Rais Jakaya Kikwete, akipokea maua kutoka kwa watoto wakati wa uziduzi wa Tamasha la kampeni dhidi ya ugonjwa wa malaria lililofanyika juzi usiku katika viwanja vya leaders Club jijni Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa. |
Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa marais wanaopambana na malaria barani Afrika alisema kwamba, ugonjwa wa malaria ni vita ambavyo ni lazima Watanzania wavishinde kwa vile nia ipo, sababu ipo na uwezo upo.
Aliongeza kusema kuwa, lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa malaria inakuwa ugonjwa wa historia kwa Tanzania kwa kuwa hata nchi nyingine zimefanikiwa kuutokomeza.
Alisema kuwa kila siku ya Mungu, kiasi cha watu kufikia 291 hufariki kwa ugonjwa wa malaria, wengi wao wakiwa watoto wadogo, vifo ambavyo alivielezea kuwa vinaweza kuzuilika na kutibika.
"Kila siku ya Mungu, hapa nchini, wanakufa watu hadi 291 kwa ugonjwa wa malaria. Kwa maneno mengine, kila saa inayopita, wanakufa watu zaidi ya 10 kwa ugonjwa wa malaria." Rais Kikwete aliliambia taifa usiku wa kuamkia jana.
"Hawa ni watu wengi mno. Hivyo, malaria ni Janga la Taifa letu. Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba malaria ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika. Ndiyo maana tumeamua kuwa wakati tunaendelea kushughulikia kutibu wagonjwa wa malaria, tuelekeze nguvu zetu katika kuzuia kwa kuanza juhudi za kutokomeza malaria nchini."
Rais Kikwete alikuwa akizungumza moja kwa moja na taifa wakati anazindua Kampeni dhidi ya Malaria katika burudani maalumu iliyofanyika kwenye Viwanja vya Leaders Club mjini Dar es Salaam juzi usiku.
Kampeni hiyo imeanzishwa kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini na taasisi za Malaria No More, Population Services International (PSI) na Chuo Kikuu cha John Hopkins, vyote vya Marekani.
Shughuli ya jana usiku ilifadhiliwa na makampuni ya Exxon Mobil ya Marekani, Vodacom Tanzania Limited na Kiwanda cha A to Z cha Arusha.
Wadau wengine ambao wanachangia mapambano dhidi ya malaria nchini ni taasisi za Tanzania Red Cross, United Against Malaria, MEDA, Christian Social Services Commission, Bakwata, The Global Fund for the Fight Against HIV, Malaria and TB na The US President Malaria Initiative.
0 comments