Mtikila sasa kusambaza waraka wake nje ya nchi | |||||||
Akizungumza nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Slaam jana, Mtikila alisema waraka huo utasambaswa kwa waumini wa dini zote wa ndani na nje ya nchi ili wausome na baadaye kutoa maoni kama kweli unachochezi. Mtikila ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), alisema anaendelea kushangazwa na hatua ya serikali kuuona waraka huo kuwa ni wakichochezi na kwamba hawezi kuvumilia kuona nchi ikichezewa. Alisema waraka huo sasa utatafsiriwa katika lugha za kimataifa na kusambazwa katika mbalimbali wananchi wa huko wajue yanayoendelea nchini. “Siwezi kuvumilia kuona nchi ikichezewa. Nimefikia uamuzi wa kuuboresha waraka huu unaosemekana kuwa ni wa kichochezi juu ya Rais Jakaya Kikwete na wengine na sasa utatafsiriwa kwa lugha mbalimbali za kimataifa ili watu wausome na kutoa maoni yao kama ni wa uchochezi au la," alisema Mtikila. Alisema ataendelea na hatua hiyo akiamini kuwa hawezi kutiwa hatiani kwa kosa la kuandika waraka huo huku akirejea kusema kwamba iwapo akiendelea kufuatiliwa nchi itakumbwa na mabadiliko makubwa ya uongozi. Hata hivyo, Mtikia alisema hata akishtakiwa haogopi mahakama kwa kuwa ameshashtakiwa mara nyingi tangu mwaka 1988 na kwamba kwa sasa ana jumla ya kesi tofauti 46 kati ya kesi hizo ni moja pekee aliyomweka gerezani. "Siogopi mahakama kwani tangu mwaka 1988 nimeshashtakiwa kesi 46 na kesi moja tu ndio iliyoniweka ndani," alisema. Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa DP ametangaza nia yake kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao kama mgombea binafsi. Alisema kuwa katika uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba mwaka huu amejipanga kuchukua fomu ya kugombea urais huku akimtaka Rais Jakaya Kikwete kujiandaa kukabiliana naye. “Lazima Rais Kikwete ajiandae kwa kuwa mimi haniwezi. Katika siasa mimi nina uwezo, naamini hivyo kwa kuwa nina roho ya Kristo ndani yangu,"alisema Mtikila. Juzi Mtikila pamoja na kueleza sababu za kuandika waraka huo, alieleza kuwa kukamatwa kwake kulitokana na viongozi aliowatuhumu kupata presha ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini Mwezi Oktoba mwaka huu. Alisema kuwa udini ni jambo la kuogopa na kwamba hata ibara ya 26 ya katiba inasema kuwa ni lazima kuheshimu mamlaka yeyote katika nchi kutunga sheria au kufanya jambo lolote kwa ajili ya kupendelea kikundi fulani cha dini. |
You Are Here: Home - - Mtikila sasa kusambaza waraka wake nje ya nchi
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments