Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - WIZI KWA NJIA YA MTANDAO: Gavana ayashukia mataifa ya Ulaya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ameyajia juu mataifa ya Ulaya akidai kuwa yamekuwa chanzo cha kukwamisha utekelezaji wa udhibitiwa wa fedha chafu.
ADAI YANAKWAMISHA UDHIBITI WA FEDHA CHAFU

Ramadhan Semtawa

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ameyalamu baadhi ya mataifa ya Ulaya kwamba, yanaficha siri za watu wanaoweka fedha zenye harufu ya uhalifu kwenye benki zilizoko katika nchi hizo.

Profesa Ndulu aliliambia gazeti hili jana kuwa tabia hiyo inapunguza kasi ya kukabiliana na matukio ya uhalifu kwenye sekta ya fedha nchini.

Kauli ya gavana Ndulu, inakuja kipindi ambacho kumekuwa na taarifa mbalimbali za uhalifu wa kutumia mtandao nchini ikiwemo kutorosha fedha katika maeneo mbalimbali ya ndani na baadhi ya watu kuweka fedha zao nje ya nchi bila kuingia kwenye rekodi za akiba ya fedha za kigeni BoT.

Wakati Profesa Ndulu akitoa kauli hiyo taarifa mpya zinaeleza kuwa kuna kigogo mmoja (jina tunalihifadhi)ameweka kiasi kinachodaiwa kuwa Sh9 bilioni kwenye benki moja nchini Uingereza.

Profesa Ndulu alipoulizwa kuhusu kiasi hicho kama kimo kwenye rekodi ya fedha za kigeni halali zilizomo kwenye rekodi ya BoT, alijibu: "Hapana, hilo sijalisikia popote, hiyo taarifa sina...lakini unajua kuna tatizo kwa wenzetu."

Lakini, vyanzo vya habari ndani na nje ya serikali, vinasema tayari fedha hizo zimeanza kustua mamlaka za ndani za Uingereza ambazo zimeanza kuomba taarifa za uhalali wake kutoka mamlaka za Serikali ya Tanzania.

Kuhamishwa kwa kiasi hicho kunakuja kipindi ambacho pia mabenki matatu makubwa nchini yakiwa yamekumbwa na wizi mkubwa wa fedha zinazoelezwa kufikia Sh300 bilioni ingawa vyombo vya usalama na BoT vimekuwa vikikana kuwepo tukio hilo kubwa.

Fedha za amana za mabenki yote nchini zilizopo ni Sh7.8 trilioni kiasi ambacho ni kikubwa na kinachodhihirisha uwezekano wa mabenki hayo matatu makubwa, kuweza kuibiwa kiasi hicho cha fedha bila athari zake kuonekana mapema na kwa urahisi.

Lakini, mkuu huyo wa taasisi ya fedha nchini pasipo kutaja jina la nchi yeyote, akizungumzia suala zima la kupambana na utoroshaji wa fedha nje ya nchi bila rekodi za benki hiyo, alisema: "Tatizo wenzetu hawa huwa hawatoi taarifa za kutosha kutuwezesha kufuatilia akaunti za watu kwenye benki zao kuona kama fedha zilizopo ni halali."

Alifafanua kwamba, yamekuwepo baadhi ya matukio, lakini kila yakifuatiliwa huwa vigumu mno kuweza kupata taarifa za siri za akaunti ya mteja kwenye benki zao kutokana na sheria na miiko yao.

"Wenyewe wanasema wana miiko na sheria zao, sasa ukiona mtu wanaanza kumfuatilia na kutoa taarifa zake labda atakuwa amehusika na uhalifu unaowahusu wao ndipo huanza kushirikiana," alisisitiza gavana Ndulu na kuongeza:

"Msione hivi, vyombo vyetu vinafanyakazi kubwa FIU (Financial Intelligency Unit) na sisi tunaweza kufuatilia kitu, lakini kuna ugumu wa kupata taarifa za kina na za kutosha kuhusu baadhi ya akaunti".

Profesa Ndulu alifafanua kuwa BoT ina mamlaka ya kuomba na kupatiwa taarifa za akaunti yoyote ndani ya nchi kama ina utata, lakini linapokuja suala la nje ya nchi hasa katika mataifa hayo ya Ulaya huwa ngumu kutokana na sheria zao.

Kwa mujibu wa Profesa Ndulu hiyo ndiyo sababu ya kuwapo shinikizo kubwa la asasi zisizo za kiserikali (NGOs) barani Afrika, kuomba mataifa ya Ulaya yasaidie kurejesha fedha zote za Afrika zilizoibwa na kufichwa kwenye benki zao.

Alidai kuwa mataifa hayo yamekuwa yakifurahia fedha zinazowekezwa kwenye benki zao ndiyo maana husita kutoa taarifa za kina na msingi kusaidia mbinu za kuchunguza uhalifu kwenye sekta ya fedha katika nchi za Afrika.

Alisema kama mataifa hayo hayatasaidia kutoa taarifa za msingi yanaweza kuweka ugumu wa kubana fedha zisizo halali zinazotoroshewa nje ya nchi.

Mataifa ya Ulaya ambayo yamekuwa yakipiga kelele za ufisadi yamekuwa yakilalamikiwa pia na wanaharakati barani Afrika kutokana na kuhifadhi mabilioni ya fedha zilizoibwa na viongozi au familia zao na wahalifu kisha kuwekwa kwenye benki zao na wanapogundua wanashindwa kuzirejesha.

Marais kama marehemu Jeneral Sanni Abacha wa Nigeria na Mobutu Seseseko, wanatuhumiwa kuweka kiasi kikubwa cha fedha kwenye benki za nchini Uswis na nyingine za Ulaya.

Abacha ambaye alifariki dunia mwaka 1998 akiwa madarakani alituhumiwa kuhifadhi dola za Marekani 1bilioni katika benki mbalimbali huko Uingereza, Marekani na Uswis.

Kwa upande wa Mobutu, katika nchi ya Uswis alibainika kuwa na dola 3.4milioni huku akituhumiwa kuwa na mamilioni ya dola nyingine katika akaunti za siri nchini humo na baadhi ya nchi za Ulaya.
Tags:

0 comments

Post a Comment