You Are Here: Home - HABARI ZA MICHEZO - Yanga inatisha, yatwaa ubingwa kabla ya ligi kuisha licha ya TFF kuwanyang'anya point 2....
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Na Tedy Mwarabu
Mabigwa wa soka Tanzania bara 2008/9 Yanga wakipongezana. Wamefanikiwa kutangaza ubingwa kabla ligi haijaisha.
BAO la mwaka la kipa Juma Kaseja lilitosha kuweka historia mpya kwa kuipa Yanga ubingwa wa 22 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza huku Azam ikiichapa 6-2 Villa Squad jijini Dar es Salaam.
Yanga iliyokuwa ikihitaji pointi tatu ili kutangazwa mabingwa kwa msimu wa 2008/'09, iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya 21 lililofungwa na Kaseja aliyetumia vizuri udhaifu wa mwenzake, Abdallah Msafiri wa Toto Africa na kuachia mkwaju ambao ulidunda na kutinga nyavuni.
Awali, Kaseja alidaka na kupiga mpira mrefu wa juu uliokwenda moja kwa moja wavuni, dakika tisa baadaye Hussein Sued aliisawazishia Toto Afrika kabla ya Mike Baraza kufunga bao la pili na ushindi kwa mabingwa hao.
Katika mchezo huo ulioshuhudia timu hizo zikikosa penalti kila moja, mshambuliaji MkenyaMike Baraza wa Yanga alikosa penalti dakika ya 18 kipindi cha kwanza , naye Said Dilunga alipoteza nafasi ya pekee ya kuisawazishia Toto wakati mkwaju wake wa penalti ulipoishia mkononi mwa Kaseja, dakika ya 62.
Naye Sweetbert Lukonge anaripoti kutoka Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuwa jahazi la Villa Squad limezidi kuzama baada ya kukubali kipigo cha mabao 6-2 kutoka kwa Azam FC.
Mshambuliaji Nsa Job ndiye aliyekuwa mwiba mkali kwa ngome ya Villa kwa kupachika mabao matano peke yake na kuzawadiwa mpira akimwachia mchezaji wa kimataifa wa Uganda, Danny Wagaluka akihitimisha karamu hiyo ya mabao kwa bao la sita.
Katika mchezo huo uliokuwa na raha ya aina yake, ulishuhudia mabao manne yakifungwa ndani ya dakika nane za mchezo huo, Azam ilipata mabao kupitia kwa Nsa Job, dakika ya 16 na 25 wakati Villa walisawazisha kupitia kwao, Juhudi Samwel 19 na Lewede Dayton (24),kipindi cha kwanza na kufanya matokeo kuwa 2-2 hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilikuwa kibaya zaidi kwa Villa baada ya Nsa Job kufunga bao la tatu, nne na sita katika dakika ya 51,74 na 88, huku Mganda Wagaluka akipachika bao la tano (85).
Katika kile kilichoonekana kama kuchanganyikiwa na kipigo, mchezaji wa Villa , Launt Bagia alikosa penalti mwisho mwa mchezo, dakika ya 90 iliyopanguliwa na kipa wa Azam, Vladimir Niyonkuru.
Kutoka Mbeya, Brandy Nelson anaripoti kuwa mvua kubwa iliyokuwa inanyesha mjini humo ilisababisha mwamuzi Dominick Nyamsana kutoka Dodoma kuusimamisha mchezo huo katika dakika ya 28.
Mchezo huo baina ya Prisons na Kagera Sugar ulikuwa ukichezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini hapa huku zikiwa zimefungana bao 1-1.
Akizungumzia kuahirishwa kwa mechi hiyo mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoani Mbeya, Festo Nkemwa alisema mvua kubwa iliyojaza maji uwanjani ndiyo sababu ya kuahirishwa kwake.
Nkemwa alisema mvua hiyo ilisababisha wachezaji wa timu hizo kuanguka na kuweza kuhatarisha afya zao.
Naye mwamuzi Nyamsana alisema hadi uamuzi huo ulifikiwa kutokana na hali ya uwanja kutofaa tena kwa mchezo huo.
Mabao hayo, Prisons yalifungwa na Shaban Mtupa dakika ya nne, Haruna Hassan wa Kagera akasawazisha, dakika ya 18.
0 comments