Wagombea watakaochuana kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika timu ya Simba nchini Tanzania wamejulikana baada ya kutangazwa na kamati ya uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF.
Awali wagombea 57 waliomba nafasi mbalimbali katika klabu hiyo, kabla ya baadhi yao kuwekewa mapingamizi, kamati hiyo ya TFF ilitangaza orodha ya waliokidhi matakwa.
Katika nafasi ya mwenyekiti, mgombea wa kwanza kuwekewa pingamizi alikuwa ni mwenyekiti anayemaliza muda wake Hassan Dalali ambaye aliondolewa kutokana na vyeti vyake kuwa na matatizo.
Wengine waliowania nafasi hiyo ni Michael Wambura, Aden Rage, Mohamed Nyangamala, Andrew Tupa, Hassan Hassanoo na Zacharia Hans Pope. Hata hivyo, Tupa aliondolewa jina lake kwa kukosa sifa, ingawa wote walikuwa wamewekewa pingamizi isipokuwa Hassan Hassano.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TFF, Deo Lyatuu alisema baada ya mahojiano na wote waliowekewa pingamizi, ni Aden Rage pekee ndiye aliyesalimika ambaye atasimama na Hassano kupigania nafasi ya mwenyekiti.
Katika nafasi ya makamu mwenyekiti, katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda, ameondolewa kutokana na kutotimiza majukumu ya kikatiba ya Simba.
Hata hivyo, Michael Wambura amesema anatafakari uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria kupinga uamuzi huo kwa maelezo kuwa amefanyiwa mizengwe.
0 comments