Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kikao cha NEC-CCM ngoma nzito Dodoma

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Image
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania, Samuel Sitta, akisalimiana na wajumbe wenzake ambao pia ni mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye (Kushoto) na Edward Lowassa, kabla ya kuanza kwa mkutano wa NEC mjini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

MKUTANO wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), umeanza mjini hapa ukiwa umefunikwa na usiri mkubwa kutokana na mambo mazito yanayojadiliwa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba.

Tofauti na mikutano iliyopita, safari hii hali inaonekana kuwa tete huku wajumbe wa wakionekana kutopenda kuzungumza lolote kwa wazi kuhusiana na mjadala wa ajenda za mkutano huo.

Katika hali ambayo inadhihirisha kuwa mambo si shwari katika mwenendo mzima wa mkutano huo jana habari kutoka ndani ya kikao na ambazo hata hivyo, hazikuthibitisha mvutano wa Mbunge wa Igunga Rostam Aziz na Spika wa Bunge Samuel Sitta lilitikisa huku baadhi ya wajumbe wakiwataka wafanye suluhu ili kusudi mvutano wao unaokitikisa chama uishe.

Mnamo saa 12:15 hivi jioni Spika Sitta, Mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela walitoka ndani ya chumba cha mikutano na kukaa kwenye chumba kimoja kwa pamoja wakijadili jambo linaloonekana kuwa ni zito kwa muda wa takribani saa nzima.

Baada ya kuketi pamoja kwa muda huo, baadaye waliamua kuingia ndani ya kikao, haikufahamika kama waliitwa au la, lakini alianza kuingia Dk Mwakyembe akifuatiwa na mama Kilango na baadaye Spika Sitta.

Saa moja usiku umeme ulikatika kwa dakika kama kumi hivi, lakini hakuna hata mjumbe aliyetoka ndani kwenda nje badala yake walibaki chumba cha mkutano na taa zikaingizwa huku walinzi wakiwasukumizia mbali baadhi ya watu waliokuwa na hamu ya kusikiliza nini kilijiri.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete aliingia ukumbini katika jengo la White House saa 8:55 mchana. Punde alipoingia ukumbini alifungua mkutano baada ya kupewa taarifa kuwa idadi ya wajumbe ilikuwa imekamilika.

Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba, alimwambia Rais Kikwete kwamba, idadi kamili ya wajumbe ilikuwa 211, lakini waliohudhuria katika kikao hicho walikuwa wajumbe 205 sawa na asilimia 97 ya wajumbe wote.

"Mheshimiwa mwenyekiti idadi kamili ya wajumbe katika kikao hiki ni 211, lakini waliohudhuria hadi sasa ni wajumbe 205 hivyo mkutano huu ni halali naomba kukukaribisha ili ufungue," alisema Makamba.

Baada ya kusomewa idadi hiyo, tofauti na siku zote Kikwete alitamka neno moja akisema: "Nimefungua" huku akiwa amekaa, kabla ya kuwaomba wajumbe wasimame kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka Rashidi Kawawa (Simba wa Vita).

Mkutano huo ulio chini ya Mwenyekiti wa CCM Kikwete na kuhudhuriwa na wenyeviti wote waliomtangulia, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi unajadili ajenda kuu tatu ambazo ni kupokea na kujadili taarifa ya hali ya kisiasa nchini, taarifa ya Kamati ya Mzee Mwinyi na Uchaguzi wa kuziba nafasi mbili za wajumbe wa Nec.
Tags:

0 comments

Post a Comment