Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kada CCM afanya kufuru

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter WAKATI kampeni za kuwania uongozi ndani ya Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeanza, mfanyabiashara maarufu ambaye ni mmiliki na mkurugenzi wa kampuni ya Shivacom, Tanil Somaiya, ametoa msaada wa sh milioni 400 kwa ajili ya kugharamia mkutano mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM). Somaiya alitoa msaada huo jana mbele ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, katika hafla iliyofanyika katika jengo la Makao Makuu ya chama hicho la White House, mjini hapa. Mbali ya fedha hizo, mfanyabiashara huyo alitoa pia fulana 1000, kofia 1000, mabegi 1,000 maalum kwa ajili ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi, vitabu vidogo 1,000 (Note Book) na bendera za UVCCM; vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh milioni 250. “Mimi ni mkereketwa na kada wa CCM, hivyo nimeamua kwa mapenzi yangu kutoa msaada huo kwa ajili ya kugharamia mkutano mkuu wa uchaguzi wa jumuiya hiyo,” alisema mfanyabiashara huyo, huku akiwashangaza wajumbe wengi wa NEC waliohudhuria hafla hiyo. Baadhi ya viongozi wengine walioshuhudia msaada huo ukikabidhiwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, John Malecela, Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, mawaziri, wabunge na wajumbe wengi wa NEC waliokuwa kwenye mkutano wao juzi na jana mjini hapa. Akizungumza kabla ya kukabidhiwa kwa msaada huo, Mwenyekiti wa UVCCM, anayemaliza muda wake, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema msaada huo umetokana na kazi nzuri zinazofanywa na jumuiya hiyo. Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Francis Isaack, alisema UVCCM uliunda tume ya kufanya maandalizi ya mkutano huo yenye wajumbe wanne. Aliwataja wajumbe hao kuwa ni William Ngeleja, (Waziri wa Nishati na Madini), William Lukuvi (Mkuu wa Mkoa wa Dodoma), Somaiya na Laurence Masha (Waziri wa Mambo ya Ndani). Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema alipojulishwa na kuombwa na Lukuvi kuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya utoaji wa msaada huo, alihisi ni kitu kidogo, lakini hakusita kueleza kuwa msaada huo ni mkubwa kwa chama. Alimtaka mfanyabiashara huyo wakati mwingine kutengeneza pia hata bendera za chama badala ya za UVCCM pekee. “Ila pia hii ni njia mojawapo ya kujitangaza, tukitaka kofia, tutasema mwende Shivacom, tukitaka fulana, tutasema mwende Shivacom, tukitaka mabegi, Shivacom, kwa hiyo na sisi tutakusaidia kujitangaza, ili upate zaidi ya kile alichotoa,” alisema Kikwete. Uchaguzi mkuu wa jumuiya hiyo, unatarajia kufanyika Desemba 15 mwaka huuu baada ya juzi NEC kukamilisha kazi ya kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu wake. Waliopitishwa kuwania nafasi ya Mwenyekiti inayomwezesha mshindi kuingia ndani ya kikao cha juu cha chama hicho cha Kamati Kuu (CC) ni Yusuf Hamad Masauni, Suleiman Haji na Adila Hilal Vuai, wote kutoka Zanzibar wakati nafasi ya Makamu Mwenyekiti inawaniwa na Beno Malisa, Hassan Bashe na Zainabu Kawawa, ambao awali waliomba nafasi ya Mwenyekiti. Kwa msimamo huo, nafasi ya mwenyekiti wa UVCCM, inaweza kwenda Zanzibar na endapo itakuwa hivyo, itakuwa ni mara ya pili kwa kiti hicho kwenda visiwani humo baada ya mara ya mwisho kukaliwa na Mohamed Seif Khatib, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano).
Tags:

0 comments

Post a Comment