IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MFANYAKAZI wa Wizara ya Nishati na Madini, Doroth Mtweve, amehamishwa kutoka makao makuu ya wizara hiyo baada ya kudaiwa kuvujisha siri za ofisi kuhusiana na sakata linaloendelea baina ya Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).
Mtweve ambaye alikuwa Katibu Muhtasi Daraja la Tatu katika ofisi hiyo, pia anadaiwa kuhamishwa katika ofisi hiyo na kupelekwa Ofisi ya Madini Kanda ya Mashariki, baada ya kugundulika kuwa ni muumini wa kanisa hilo linaloongozwa na Askofu Zakaria Kakobe.
Muumini huyo aliyekuwa Katibu ya Wizara ya Nishati na Madini alikabidhiwa barua hiyo Februari 22 mwaka huu na kutakiwa kuhama.
Habari za kuaminika ambazo Tanzania Daima imezipata zinaeleza kuwa Mtweve alikabidhiwa barua ya uhamisho Februari 22 mwaka huu yenye kumbukumbu namba Na . MEM/PF.216/52 iliyosainiwa na C.M Musika kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara.
Chanzo hicho kinaendelea kueleza kuwa mfanyakazi huyo anadaiwa kuvujisha baadhi ya barua zinazohusiana na mgogoro huo ambazo zimekwa zikimfikia askofu huyo bila wizara kuelewa.
Hata hivyo inadaiwa pamoja na barua hizo kufika kwa Kakobe, pia Mtweve amekuwa akionekana mara kadhaa akiwa amevaa fulana maalum ambazo huvaliwa na waumini wa kanisa hilo zenye maandishi ya kupinga upitishaji wa nguzo za umeme wa kilovolti 132. Fulana hizo kwa mbele zimeandikwa ‘TANESCO Muogopeni Mungu’ na ‘Badala ya Richmond sasa Mmeligeukia Kanisa’ kwa nyuma.
Habari hizo zinaeleza kuwa Februari 22 mwaka huu kabla ya kukabidhiwa barua ya uhamisho, Mtweve aliitwa na mkurugenzi wa masuala ya utawala aliyefahamika kwa jina moja la Musika na kumwomba amuulize swali aliloliita ‘chafu’.
“Huyu dada aliitwa na bosi wake ambaye alimuomba amuulize swali chafu, kuwa ni muumini wa kanisa gani, ndipo Mtweve alijibu kuwa anaabudu katika Kanisa la Askofu Kakobe lililopo Mwenge,” kilieleza chanzo hicho cha habari.
Chanzo hicho kieleza kuwa kitendo hicho kilimfanya mkurugenzi huyo kumweleza kuwa aliliita swali chafu kwa kuwa kazi haihusiani na masuala ya dini ya mtu na kumruhusu kuendelea na shughuli zake.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa baada ya dakika 10 toka Mtweve atoke ofisi za Musika ndipo alimfuata Katibu Mhtasi wake na kumtaka aonyeshe lilipo jalada lake la kazi.
“Huwezi kuamini lakini ndiyo ukweli; huyo dada amefanyiwa fitina kama siyo mtego, kwani baada ya kutoka ofisi za mkurugenzi alifuatwa na kuambiwa aonyeshe lilipo jalada lake la kazi wakifikiri atakuwa amelificha ndipo alipowaambia lipo kwa mhasibu wa wizara,” kilifafanua chanzo chetu.
Chanzo hicho kinaeleza kuwa ilipofika majira ya saa 10 siku hiyo hiyo, Mtweve alipewa barua ya uhamisho ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake.
“Ili kuimarisha kazi, imeamuliwa uhamishiwe ofisi ya Madini Kanda ya Mashariki. Upatapo barua hii unatakiwa kukabidhi kazi zako kwa mkuu wako wa kazi na kuripoti kwa Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Mashariki,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa kwa Kamishna wa Madini, Kanda ya Mashariki.
Tanzania Daima ilipowasiliana na Mtweve, alikiri kupewa barua ya uhamisho na kwamba ni kweli ni muumini wa Kakobe.
“Baada ya kuhamishwa na kwenda kuripoti bosi wangu mpya aliniuliza kwa nini nimekuwa nikivujisha siri za ofisi kwa Askofu Kakobe? Nilimjibu kosa langu ni kukubali kupeleka barua kwa watu, kwani mara kadhaa nimekuwa nikitumwa na kupeleka barua sehemu mbalimbali ikiwamo kwa Askofu Kakobe,” alisema.
Alisema baada ya siku chache alitakiwa kujieleza kwa maandishi kuhusiana na tuhuma hizo na kuongeza kuwa mpaka sasa bado hajaandika maelezo hayo.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, David Ngairo, kuzungumzia suala hilo, alishindwa kukubali wala kukanusha na badala yake kumtaka mwandishi wa habari hizi kumweleza ni wapi alikozipata taarifa hizo.
“Kwanza sina la kujibu, iwapo unataka nizungumze niambie aliyekuletea taarifa hizo ili niweze kujibu,” alisema na mwandishi alipokataa kumweleza alikopata habari hizo alikata simu.
Mgogoro wa Kakobe na TANESCO ambao umedumu kwa zaidi ya siku 60 sasa bado hatma yake haijajulikana licha ya Waziri William Ngeleja kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa wiki hii angeweza kutoa ripoti kamili kuhusu upitishwaji wa waya katika eneo hilo
You Are Here: Home - - Kakobe amponza muumini wizarani
0 comments