Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA MICHEZO - Ni TFF ya Simba na Yanga

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Ni TFF ya Simba, Yanga

WAKATI leo ni mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu za kuomba uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), idadi ya wagombea imezidi kuongezeka. Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage, aliwataja waliochukua fomu jana ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha, Khalifa Mgonja anayewania nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na mmoja kati ya wanaounda kundi la Friend's of Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' anayetaka nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais. Aliwataja wengine waliochukua jana ni Katibu Mipango wa zamani wa Yanga, Abdul Sauko, Vicent Oswald, Mbasha Matutu, John Mwangakala, Lameck Lyambaya, Nassor Kipenzi na John Kiteve wanaowania ujumbe wa Kamati ya Utendaji. Lakini uchaguzi huo licha ya kumvutia Kaburu, wengine wa kundi la Friends of Simba ambao wametia mguu jana wakiomba ujumbe ni Hassan Hassanoo, Mlamu Ng'ambi na Mohammed Nassoro, wakati Evarist Hagila ambaye pia yupo Friends of Simba aliingia mwanzoni mwa wiki akiomba ujumbe wa TFF. Hassanoo pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Simba. Wanamichezo wengine waliochukua fomu za TFF siku za nyuma ni Amir Roshan, Warles Karia, Samuel Nyara, Shaaban Nampunde, Joseph Mapunda, Israel Mwansasu, Eliud Mvella na Said Mohammed Said wote wakitaka ujumbe. Pia wapo Leodeger Tenga, Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga Jamal Malinzi na Richard Rukambula wanaowania urais, wakati Makamu wa Kwanza wa Rais ni aliyepata kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Simba na pia mdau wa Friends of Simba Michael Wambura, mwanachama wa Yanga Athumani Nyamlani na Lawrance Mwalusako, huku Makamu wa Pili wa Rais ni Katibu Mkuu wa Yanga Lucas Kisasa. Tayari wanamichezo mbalimbali wameanza kurudisha fomu kwenye ofisi za TFF zilizopo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi huo utakaofanyika Desemba 14 mwaka huu, ambapo siasa za Simba na Yanga zinaonekana kuchukua nafasi.

0 comments

Post a Comment