You Are Here: Home - - Watuhumiwa EPA waongezeka
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Malkia Margerethe II wa Denmark kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Dar es salaam leo kabla ya kuondoka kwa Malkia huyo kurejea Nchini Denmark baada ya kukamilisha ziara yake ya kiserikali ya hapa Nchini, ambapo ametembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria ikiwemo Arusha, Ngorongoro, Morogoro na Zanzibar
HATIMAYE mfanyabiashara Mwesiga Rutakyamilwa Lukaza, anayekabiliwa na tuhuma za wizi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), jana alifikishwa mahakamani baada ya Jeshi la Polisi kufanikiwa kumnasa ikiwa ni wiki ya pili tangu watuhumiwa wa wizi huo waanze kufikishwa mahakamani.
Kwa pamoja, watu hao ambao wamefikia 19, wanatuhumiwa kuchota kiasi cha Sh133 bilioni kutoka akaunti hiyo ya EPA, lakini wanaopandishwa kizimbani ni wale ambao hawakuitikia wito wa Rais Jakaya Kikwete wa kutaka wote waliochota fedha hizo wawe wamezirejesha ifikapo Oktoba 31.
Na kama ilivyokuwa kwa watuhumiwa wengine 14 ambao tayari wameshafikishwa mahakamani, Lukaza na wengine wawili waliopanda kizimbani jana hawakuweza kutoka mahabusu kwa dhamana baada ya kuwekewa masharti magumu.
Tangu wiki iliyopita, watuhumiwa 16 walikuwa wamefikishwa mahakamani, akiwemo mfanyabiashara maarufu mwenye asili ya Kiasia Jayantkumar Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel, na kusomewa mashtaka tofauti kuhusiana na wizi huo unaosadikiwa kufanyika kati ya mwaka 2005/06 na jana ilikuwa ni zamu ya Lukaza na watuhumiwa wengine wawili.
Lukaza ilibidi asomewe mashitaka yake wiki iliyopita sambamba na ndugu yake Johnson Mutachukurwa, hata hivyo ilishindikana kutokana na Jeshi la Polisi kushindwa kumtia nguvuni kwa kile kilichodaiwa kuwa alikuwa nje ya nchi.
Mfanyabiashara huyo alifikishwa mahakamani hapo jana sambamba na wafanyabiashara wawili wenye asili ya Kiasia kujibu tuhuma za kula njama na kuibia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zaidi ya Sh5 bilioni.
Lukaza jana alisomewa jumla ya mashitaka matatu, likiwemo la kula njama na kujipatia zaidi ya Sh6 bilioni kwa njia ya udanganyifu.
Wakili wa serikali, Biswalo Mganga alidai kuwa Desemba 7 mwaka 2005 jijini Dar es salaam mshitakiwa huyo akiwa na ndugu yake Johnson Rutakyamilwa Lukaza, walikula njama na kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka BoT.
Mganga alidai kuwa washitakiwa kwa pamoja walijipatia kiasi hicho cha fedha baada ya kudai kuwa kampuni ya Kernel Limited ilipewa deni na kampuni ya Maruben Corporation ya nchini Japan, kitu ambacho Mganga alidai haikuwa kweli.
Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Novemba 18 mwaka huu itakapotajwa tena na mtuhumiwa huyo amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili, mmoja kati yao awe ndugu wa karibu na mtuhumiwa huyo anatakiwa kuwasilisha mahakamani hapo nusu ya fedha anazodaiwa kuiba, ambazo ni sawa na Sh3 bilioni.
Wakati Lukaza akirudishwa rumande wafanyabiashara wengine wawili waliofikishwa naye mahakamani hapo jana walipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuiibia benki hiyo Sh5 bilioni.
Mbele ya Hakimu Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali, Stanslaus Bonifance aliwataja wafanyabiashara hao kuwa ni Ajay Soman na ndugu yake Jay Soman ambao ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya mwaka 2003 na mwaka 2005 watuhumiwa hao, wakiwa na watu wengine ambao bado hawajakamatwa, walikula njama ya kutenda kosa hilo la wizi katika benki hiyo.
Aliongeza kuwa Septemba 2 mwaka 2005 watuhumiwa hao kwa njia ya ujanja na udanganyifu, wakiwa jijini Dar es Salaam, wanadaiwa kuiba kiasi hicho cha fedha mali ya BoT kwa kutumia Kampuni ya Liquidty Services ambayo ilipokea ingizo la pesa hizo kama malipo kutoka Kampuni ya Society Aisacenner Contruction de Machine ya jijini Dar es salaam.
Watuhumiwa hao walisomewa jumla ya mashitaka matatu yakiwemo ya kula njama na kuiibia BoT, lakini walikana kuhusika na tuhuma hizo na kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 25 mwaka huu itakapotajwa tena.
Hata hivyo watuhumiwa hao walijikuta wakirudishwa rumande kama ilivyo kwa washitakiwa wengine baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ikiwemo kuwasilisha hati ya kusafiria mahakamani hapo na kuwasilisha nusu ya fedha inayodaiwa kuibwa na watuhumiwa hao na kutotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam.
Wakati watuhumiwa hao wanafikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka yao, Jeetu Patel anaendelea kusota mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Mpaka sasa watuhumiwa wawili Davie Kamungu na Godfrey Mosha ndiyo pekee waliofanikiwa kutimiza masharti ya dhamana huku washitakiwa wengine mpaka jana walikuwa wanashughulikiwa.
Watuhumiwa hao kwa mara ya kwanza walianza kufikishwa mahakamani hapo Novemba 5 mwaka huu na kusomewa mashitaka yao kwa mahakimu tofauti katika mahakama hiyo.
0 comments