Na Sadick Mtulya (Mwananchi) MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amedai kuwa Rais Jakaya Kikwete hakuwa na msimamo katika kutatua matatizo tangu alipokuwa chuoni. Profesa Lipumba ametoa madai hayo wakati utatuzi wa masuala mbalimbali yanayoikabili nchi na ndani ya CCM unasuasa na kusababisha makundi ambayo yanaathiri utendaji wa serikali na chama hicho. Profesa Lipumba alitoa madai hayo juzi alipotakiwa na wahadhiri na wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) waliohudhuria mkutano wa siku tatu wa kujadili umuhimu wa falsafa katika nchi za Afrika Mashariki kutoa maoni yake kuhusu mbinu zinazotumiwa na Rais Kikwete katika kutatua matatizo ya nchi na CCM. Lipumba ambaye amesoma na Rais Kikwete Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alidai kuwa Rais Kikwete kabla hajashika nyadhifa mbambali serikalini na katika chama, hakuwa na msimamo thabiti katika kufanya maamuzi ya masuala mbalimbali. “Suala la Rais Kikwete kutokuwa na msimamo katika kuyapatia ufumbuzi masuala nyeti yanayoikabili nchi na ndani ya CCM ni tatizo alilokuwa nalo tangu akiwa shuleni na waliosoma naye wanajua hilo. “Alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakuwa na msimamo katika kutatua masuala mbalimbali hivyo ni dhahiri kuwa historia yake ndiyo inamuhukumu,†alidai Profesa Lipumba. Lipumba alifafanua kwamba, ndiyo maana watu ambao sio waaminifu na wanaojua historia yake wanatumia mwanya huo kufanikisha mambo yao mabaya. “Unajua kila mtu ana udhaifu wake na historia yake katika maisha, sasa watu wanatumia mwanya wa Rais Kikwete wa kutokuwa na maamuzi ya haraka pamoja na msimamo,†alisema Lipumba. Hivi karibuni Profesa Lipumba aliwahi kunukuriwa na vyombo vya habari akisema tabia ya Rais Kikwete kutaka kuwa mwema kwa makundi yote ndani ya CCM na kushindwa kutoa msimamo wake kama kiongozi mkuu, ndiyo kiini cha mgawanyiko unaoendelea wa wabunge wa chama hicho. Mgawanyiko huu uliongezeka hivi karibuni kwa wabunge wa CCM walipokutana na kamati ya Rais Hassan Mwinyi mjini Dodoma iliyopewa kazi ya kutafuta namna ya kuupatia ufumbuzi mgawanyiko uliomo ndani ya chama. Katika mkutano huo, wabunge na mawaziri walirushiana makombora wazi wazi baadhi wakiwatuhumu wenzao kwa kuwakumbatia mafisadi wengine wakijitoa muhanga kuwatetea wanaotuhumiwa kwa ufisadi. Mbunge wa Simajiro, Christopher Ole Sendeka ambaye ni mmoja wa wapambanaji wa ufisadi, alipendekeza aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, mwanasheria mkuu wa zamani, Andrew Chenge na Mbunge wa Igunga na Mweka Hazina wa zamani wa CCM, Rostam Aziz waondolewe kwenye nyadhifa zao katika chama kwa vile ni watuhumiwa wa ufisadi. Hoja hiyo ilipingwa na Chenge ambaye alisema hawezi kuhukumiwa kwa tuhuma tu bila ya kuwepo ushahidi wa anayodaiwa kufanya. Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais , (Utawala bora), Sophia Simba na Naibu waziri Kazi na Maendeleo ya Vijana, Makongolo Mahanga walijitokeza kuwatetea watu hao wakidai kuwa wanaonewa na kwamba kuna haja ya kuchunguza upya kashfa ya Richmond. Profesa Lipumba alidai kuwa kutokana na udhaifu huo wa Kikwete ndio maana anashindwa kuwawajibisha wahusika wa kashfa mbalimbali wakati anajua kila kitu na ushahidi wa kutosha umetolewa. "Anashindwa kusimamia uwajibishwaji wa wahusika; anajua kila kitu na ushahidi umetolewa wa kutosha kuhusu mambo ya ufisadi, kama angekuwa makini ni lazima watuhumiwa wote wangeshughulikiwa ndani ya miezi sita hadi mwaka mmoja," alisema Lipumba. |
0 comments