SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa onyo kali dhidi ya wanaojihusisha na kuchochea ghasia nchini, akisema "tusije tukalaumiana," wanasiasa wamejibu wakisema kauli hiyo si sahihi na ni ya vitisho ambavyo haviwezi kuwazuia kufanya kazi zao.
Rais Kikwete alitoa onyo hilo juzi wakati wa hotuba yake ya salaam za mwaka mpya alipoonya wale aliowaita wanasiasa hasidi, akisema "tuache vitendo vya kuchochea ghasia kwa kisingizio chochote kile... ni vizuri tukaambiana mapema tusije tukalaumiana".
Lakini kauli yake haijawa nzuri masikioni mwa wanasiasa ambao wanaona kuwa mwaka 2008 ulitawaliwa na vitendo vingi vya kudai haki, ikiwemo migomo na vurugu, wakisema vinathibitisha kuwa nchi haikuwa tulivu kama Rais Kikwete alivyoeleza.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohammed (Mbunge) alisema, Rais hakupaswa kutoa kauli hiyo kwa kuwa ni jambo la kawaida katika nchi yoyote kutokea vurugu.
Alisema sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na kutiwa saini na rais zipo na kwamba hizo ndizo zinapaswa kutumika kushughulikia wanaosababisha vurugu na si kutoa vitisho tu.
"Nilidhani kuwa rais atasema kuwa ataendelea kusimamia haki na utawala bora katika vitu ambavyo vinalegalega, lakini anatoa vitisho... vitisho ni kinyume kabisa na misingi ya utawala bora," alisema Mohammed.
Alifafanua kwamba kwa kawaida zinapotolewa kauli za vitisho kama hivyo, Watananzania hufikiria kuwa ni wapinzani tu ndio walengwa, lakini ukweli ni kwamba hata chama tawala husababisha vurugu katika baadhi ya maeneo.
"Isiwe kwa wapinzani tu, sheria lazima iwe msumeno kwa kila mtu. Kwa chama tawala na vyama vya upinzani, yaani wanasiasa wote," alisistiza Mohammed.
Alipinga kauli ya rais kuwa mwaka 2008 ulikuwa tulivu na kuhoji kuwa rais alitaka aone nchi inawaka moto ndio ajue kuwa si tulivu.
Alisema mwaka jana nchi ilitawaliwa na vurugu, migomo na maandamano na ghasia katika sekta mbalimbali nchini Tanzania.
"Mwaka jana hautasahaulika kwa matukio ya migomo na maandamano ya walimu, wanafunzi wa vyuo vikuu na sekondari, wafanyakazi wa Benki ya Makabwela (NMB), wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na matukio ya ufisadi pamoja na mauaji ya albino. Hii ni amani tu, sijui alikuwa anataka kiashiria gani rais wetu?" alihoji Mohammed.
Hata hivyo, alisema mpasuko wa kisiasa Zanzibar na mfumko wa bidhaa muhimu nchini ambao umesababisha wananchi kutokuwa na amani kwa kukosa mlo wao wa kawaida, yaliutikisa mwaka 2008.
Mohammed alilaumu hotuba ya rais kwa kulifumbia macho suala la ajira kwa Watanzania na kuamua kubaki bubu bila ya kuzungumza chochote kuhusu ahadi hiyo, jambo ambalo alilielezea kuwa ni usaliti kwa wapiga kura.
"Tulitegemea kuwa rais angetuambia katika hotuba yake kuwa ndani ya miaka mitatu ya utawala wake amefanikiwa kutoa ajira ngapi kwa Watanzania lakini hakuligusia kabisa. Huu ni usaliti kwa wapiga kura," alisema Mohammed.
Naye Gedius Rwiza anaripoti kuwa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimeelezea kushangazwa kwake na kauli ya Rais Kikwete ya kuonya dhidi ya wanasiasa na vikundi vya kijamii vitakavyojihusisha na kuchochea ghasia.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema wameipokea kwa mshangao kauli hiyo, kwa sababu rais wa nchi anapozungumzia migomo, anajumuisha walimu ambao wamekuwa wakidai haki zao na sio kuchochea migomo.
Mukoba alisema kauli hiyo ya rais inalenga kuwatisha walimu na wafanyakazi wote wanaoidai serikali madai mbalimbali na kwamba, katika matukio yote yaliyotokea mwaka jana hakuna tukio la mgomo ambalo lilikuwa la uchochezi bali yalilenga kudai haki.
Aidha alisema kuwa, pamoja na kauli hiyo wanategemea kufanya mkutano mkuu mwishoni mwa mwezi huu, kufanya majumuisho ya mwenendo mzima wa ulipaji wa madai ya walimu na kuongeza kuwa baada ya kufanya uhakiki huo watatoa tamko dhidi ya serikali.
"Baada ya kufanya uhakiki huo kama madai hayo yatakuwa hayajawa tayari na mimi nasema tusije kulaumiana maana hapa naona ni kama mchezo wa paka na panya," alisema Mukoba.
Walimu waliitisha mgomo nchi nzima wakishinikiza walipwe zaidi ya Sh16 bilioni ikiwa ni malimbikizo ya malipo yao mbalimbali, hata hivyo mgomo huo ulikumbana na vizingiti mbalimbali vya mahakamani, ikiwemo amri isiyo ya kawaida ya kuuzuia mgomo iliyotolewa usiku na jaji wa Mahakama ya Kazi.
Alisema kauli kwamba baadhi ya watu wamekuwa na lengo la kujinufaisha na ghasia hizo, si kweli kwani upande wa walimu ni jambo ambalo liko wazi hadi sasa bado wanapigwa chenga na kushindwa kupata haki zao.
Naye Fidelis Butahe anaripoti kuwa wastaafu wa EAC, ambao waliwahi kuzuia barabara ya Ali Hassan Mwinyi inayotumiwa na vigogo wengi wa serikali katika harakati zao za kudai haki, wameahidi kuendelea na mikakati yao kama hawatalipwa mafao wanayodai kwa zaidi ya miaka 31.
Mjumbe wa Jumuiya hiyo, Ramadhani Makingi alisema kuwa licha ya Rais Kikwete kutoa onyo kwa wanasiasa na vikundi vya kijamii dhidi ya ghasia, hawatakubali kuona haki yao inapotea kwani hadi sasa hawajalipwa mafao yao huku serikali ikiwa imeshatoa tamko kuwa zoezi la malipo hayo limeshafanyika.
"Kama unavyojua hivi sasa suala letu linashughulikiwa na Kamanda (wa kanda maalum ya Dar es salaam, Suleiman) Kova ametuahidi kuwa atalifikisha sehemu husika na atatupatia jibu.
Lakini kama serikali haitakubali kukaa na sisi kujadili malipo yetu na ikiendelea kung’ang’ania msimamo wake kuwa imeshatulipa, hatutasita, tutaendelea na harakati zetu mpaka tutakapohakikisha tumelipwa," alisema Makingi.
Alisema kuwa licha ya rais Kikwete kutoa onyo kwa wanaochochea vurugu, wapo watu wanaodai haki zao kwa hiyo serikali inatakiwa iwaangalie na sio kuwatisha ili washindwe kudai haki zao, akisema vitisho ni kinyume na sheria za haki za binadamu.
"Tulipanga matembezi zaidi ya mara nne tumezuiwa na polisi; tumefukuzwa kutumia uwanja wa Mnazi Mmoja; tumedai malipo yetu tukaambiwa kuwa hatukuwa wafanyakazi wa EAC bali tulikuwa vibarua; wastaafu wengine wanakufa kila siku, lakini hakuna msaada wowote tunaopata.
Sasa hapo tukiandamana au kudai mafao yetu utatuambia kuwa tunachochea vurugu wakati ni wazi kuwa madai yetu hayasikilizwi," alisema Makingi.
Licha ya Kikwete kuhusisha baadhi ya vurugu hizo kuwa zinachochewa na wanasiasa, lakini hakuweka bayana vitendo hivyo vya uchochezi vilifanywa na watu gani.
Wastaafu hao mpaka sasa wameshafanya matukio makubwa manne. Julai 26 na Septemba 4 mwaka jana waliandamana mpaka Ikulu, Oktoba 17 walijazana nje ya ofisi za Wizara ya Fedha na Uchumi kwa nia ya kuzungumza na Naibu Waziri wa Wizara hiyo juu ya mafao yao.
Hatua yao ya nne, ambayo ilisababisha viongozi nane wa Jumuiya hiyo kukamatwa na kufunguliwa mashitaka ya kukusanyika bila kuwa na kibali, waliifanya Oktoba 29 baada ya kukaa katikati ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Umoja wa Mataifa kuanzia alfajiri na kusababisha msongamano mkubwa wa magari jijini Dar es Salaam.
cool blog
It seems my language skills need to be strengthened, because I totally can not read your information, but I think this is a good BLOG