Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Dk. Slaa alipua bomu • ADAI MCHEZO MCHAFU UMEFANYIKA SHERIA YA UCHAGUZI

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter KWA mara nyingine, Rais Jakaya Kikwete, amepotoshwa ukweli kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi aliyoisaini hivi karibuni katika Ikulu yake jijini Dar es Salaam baada ya kubainika kuwa baadhi ya vipengele vimeingizwa kinyemela nje ya Bunge, Tanzania Daima Jumatano, imebaini.
Kipengele kilichoingizwa kinyemela bila kujadiliwa na kupitishwa na Bunge mjini Dodoma, ni kile kinachohusu uthibitishwaji wa wajumbe wanaounda timu za kampeni kwa ajili ya wagombea wa urais, ubunge na udiwani.
Wakati Bunge linajadili na kupitisha sheria ya gharama za uchaguzi, sehemu inayohusu uthibitishaji wa timu za wagombea ilijadiliwa na wabunge wote, lakini haikueleza nani anayepaswa kukagua timu za kampeni za wagombea wa nafasi mbalimbali, lakini katika sheria aliyosaini rais, inafafanua watu wanaostahili kukagua timu za kampeni.
Kwa mujibu wa sheria iliyosainiwa kwa mbwembwe na Rais Kikwete, kipengele kinachodaiwa kuchomekwa bila ridhaa ya Bunge, kinaonyesha kuwa timu za kampeni za wagombea urais, zitathibitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, timu za kampeni za wagombea ubunge, zitathibitishwa na Makatibu Tawala wa Wilaya wakati timu za kampeni za wagombea wa udiwani, zitakaguliwa na kuthibitishwa na Makatibu Tarafa.
Akizungumzia utata wa sheria hiyo, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, alisema anashangazwa na kilichotokea Ikulu siku ya kusaini mkataba huo, huku akitaka kujua nani aliyehusika kuongeza vipengere hivyo bila idhini ya Bunge.
Dk. Slaa alitoa ufafanuzi wa kasoro hiyo jana wakati wa semina ya kujadili kanuni zinazofafanua Sheria ya Gharama za Uchaguzi, iliyoandaliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.
Dk. Slaa, ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, alionyesha kitabu cha kumbukumbu za Bunge ‘Hansard’ ambacho haikuonyesha viongozi wanaopaswa kufanya uhakiki wa timu za kampeni za wagombea.
“Katika sheria aliyosaini rais kuna kifungu cha 7 (3), ambacho hakikuwepo kabisa kwenye muswada uliojadiliwa na kupitishwa bungeni. Kwa kweli nimeshangazwa sana kwa sababu rais amedanganywa katika hili.
“Bungeni hatukusema nani anatakiwa kukagua timu ya kampeni ya nani, lakini kwenye kipengele ambacho kimo kwenye sheria iliyosainiwa na rais inaonyesha kwamba timu za kampeni za mgombea urais zinatakiwa kuhakikiwa na Msajili.
“Timu za kampeni za mgombea ubunge, zinaonyesha zinapaswa kuhakikiwa na Makatibu Tawala wa Wilaya na kwa kesi ya wagombea udiwani, timu zao kampeni zinapaswa kukaguliwa na Makatibu Tarafa,” nani kaichomeka hii?” alihoji Dk. Slaa, huku wajumbe wengi wakipigwa na butwaa.
Alisema, haiwezekani timu za kampeni ambazo ndiyo kikosi cha ushindi cha mgombea yeyote, kukaguliwa na mtu wa nje ya chama chake, hususan anayetoka chama tawala, yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katibu huyo wa CHADEMA ambaye alikuwa mbogo wakati wa kujadili utata huo wa sheria hiyo, alisema kuna mchezo mchafu uliofanyika kwa lengo la kufifisha kambi ya upinzani nchini.
Dk. Slaa alifafanua kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa ni nafasi ya kuteuliwa na rais, hivyo kambi ya upinzani haitakuwa na imani kwa timu zake za kampeni za mgombea wao wa urais, zikaguliwe na mtu huyo.
Alisema si sahihi pia kwa Makatibu Tawala wa Wilaya au Makatibu Tarafa, kuzikagua timu za kampeni ya wagombea ubunge ama madiwani kwa vyama vya upinzani kwa kuwa watendaji hao ni makada wa CCM, hivyo haki haitatendeka.
“Hawa wenzetu wana mbinu nyingi hasa za kuwanunua wafuasi wa upinzani, hivyo kesho nikikubali timu yangu ya kampeni ikaguliwe na DAS (Katibu Tawala wa Wialaya), ni rahisi kwake kuniingizia mamluki...
“Unatakiwa kujua kwamba timu ya kampeni, ndiyo yenye mbinu zote za ushindi hivyo yanaweza kutokea kama yaliyonitokea mimi mwaka 2005, ambapo mmoja wa watu wangu wa kampeni aliyekuwa anaingia kwenye vikao vya siri alirubuniwa na CCM akanikimbia wakati tunakaribia uchaguzi,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema kwa mchezo mchafu huo uliofanywa na serikali, anakusudia kuchukua hatua za kisheria ili kumbaini aliyeingiza kipengele hicho kinachofinya uhai wa demokrasia kwa vyama vya upinzani nchini.
Machi 17 mwaka huu, taifa liliandika historia pale wabunge, wawakilishi wa vyama vya siasa, mabalozi, viongozi wa dini na wasomi mbalimbali walipokutana Ikulu ya Dar es Salaam kushuhudia utiwaji saini wa sheria ya gharama za uchaguzi uliofanywa na Rais Kikwete. Sheria hiyo itaanza kutumika kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu kidogo cha pili, kinaeleza maana ya timu ya kampeni kuwa ni kundi la watu lililoundwa na mgombea wakati wa zoezi la uteuzi lenye madhumuni ya kumwakilisha au kumsaidia mgombea kwenye kampeni za uchaguzi ambaye amepitishwa kuwania.
“(a) Kwa kesi ya urais watathibitishwa na Msajili, (b) Kwa kesi ya Mbunge watathibishwa na Katibu Tawala wa Wilaya na (c) Kwa kesi ya Diwani watathibitishwa na Katibu Tarafa...,” ilieleza sehemu ya sheria hiyo iliyosainiwa na Rais Kikwete ambayo nakala yake tunayo.
Muswaada huo wa sheria ulioasisiwa na Rais Kikwete mwenyewe, ulipitishwa kwa mbinde Februali 12 mjini Dodoma huku ukiibua malumbano makubwa baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, pamoja na wabunge wengine kuhusu vipengele mbalimbali vya muswada huo.
Mwanasheria Mkuu wa serikali alipingana waziwazi na Chenge aliyekuwa mwanasheria mkuu wa zamani hali iliyomlazimu Naibu Spika kuingilia kati mara kwa mara.
Muswada huo ulimlazimisha Mwanasheria wa Serikali kusimama kwa zaidi ya mara 11 kwa ajili ya kutoa ufafanuzi huku akitahadharisha kuwa yeye ni jaji, hivyo kuwataka wabunge kuwa watulivu baada ya kubaini kuwa baadhi yao walikuwa wakizungumza kwa sauti za juu wakati mwanasheria huyo aliposimama.
Wanasheria hao pamoja na wengine walikuwa wakibishania kifungu cha saba ambacho hakikuwa na ufafanuzi kuhusu gharama za watu wanaosaidia katika kampeni ambapo Chenge alitaka baadhi ya mambo yaongezwe ili kupanua wigo kwa wapiga kampeni hao katika kugharamiwa baadhi ya mambo ikiwemo chakula na malazi.
Chenge alitaka kifungu hicho kiwekwe kwani kwa mtazamo wake ni halali kwa mgombea kuwalisha na kuwagharamia watu ambao wanamsaidia katika kampeni jambo lililotafsiriwa vibaya na baadhi ya wabunge.
Wabunge wengine ambao walikuwa moto na muswada huo ni pamoja na Halima Mdee, Dk Slaa, na Peter Serukamba.
Tags:

0 comments

Post a Comment