Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - KINYANG'ANYIRO UCHAGUZI MKUU: Zitto, Mbatia wajitosa ubunge Dar

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


Mbungewa Jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema),
Zitto Kabwe anayetarajia kugombea ubunge
katika jimbo la Kinondoni.



MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe anatarajia kugombea ubunge katika Jimbo la Kinondoni huku Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia akitarajiwa kugombea Jimbo la Kawe, yote ya jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam viongozi hao walisema wataweka hadharani nia zao za kugombea nafasi hizo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu baada ya wiki mbili.

Zitto aliliambia gazeti hili kuwa mbali na jimbo hilo pia wananchi wa majimbo ya Geita, Kahama, Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini wote wanamuhitaji ili awawakilishe.

"Hadi sasa nimekwishapokea maombi mengi kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Kinondoni, Kahama, Geita, Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini ili niwawakilishe bungeni," alisema Zitto.

Hata hivyo, Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema alisema hadi sasa bado hajafanya uamuzi rasmi wa jimbo gani kati ya hayo atakwenda kugombea.

Habari za Zitto kugombea Kinondoni ambako Iddi Azan wa CCM ndiye mbunge huenda zikatoa mshtuko kwa mbunge mwenzake wa Chadema, Suzan Lyimo ambaye pia inadaiwa analiwania jimbo hilo.

Zitto ambaye mwishoni mwa mwaka uliopita alitangaza kuachana na masuala ya siasa ili afanye kazi zake za kitaaluma alisema ameamua kuvunja msimamo wake huo kutokana na maombi ya wananchi kumtaka asiondoke katika medani ya siasa.

"Napenda kuchukua nafasi hii kutangaza kuwa nitagombea katika moja kati ya hayo majimbo ambayo wananchi wameniomba, lakini hadi sasa bado sijafanya uamuzi rasmi. Pia nimeuvunja msimamo wangu wa kujiondoa katika siasa kama nilivyotangaza awali, hii ni kutokana na maombi ya wananchi kutaka nibakie katika medani ya siasa," alisema Zitto.

Zitto alifafanua kwamba uamuzi wa kugombea moja kati ya majimbo hayo utategemeana na utafiti na uchunguzi ambao amekwisha uanza kuufanya kupitia watu wake maalumu pamoja na ushauri kutoka kwa viongozi wa chama chake, ndugu, jamaa na marafiki zake.

"Pamoja na kuhitajika katika majimbo hayo, siwezi kukurupuka na kutangaza tu kuwa nitagombea jimbo hili. Kwanza nimekwishaanza kufanya utafiti na uchunguzi wa kina katika hayo majimbo pia uamuzi wangu utategemeana na ushauri kutoka kwa viongozi wangu wa Chadema, ndugu, marafiki na jamaa zangu," alisema Zitto.

Zitto ambaye amerejea hivi karibuni kutoka nchini Ujerumani alikokuwa akisoma alisema wananchi wa Jimbo la Kinondoni wamemtaka kugombea jimboni humo ili aweze kupata muda mwingi wa kuwasaidia vijana nchini katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo katika siasa.

"Ukweli ni kuwa kugombea katika moja ya majimbo yaliyopo Dar es Salaam ni tofauti na majimbo mengine ya mikoani kutokana na kwamba ukiwa mikoani unahitaji muda mwingi kujipigia kampeni tofauti na Dar es Salaam ambapo anaweza kuwasaidia hata wanasiasa wengine ndani ya Dar es Salaam na mikoani pia," alisema.

Kuhusu jimbo la Geita na Kahama, Zitto alisema wananchi wa majimbo hayo wamemuhitaji kutokana na uwelewa wake wa mambo mengi yanayohusu sekta ya madini.

Katika Jimbo la Kigoma Mjini na la Kaskazini, Zitto alisema ni vigumu kuwaacha wananchi wa huko kutokana na kwamba ndiko alikozaliwa na kwamba wanamuumiza kichwa.

"Jimbo la Kigoma Mjini na lile la Kaskazini, yananiumiza kichwa kutokana na kwamba yote yapo nyumbani nilipozaliwa, lakini natumai uamuzi wangu nitakaoutoa utazingatia mambo muhimu na wananchi watahuheshimu na kukubaliana nami."

Tayari uongozi wa mkoa wa Kigoma, umemega eneo la Mwandiga la Kigoma Kaskazini ambalo Zitto anakubalika na kulipeleka Kigoma Mjini. Eneo hilo lililomegwa linadaiwa kuwa ngome kuu ya Zitto na kwamba hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kama sababu ya kuhamia Dar es Salaam.

Naye Mbatia alisema uamuzi wa kugombea katika Jimbo la Kawe unatokana na msingi wa kikatiba na haki ya kila Mtanzania ya kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi zozote.

"Uamuzi wangu umezingatia msingi wa kikatiba na haki ya kila mtu kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi zozote nchini, pamoja na utashi wa kisiasa nilionao," alisema Mbatia na kuongeza;"

"Nimechukua uamuzi huu mgumu kutokana na hali halisi ya mazingira ambayo yanahitaji kuwa na mgombea ambaye ataweza kuleta upinzani mkubwa dhidi ya CCM ili iweze kushindwa."

Kwa sasa Jimbo la Kawe linashikiliwa na mbunge wa CCM, Rita Mlaki. Hata hivyo, mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Halima Mdee alikwisha tangaza kwamba katika uchaguzi wa mwaka huu anawania jimbo hilo.

Mbatia alisema kutokana na mazingira ya Bunge yalivyo yanahitaji wabunge wenye uwezo wa kutoa hoja pamoja na kulishinikiza Bunge liweze kuisimamia na kuiwajibisha serikali vizuri katika masuala nyeti na tete.

"Bunge jipya lijalo linahitaji kuwa na wabunge wenye nguvu na uwezo wa kutoa hoja pamoja na kulishinikiza Bunge liweze kuiwajibisha na kuisimamia ipasavyo serikali katika masuala nyeti na tete ambayo kwa muda mwingi yanaitafuna na kuimaliza nchi," alisema Mbatia Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema ataweka nia hiyo hadharani baada ya wiki mbili kuanzia sasa.

"Wananchi wasiwe na wasi kila kitu kitakuwa bayana baada ya wiki mbili kuanzia sasa ya ama mimi nitagombea au la,"alisema Mbatia ambaye amewahi kuwa mbunge wa Vunjo mwaka 1995-2000.

Mbatia kama mwenyekiti wa NCCR Mageuzi anaungana na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kugombea nafasi ya ubunge.

Mbowe amekwisha tangaza nia ya kugombea katika Jimbo la Hai wakati Mrema anagombea Jimbo la Vunjo.
Tags:

0 comments

Post a Comment