Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mwanasheria mkuu wa Serikali ahofu nchi kuwa na Rais mpenda vita

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MUSWADA wa Baraza la Usalama wa Taifa wa mwaka 2009 umezidi kubainisha tofauti ya mitazamo kati ya Serikali na Bunge, ingawa pia tayari serikali iliridhia kuchomoa muswada huo ili ukafanyie kazi zaidi kama ambavyo Bunge limetaka, Raia Mwema limethibitisha.


Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema
Katika mazungumzo maalumu na Raia Mwema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema amehoji, itakuwaje siku nchi itakapokuwa na Rais anayependa vita na kushangazwa na watu waliokuwa wakidai mamlaka ya Rais ni makubwa mno, lakini leo wanapinga muswada huo.
Akihoji kujadili sheria kwa kuangalia uongozi wa sasa, Jaji Werema amesema: “Sio siku zote tutakuwa na marais wapole kama Mwalimu Julius Nyerere, Mwinyi, Mkapa au Kikwete.”
Kwa mujibu wa mapendekezo ya muswada huo, uamuzi kuhusu usalama wa nchi na hasa wa kuamua nchi iingie vitani au la na nchi nyingine unatajwa kutolewa kwa kupigwa kura na wajumbe wa Baraza hilo ambao wanapswa kuwa 20.
Uamuzi wa kupiga kura, unatajwa kumnyang’anya mamlaka ya Rais ambayo kwa sasa Katiba inamtambua kuwa ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu suala la usalama wa nchi.
Lakini wakati wabunge waliopinga muswada huo ambao baadhi ni wakongwe wa siasa nchini na viongozi wastaafu wanaamini muswada hauko sawa, AG anasema; “Sio siku zote tutakuwa na marais wapole kama Mwalimu Julius Nyerere, Mwinyi, Mkapa au Kikwete,”
“Siku nyingine tunaweza kuwa na Rais anayependa vita kama mimi, nikisikia nchi inatuchokoza tu naamuru vita, nasema ni vita tu kilimo kwanza baadaye...itakuwaje kama sitapunguziwa madaraka?
“Zamani wakati tunapata uhuru tulimpa madaraka makubwa Rais kutokana na weakness ya system...sasa hivi ni miaka zaidi ya 40 tangu Uhuru mazingira ni tofauti hivyo ni lazima tubadilike, wanasema Katiba inavyunjwa mimi sioni inavunjwa wapi,” alisema.
Kwa upande wa hoja za wabunge kuhusu muswada huo, wameeleza kuwa licha ya kumnyang’anya mamlaka Rais, lakini pia  usiri katika masuala ya usalama wa nchi usingeweza kudhibitiwa kutokana na baraza hilo kupendekezwa kuwa na idadi kubwa ya wajumbe.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, wakati wa kuchangia muswada huo alisema, sheria ambayo ingetungwa kutokana na muswada huo ingeweza kusababisha Rais wa Tanzania apinduliwe.
Mbunge huyo wa Wawi, Zanzibar alisema hakuna sehemu yoyote duniani inayopiga kura kuhusu masuala ya ulinzi hivyo muswada huo haufai.
“Suala la ulinzi ni time, ukichelewa dakika mbili umekosea...ulinzi bwana ni amri. hakuna sehemu duniani ulinzi unapigiwa kura” alisema Hamad Rashid.
Wakati mbunge huyo akiwa na mtazamo huo, Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo, aliibua hoja ya baraza hilo kuwa kubwa mno akitilia shaka uwezo wake wa kutunza siri za kiusalama na kusisitiza kuwa; kitaalamu, watu saba hadi tisa tu ndiyo wanaoweza kutunza siri za Serikali, wakizidi utakuwa ni sawa na mkutano wa hadhara.
Mbunge wa Bumbuli, William Shellukindo, amesema, Baraza la Usalama wa Taifa si kongamano au sehemu ya kujadiliana, ni mahali pa uamuzi na kwamba; Rais wa Tanzania ni Amiri Jeshi Mkuu, aachiwe madaraka yake ya kuamua kuhusu masuala ya ulinzi na usalama wa taifa. Akahoji; “Julius Nyerere alipoamua taifa liingie vitani Kagera, kongamano gani lilikaa?
Mbunge wa Mtera, John Malecela amesema, muswada huo umewasilishwa bungeni wakati usio muafaka, ukarekebishwe, upelekwe bungeni wakati unaostahili.
Malecela ametaka Rais aachiwe madaraka ya kuamua kuhusu masuala ya ulinzi wa nchi na ameuliza, ni wapi Rais aliyechaguliwa anakuwa na kamati kubwa ya kumshauri kuhusu masuala ya vita.
Mbunge wa Karatu, Dk Wilbroad Slaa aliukataa muswada huo si tu uliotaja kugongana na Katiba lakini pia alisema muundo wa Baraza la Usalama wa Taifa ni lazima uwe mzuri, hivyo wahusika waangalie nchi nyingine wanafanya nini.
Hata hivyo, takriban siku nne tangu muswada huo ukataliwe kwa hoja za aina hiyo za wabunge, Serikali kupitia AG inaeleza kuwa maoni ya wabunge yatazingatiwa maelezo ambayo hata hivyo yanaonyesha msisitizo wa umuhimu wa muswada huo kwa wakati huu.
Kuhusu hoja ya kuvunjwa Katiba kutokana na kuwasilishwa kwa muswada huo, AG ananukuu Idara ya 37 kifungu cha kwanza cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Ibara hiyo ya 37 (1) inasema; “Mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii, na sheria za Jamhuri ya Muungano katika utendaji kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote.”
Jaji Werema anakanusha kwamba kuwasilishwa kwa muswada huo wenye mapendekezo yanayodaiwa na wabunge yanapora mamlaka ya Rais, kwa kunukuu kifungu hicho cha 37 (1) na hususan maneno yanayotamka; “....isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote.
Katika hatua nyingine, AG alihoji ni kwa nini anayeandamwa kutokana na kukataliwa kwa muswada huo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Sofia Simba na si yeye, ambaye ni Mwanasheria Mkuu. “Kwa nini wanamsakama Waziri Simba, wanisakame mimi siyo Waziri,” alisema AG.
Tags:

0 comments

Post a Comment