Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Bilioni 69/- EPA zarudi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Shilingi bilioni 69.3 ambazo ni sawa na asilimia 76.7 ya Sh bilioni 90.3 zilizochotwa kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zilikuwa zimerejeshwa kufikia jana, Rais Jakaya Kikwete amelitangazia Taifa. Hatua hiyo inatokana na agizo lake alilolitoa Agosti 21, mwaka huu alipohutubia Bunge mjini Dodoma ambako alielezea kwa kirefu yaliyotokea kuhusu ubadhirifu huo, hatua zilizochukuliwa na mahali suala hilo lilipokuwa limefikia katika kulishughulikia. “Napenda kuwajulisha kuwa, taarifa nilizoletewa majira ya mchana leo, ni kuwa kiasi cha shilingi 69,326,437,650 kati ya shilingi 90,359,078,804 zilikuwa zimerejeshwa. Hii ni sawa na asilimia 76.7,” alisema Rais Kikwete jana wakati akilihutubia Taifa. Aidha, Rais Kikwete alisema leo taarifa kamili itatolewa juu ya kiasi halisi ambacho kitakuwa kimerejeshwa. Alisema katika hotuba yake ya Agosti bungeni, alieleza kwamba wale wote waliokuwa miongoni mwa yale makampuni 13 yaliyolipwa Sh 90,359,078,804, waliochukua fedha ambao walikuwa hawajarejesha fedha hizo kufanya hivyo ifikapo jana, Oktoba 31. “Aidha, niliagiza uchunguzi kwa zile kampuni tisa zilizolipwa shilingi 42,656,107,417 uendelee. Kamati iliomba idhini ya kuwasiliana na vyombo husika vya dola vya mataifa husika ya nje ili kupata ukweli na kukamilisha uchunguzi wao,” alisema na kuongeza, aliagiza kwamba wote ambao kufikia jana watakuwa hawajatekeleza agizo hilo, hatua za kisheria zichukuliwe. Alisema pamoja na kutolewa taarifa hiyo, amekwishatoa maelekezo kamili kwa wale ambao hawakutimiza malipo, Kamati ikabidhi majalada yao kwa Mkurugenzi wa Mashitaka mara moja, kwa hatua zipasazo za kisheria. Kuhusu uchunguzi uliokuwa unaendelea kufanywa kuhusu kampuni tisa, alisema anasubiri taarifa yao mpya kuhusu maendeleo ya uchunguzi huo. "Taarifa niliyopewa wiki mbili zilizopita zinaonyesha kuwa Polisi wetu hawajapata majibu kutoka kwa wenzao katika nchi walizoomba msaada. Hivyo, nakusudia kuwataka waendelee kufuatilia kwa wenzao ili hatua zipasazo ziweze kuchukuliwa,” alisema Rais Kikwete. Aliipongeza Kamati ya Mwanasheria Mkuu kwa kazi nzuri iliyofanya ambayo mbali na kubaini namna ya tuhuma za uhalifu zilivyofanywa, pia ilibaini wahusika na kuwabana kiasi cha kufanikiwa kurejeshwa kwa fedha ambazo vinginevyo zingepotea kabisa. “Lakini kubwa zaidi, nawashukuru wananchi kwa uvumilivu na uelewa wao wakati wote serikali ilipokuwa inalishughulikia sakata hili la aina yake katika historia ya nchi yetu. Tumefarijika sana kwa uelewa na ushirikiano wenu. Nawaomba tuzidi kushirikiana katika mambo yote yanayohusu mustakabali wa nchi yetu. Aidha, utaratibu wa kuzigawa fedha hizo kwa ajili ya shughuli za kilimo na miundombinu zimekamilika. Kampuni 23 zinadaiwa kuchota fedha, Sh bilioni 133 katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya BoT, na iligundulika baada ya ukaguzi wa hesabu uliofanywa na Kampuni ya kigeni ya Ernst & Young mwaka 2005/2006 ambayo ilipewa kazi iliyoachwa na Deloitte & Touche ya Afrika Kusini.
Tags:

0 comments

Post a Comment