KESI inayoelekea kuwa mashuhuri hapa nchi ya ufisadi uliofanyika kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu, imeendelea jana ambapo watuhumiwa watatu zaidi wameburutwa kortini. Waliofikishwa jana kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ni pamoja na Bw. Mwesiga Lukaza ambaye ameunganishwa katika kesi ya awali iliyokuwaikimkabili mdogo wake, Bw. Johnson Lukaza aliyefikishwa katika kundi la kwanza lililokuwa na watu 10 na kusomewa mashtaka huku Bw. Mwesiga akiwa hayupo mahakamani. Ndugu hao wawili wanadaiwa pamoja na mashitaka mengine kula njama na kuiba fedha Benki Kuu wakitumia kampuni ya Kernel Ltd ya Tanzania. Wengine waliofikishwa mahakamani hapo jana ni Bw. Ajay Somani na Bw. Jay Somani, wamiliki wa kampuni ya Liquidity ambao wote kwa pamoja walisomewa mashtaka ya kula njama, kuiba pamoja na kujipatia ingizo la fedha kinyume cha sheria. Upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa serikali Bw. Manyanda, Wakili Mkuu wa serikali, Bw. Stanlaus Boniface na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bw. Charles Kenyelah, huku jopo la mawakili wa upande wa utetezi likiongozwa na Bw. Majura Magafu. Katika kesi ya kwanza, mshtakiwa Bw. Mwesiga alisomewa mashitaka matatu ambapo katika shtaka la kwanza alidaiwa kuwa kati ya Desemba 2003 hadi Desemba 2005, mshtakiwa pamoja na ndugu yake aliyeko mahabusu, walikula njama za kuiba fedha katika Benki Kuu ya Tanzania. Akisoma mashitaka hayo, Bw. Manyanda alidai kuwa mnamo Desemba 7, 2005, watuhumiwa waliiba zaidi ya shilingi bilioni 6.3 mali ya Benki Kuu ya Tanzania. Na katika shtaka la mwisho, ilidaiwa kuwa mnamo Desemba 7, 2005, katika maeneo ya jijini Dar es Salaam, watuhumiwa walijipatia ingizo la zaidi ya shilingi bilioni 6.3 mali ya Benki Kuu ya Tanzania isivyo halali, wakijifanya kuwa kampuni ya Kernel imepata idhini ya kununua deni la thamani ya fedha hizo kutoka katika kampuni ya Maruben Corporation ya nchini Japani. Wakili Manyanda alisema kuwa upelelezi bado unaendelea na hakupinga washitakiwa hao kupewa dhamana. Kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai (CPA), makosa waliyohusishwa nayo yana dhamana. Hakimu Mkuu Mkazi, Bi. Euphimia Mingi anayesikiliza kesi hiyo aliyataja masharti ya dhamana kuwa ni washitakiwa watoe nusu ya fedha wanazodaiwa kuziiba. Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 18 mwaka huu. Mbali na kesi hiyo, katika shauri jingine lililofunguliwa kwa Hakimu Mkazi, Bi. Victoria Nongwa wa mahakama hiyo, ndugu wawili, Bw. Ajay Somani na Bw. Jay Somani walishitakiwa kwa kesi nyingine wakidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2003 hadi Oktoba 2005, walikula njama ya kuiba Benki Kuu ya Tanzania. Akisoma shitaka hilo, wakili Manyanda alidai kuwa mnamo Septemba 2, 2005, katika maeneo ya jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliiba zaidi ya shilingi bilioni 5.9 mali ya Benki Kuu ya Tanzania. Katika shitaka jingine ambalo ni mbadala wa lile la awali, ilidaiwa kuwa mnamo Septemba 2, 2005, washtakiwa walijipatia ingizo hilo la fedha wakionesha kuwa, kampuni yao ya Liquidity Services ya jijini Dar es Salaam, imepata uhalali wa kununua deni lenye thamani ya zaidi ya bilioni 5.9 kutoka katika kampuni ya Ulaya, ya Society Aisacenne de Construction de Machines Textiles kitu ambacho walijua si kweli. Upelelezi wa kesi unaendelea na Hakimu Nongwa alitaja masharti ya dhamana kuwa ni pamoja na kutoa fedha taslimu zaidi ya bilioni 1.4 au mali yenye thamani ya pesa hiyo isiyohamishika, pamoja na wadhamini wawili wa kuaminika, pamoja na kuwasilisha mahakamani hati zote za kusafiria. Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 25 mwaka huu. Watuhumiwa wote wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Sakata la EPA kwa kifupi Kati ya mwaka 1970 na 1980, Serikali ya Tanzania ilipokea huduma mbalimbali kutoka kampuni na taasisi za nje, lakini kushuka kwa thamani ya shilingi kulikochangiwa na vita ya Kagera kunaifanya Serikali ishindwe kulipa madeni hayo kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni. Kati ya mwaka 1985 na 1995, Benki ya Dunia iliona haja ya kuisaidia Tanzania kulipa madeni hayo kupitia mikakati mbalimbali ukiwamo wa kuyanunua (Debt Buy Back). Mwaka 1985 Akaunti ya EPA ilihamishwa kutoka NBC kwenda BoT. Mwaka 1994, ili kuhakiki wadai halisi, Tanzania ilitangaza kwenye vyombo vya habari vya kimataifa wenye madai wajitokeze. Kampuni chache sana zikaitikia mwito huo. Hivyo kwa sehemu kubwa orodha muhimu ya madeni ikawa ikitumika ile iliyoandaliwa awali na NBC, ambayo wakaguzi wengi waliitilia shaka kuwa haikuwa sahihi kwa asilimia 100. Mwaka 1997, Serikali ilianza kutilia shaka uendeshaji wa EPA na kuiandikia barua BoT. Haikupewa hesabu hizo. Mwaka 2004, wakaguzi wa kimataifa wakiongozwa na kampuni ya M/S Lazard walitoa ripoti inayoonesha mwenendo wa akaunti ya EPA, wadeni waliolipwa, wasiolipwa na sababu zao na hali halisi ya madeni. Pia wakaishauri BoT isilipe sehemu kubwa ya deni lililokuwapo kwa sababu lina utata. Novemba 25, 2004, kampuni ya wakaguzi wengine wa kimataifa PriceWaterhouseCoopers ilithibitisha kuwa mapendekezo na yale yote yaliyobainishwa na ripoti ya Lazard na wenzake, pamoja na kasoro ndogo ndogo, yalikuwa sahihi. Julai, 2005, Gavana wa BoT, Dkt. Ballali aliijibu Serikali kuwa hawezi kutoa mchanganuo wa akaunti ya EPA kwa sababu ya ubovu wa mfumo wa kompyuta. Hakuwahi kutoa mchanganuo huo. Septemba, 2005 hadi Januari,2006, harakati nzito zilifanyika kwenye akaunti hiyo ambapo kampuni 22 za kitanzania zinalipwa jumla ya sh. bilioni 133 zikidai ni mawakala wa kampuni za nje zinazoidai Serikali. Juni, 2006, wakaguzi wa ndani wa BoT, kampuni ya Delloite & Touche, walibaini malipo yenye utata katika akaunti ya EPA kwenda kampuni ya Kagoda Agriculture. Septemba 8 na 9,2006, Gavana wa BoT, Dkt. Ballali aliwaambia wakaguzi kuwa Serikali ndiyo inayojua yote kuhusu fedha zilizochotwa na Kagoda kutoka EPA. Septemba 15, 2006, Waziri wa Fedha, wakati huo, Bibi Zakia Meghji, alijibu wakaguzi kuwa Serikali inazitambua fedha hizo kuwa zilitumika katika 'matumizi mahsusi yenye maslahi kwa Taifa.' Alishindwa kutoa nyaraka kuthibitisha matumizi hayo. Baadaye alikiri kuwa alidanganywa, hakupewa maelezo sahihi na maofisa wa BoT. Oktoba 28, 2006, Waziri Meghji alikiri mbele ya wakaguzi wa Deloitte & Touche kuwa aliposaini barua ya kuidhinisha malipo kwenda Kagoda aliegama zaidi katika maelezo tu ya Gavana Ballali kuwa ni malipo halali. Akakiri katika mahojiano na wakaguzi kuwa baadaye ndipo akabaini kulikuwa na ubadhirifu kwenye akaunti ya EPA. Desemba, 2007, wakaguzi wa Ernst & Young nao walisema baada ya mahojiano marefu na Waziri Meghji, hakuna ushahidi kuwa Serikali iliagiza malipo kutoka kwenye akaunti ya EPA. Januari, 2008, Ikulu ilitoa kwa ufupi kilichobainika kwenye ripoti ya Ernst & Young na kuanza hatua alizozichukua Rais Kikwete za kuunda Kamati Maalumu kuangalia hatua zaidi za kuchukuliwa dhidi ya waliohusika. Ikapewa miezi sita. Januari 10, mwaka huu, Rais Kikwete alitangaza kumfuta kazi Dkt. Ballali na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Benno Ndulu. Aprili mwaka huu, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa Baraza jipya la Mawaziri na kumwondoa Bibi Meghji na nafasi yake kuchukuliwa na Bw. Mustapha Mkulo. -Juni mwaka huu, miezi sita iliyopewa Kamati Maalumu ya Rais ilielezwa kufikia mwisho, Bunge linaendelea Dodoma huku Serikali ikiwataka wabunge kutulia na kusubiri matokeo ya Kamati ya Rais inayosimamia urejeshwaji wa fedha hizo. -Agosti 21-Rais Kikwete alihutubia Bunge na kutoa hadi Oktoba 31 waliochukua fedha hizo wazirejeshe. -Oktoba 31;Rais alilihutubia taifa na kueleza fedha zilizorejeshwa huku asilimia takribani 30 zikiwa hazikurejeshwa na kutangaza kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka amepewa kazi ya kuzifungua kesi hizo. -Novemba; Kesi za EPA zaanza kufunguliwa kwenye Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam.
You Are Here: Home - -
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Watuhumiwa wengine wa wizi wa Fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania ( BoT) wakisubili kusomewa mashtaka yao kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Bw. Mwesiga Lukaza, Bw. Ajay Suryavant Somani na Bw. Jai Chohotalal Somani. (Picha na Charles Lucas).
0 comments