Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Makao Makuu CCJ kuwa Mwananyamala

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAKATI kesho Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa akitarajiwa kutoa usajili wa muda kwa Chama cha Jamii (CCJ), taarifa zinaonyesha makao makuu ya chama yanarajiwa kuwa Mwananyamala.

Hatua ya CCJ kupewa usajili wa muda inakuja kipindi ambacho joto la siasa nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, likiwa juu.

Msajili wa Vyama Siasa John Tendwa akiweka bayana kwamba, atakuwa tayari kuhakiki wanachama wa CCJ hata ndani ya miezi mitatu wakimaliza kazi, taarifa zinasema tayari chama hicho kimeanza maandalizi makubwa.

Katibu Mkuu wa CCJ Renatus Muabhi, alithibitishia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kwamba, makao yao makuu yanatarajiwa kuwa Mwananyamala kama hakutakuwa na mabadiliko.

"Makao makuu yatakuwa Dar es Salaam eneo la Mwananyamala, tumejipanga vema kila kitu kiko vizuri tu hadi sasa tunaamini tutakwenda vizuri," alifafanua Muabhi.

Kwa mujibu wa Muabhi, CCJ itatangaza ofisi hiyo itakuwa mtaa gani kesho wakati wa mkutano na waandishi baada ya kupewa usajili huo wa muda na Msajili wa Vyama.

Muabhi alifafanua kwamba, chama kimejipanga vema katika kupanga safu ya uongozi imara ambao utawezesha kusukuma mbele ajenda za chama mara baada ya kuanza kukusanya wanachama.

"Baada ya kukusanya wanachama, tutapanga vema safu yetu ya uongozi kuanzia ngazi ya chini hadi makao makuu, tunachokifanya sasa ni kujiandaa kutimiza hilo la kukusanya wanachama," alisisitiza.

Kuhusu bendera, alisema bendera ya chama hicho siyo kama ya TANU kama ilivyoelezwa awali bali bendera ya chama hicho imefunikwa na rangi ya dhahabu.

CCJ ujio wake unaangaliwa na wadadisi wa mambo ya kisiasa kama tishio kwa CCM, kutokana na kutajwa kuhusisha vigogo wa chama hicho tawala ambao wanataka kujitenga na kugombea Urais hapo Oktoba.

Tayari Spika wa Bunge Samuel Sitta, aliwahi kusema kwamba, haoni tatizo la kusajiliwa CCJ huku pia akisema hawezi kuzuia watu kumhisisha na chama hicho kama mgombea hapo Oktoba.

CCJ imekuwa ikitikisa nchi tangu taarifa zake kuchapishwa kwenye vyombo vya habari, kwani kuna majina makubwa yanatajwa kuwemo akiwemo Spika Sitta, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, John Malecela, lakini wote wamekanusha.

Hata hivyo, mwasisi wa CCM Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuonya kwamba bila CCM madhbuti nchi itayumba na upinzani wa kweli ungetoka ndani ya CCM onyo ambalo wadadisi wa mambo ya siasa anaona kama linakaribia.
Tags:

0 comments

Post a Comment