha wananchi wa maeneo ya madini, serikali iwarudishie asilimia 20 katika wilaya zao ili ziweze kutumika katika miradi ya maendeleo yao, lakini serikali imegoma.

“Serikali imegoma, hii inaturudisha kule kule tulikokuwa na hakuna haja ya kuwa na sheria mpya kama haya yatazingatiwa,” alieleza.

Alisema hoja ni kuwanufaisha watu na madini yao, na kufafanua kuwa mwaka 2008/2009 serikali ilikusanya mapato katika sekta ya madini kiasi cha Sh 162 bilioni ambacho ni sawa na asilimia 16 ya mauzo yote ya nje, kati yake Sh57 bilioni zilikuwa ni mrahaba.

Alisema kiasi hicho kilipaswa kurudi kwa wananchi, lakini serikali inakataa na jambo hilo halikuzingatiwa katika muswada huo.

“Tunataka sehemu ya fedha hizo za mrahaba zirudi kwa wananchi na nyingine zianzishe mfuko wa serikali kwa ajili ya kusaidia kutengeneza barabara na mambo mengineyo. Serikali imegoma, tutaupinga muswada huu bungeni.” alieleza Zitto.

Alisema kutokana na upungufu huo na mengine atasimama kidete kuhakikisha anapinga muswada huo ikiwamo kuwashirikisha wabunge wengine kutoka maeneo ya madini.

Zitto alisema kesho anajiandaa kuzungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma kuelezea kasoro zilizopo katika muswada huo.

Ngeleja alisema kuna watu wanadai eti hata kuwasilishwa kwa muswada huu bungeni kwa hati ya dharula ni makosa.

Aliongeza kuwa kumekuwa na hofu kwa wadau wa sekta ya madini kuhusiana na muswada huo, wakidhani unaweza kuwa na mambo mazito.

Ngeleja alisisitiza muswada huo umezingatia mapendezo ya wadau wapatao 132kutoka taasisi, asasi na wachimbaji wadogo wa maeneo mbalimbali.
Tags:

0 comments

Post a Comment