IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta amesema madai kwamba ofisi yake ndiyo chanzo cha wabunge kuukataa muswada wa kuundwa kwa Baraza la Usalama wa Taifa ni ya kipuuzi.
Badala yake Spika Sitta alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sofia Simba ndiye aliyelikoroga kwani alipeleka bungeni muswada huo bila kufikiria mambo aliyoyaweka ndani yake.
Sitta alitoa kauli hiyo jana akifafanua taarifa zilizoibebesha lawama ofisi yake kwamba ilivurunda kwa kuupeleka muswada huo kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala badala ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa njia ya simu kutoka mjini Dodoma, jana, Spika Sitta alisema hata kama muswada huo ungepita kwenye kamati wanayosema kuwa ndiyo sahihi, bado ungekuwa na kasoro kutokana na mambo yaliyoandaliwa.
Sitta alimshangaa Waziri Simba kwa kuandaa muswada kama huo aliouita wa hatari na kuhoji kama waziri huyo alifikiria vizuri kabla ya kuupeleka bungeni.
“Hata kama muswada huu ungeenda kwenye kamati yoyote bado usingepita kwa jinsi ulivyoletwa na sijui Waziri anayepeleka kitu kama hiki amefikiria vizuri maana ni wa hatari kweli,” alisema Spika Sitta.
Kwa mujibu wa Sitta, muswada huo unapaswa kufanyiwa marekebisho na kama watauona haufai, wanaweza wakauacha kabisa kwa sasa.
“Haya madai kwamba ofisi ya Spika ndiyo chanzo cha kukwamisha muswada huo ni ya kipuuzi kabisa kwa sababu katibu ana maelekezo yote na ametoa maelekezo sahihi kabisa, na hii si mara ya kwanza.
“Kwa mfano wakati wa kuchunguza suala la mgodi wa Barrick, North Mara, ofisi yangu iliunda kamati mbili; moja ya Nishati na Madini na nyingine ya Mazingira na bado tungeweza kuwa na kamati nyingine ya Afya ishiriki, hakuna ubaya, na ndicho kilichofanyika, sasa hili linashangaza kwa kweli kwa sababu hakuna nia mbaya kama wanavyodai,” alisema Spika Sitta.
Sitta amelazimika kutoa ufafanuzi huo kufuatia taarifa kwamba kulikuwa na msuguano mkali kati ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na ile ya Katiba, Sheria na Utawala.
Naibu Spika wa Bunge, alikaririwa akisema juzi kuwa hakukuwa na ubaya katika kufanya hivyo kwani kamati husika ilikuwa na kazi nyingi.
Wiki iliyopita, katika kile kinachoonekana kugoma kuburuzwa na serikali wabunge kwa mara ya pili waligoma kuupitisha muswada wa Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa wa mwaka 2009.
Muswada huo uliowasilishwa bungeni na Waziri Simba, uliibua mjadala mkubwa kwa wabunge ambao wameweka bayana kuwa serikali isipokuwa makini, kuna kila dalili ikashindwa kuendelea.
Mwaka jana muswada huo ulikataliwa na wabunge kwa madai kuwa una upungufu mkubwa, lakini haukuweza kufanyiwa marekebisho kama walivyopendekeza wabunge.
Wabunge hao wamebainisha kuwa muswada huo unakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kuingilia madaraka ya rais kwa kumuundia chombo ambacho kitafanya kazi zake za ulinzi na usalama wa nchi.
Baadhi walidai kuwa baraza hilo lina mlolongo wa watu wengi ambao ni kama vile kuunda baraza jingine la mawaziri na litakuwa si Baraza la Usalama tena bali ni suala la kisiasa.
Pia muswada huo unadaiwa kutaka kunyang’anya madaraka ya rais na iwapo utapitishwa utaiweka nchi pabaya.
Kutokana na kasoro iliyojitokeza kwenye muswada huo, Mbunge wa Karatu, Dk. Willbrod Slaa (CHADEMA) amemtaka Rais Jakaya Kikwete kumuwajibisha Waziri Simba iwapo hatajiwajibisha kwa kujiuzulu.
Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, alisema suala hilo linaonekana kuwa dogo, lakini ni kubwa na iwapo litapuuzwa, litakuwa hatari kwa maslahi ya taifa.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa ibara ya 97 ya Katiba ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 69 cha kanuni za Bunge, Waziri Simba angetakiwa kujiuzulu mara moja kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.
Pia alitaka watendaji walio chini ya rais pamoja na Kamati ya Bunge iliyoupitia muswada huo kabla ya kupelekwa bungeni kuwajibishwa mara moja.
Baadhi ya kasoro zilizoko kwenye muswada huo, zimo katika kifungu cha 5 (2) g, ambacho hakikueleza wazi maadui wa taifa, hivyo kinatoa nafasi kwa baadhi ya watu kuonekana maadui wakati sivyo.
You Are Here: Home - - Sitta: Waziri Simba kalikoroga
0 comments