IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Baregu: CUF wamelizwa tena Z'bar
MWELEKEO wa Chama cha Wananchi (CUF) kufanikiwa katika jitihada za kupata nafasi ya kushika madaraka, huenda ukagonga mwamba kutokana na uamuzi wa Baraza la Wawakilishi kutaka kuitisha kura za maoni kuamua hatma hiyo.
Pamoja na makubaliano yaliyofikiwa kwa kupitishwa na kuungwa mkono kwa hoja hiyo ndani ya Baraza la Wawakilishi, baadhi ya wadau wa siasa wana hofu kwamba huenda utekelezaji wake utakuwa mgumu kutokana na muda uliobaki.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano kwa nyakati tofauti umebaini kuwa, kuna uwezekano mkubwa mchakato wa kura za maoni unaotarajiwa kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, kukwama au kuahirishwa.
Sababu ambazo zinatajwa kuwa zinaweza kuukwamisha mpango huo ni muda wa kupiga kura za maoni uliowekwa ambao ni kabla ya Oktoba mwaka huu, muda wa kubadilisha Katiba ya Zanzibar ili iruhusu serikali ya mseto na chombo cha kusimamia kura za maoni kitakachokuwa huru na orodha ya wapiga kura itakayotumika.
Pia wachambuzi wa siasa wanadai kuwa hoja ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff aliyoitaka siyo kuingia kwenye kura za maoni kwani suala hilo alilipinga Machi baada ya maazimio ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), kupendekeza hivyo katika mkutano wake wa Butiama.
Kwa upande mwingine inaelezwa kwamba hoja ya kiongozi wa upinzani katika baraza hilo, Aboubakar Khamis Bakar (CUF), iliyoungwa mkono na Baraza la Wawakilishi, haikutoa kile alichokuwa akikidai Maalim Seif, kwani alitaka Rais Amani Abeid Karume aongezewe muda baada ya kubadilisha katiba.
Aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mchambuzi wa masuala ya siasa barani Afrika, Profesa Mwesiga Baregu, akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana, alionyesha wasiwasi wake juu ya kufanikiwa kwa suala hilo kama ilivyopangwa.
“Hatua zozote zinazochukuliwa visiwani Zanzibar ni lazima ziwe za busara ili tusirudi kule tulikotoka. Ninashukuru kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekubali kuwa kitu kimoja na kukubali maazimio ya CCM Butiama, ambayo hapo awali CUF waliyapinga.
“Lakini katika kura za maoni ni lazima matokeo yake yawe ya kuaminika, na je tuna chombo cha kusimamia kura za maoni ili wasiibiwe? Suala hilo liwekwe kwa uangalifu, tusikurupuke kusema tunaenda kwenye kura za maoni halafu tukakwama kwa sababu mambo hayajakamilika na tukaahirisha uchaguzi itakuwa aibu. Suala hili lifanyike kwa umakini na kuaminiana,” alisema Profesa Baregu.
Alisema suala la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) linakwenda sambamba na mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ili iruhusu serikali ya mseto na yote yafanyike kwa njia ambayo haitaweza kufanya nchi kurudi kwenye migogoro.
Aidha alionyesha wasiwasi wake kwenye muda uliobaki ili kuingia katika uchaguzi huo na kufanya matukio yote kwa muda uliobaki kwani wahusika wasipokuwa makini, wanaweza kukwama.
You Are Here: Home - - CUF wamelizwa tena Z'bar
0 comments