Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Chuo Kikuu Sokoine SUA Chaendeleza Technolojia ya Panya. sasa kutumika kutegua mabomu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) cha mkoani Morogoro, kinatarajia kupeleka panya maalum kwa ajili ya kutegua mabomu yanayosadikiwa kubakia ardhini katika Kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), iliyoko Mbagala Kizuiani jijini Dar es Salaam baada ya mengine kulipuka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya chuo hicho tangu kuanzishwa kwake miaka 25 iliyopita, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Pofesa Gerald Monela, alisema awali walishindwa kuwapeleka panya hao Mbagala kutokana na maeneo hayo kutokuwa salama kufanya kazi za uteguaji mabomu.

“Naomba nieleweke kuwa, hapo mwanzo, panya hao tulishindwa kuwapeleka katika milipuko ya Mbagala kwa sababu maalum, lakini kwa sasa tunaweza, baada ya wataalam kumaliza uchunguzi na kututhibitishia usalama wa panya wetu,” alisema Profesa Monela.

Alisisitiza kauli iliyowahi kutolewa na Mkurugenzi Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu, Profesa Rhodes Makundi kuwa, kama panya hao wangepelekwa mapema, wangeweza kuchanganyikiwa kutokana na harufu ya mabomu na hata kupoteza maisha yao.

Alisema panya hao wana uwezo mkubwa wa kunusa harufu ya mabomu hata yaliyo chini ya ardhi, hivyo ingekuwa vigumu kufanya kazi ya kutegua mabomu wakati ule kutokana na uchafuzi wa mazingira uliosababishwa na mabomu yaliyolipuka Aprili 28, mwaka huu.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya panya hao kutegua mabomu nchini Msumbiji, Profesa Monela, alisema mengi yalitegwa ardhini tofauti na Mbagala ambako yalilipuka yenyewe na kusambaa katika maeneo mbalimbali.

Alikisifia chuo chake kwamba katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, kimefanya mambo mengi, likiwemo suala la uzalishaji wa panya hao.

Mbali ya utaalamu wa kutegua mabomu, alisema pia wanaweza kufanya uchunguzi kubaini magonjwa mbalimbali, yakiwemo ya kifua kikuu (TB) na tauni na kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Zaidi ya watu 30 walifariki kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea Mbagala, wilayani Temeke, huku maelfu ya wananchi wakiachwa bila makazi baada ya nyumba zao kubomoka.

Wakati huo huo, Waziri wa Mifugo na Umwagiliaji, John Magufuli, anatarajiwa kujadiliana na wataalamu wa SUA juu ya kauli mbiu ya ‘Kilimo Kwanza’ katika sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu chuo hicho kuanzishwe.

Profesa Monela alisema kutokana na kaulimbiu ya mwaka huu kulenga kuboresha hali ya kilimo, wataipa kipaumbele ili kuchochea maendeleo ya kilimo nchini.

“Sehemu kubwa ya Tanzania inategemea kilimo, pia kilimo ndiyo chanzo cha kuongeza pato la taifa, ambapo SUA mpaka sasa tunajivunia kufanya vizuri katika kipindi cha miaka 25, hivyo kwa kuona umuhimu huo, wataalamu watajadili suala la Kilimo Kwanza kwa undani na tutashirikiana na Waziri Magufuli katika mjadala huo,” alisema Profesa Monela.

Sherehe za maadhimisho hayo, zinatarajia kuanza Novemba 23 chuoni hapo kwa kujadili mada mbalimbali pamoja na maonyesho ya chuo na kilele chake kitafikiwa Novemba 27 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe.

Tags:

0 comments

Post a Comment