Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Ajali zaua 25 papo hapo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

ZAIDI ya watu 25 wamekufa na wengine 84 kujeruhiwa ambapo 50 wamelazwa katika hospitali za Singida na Dodoma baada ya mabasi mawili kupata ajali tofauti katika mikoa hiyo. Katika ajali ya Singida, watu zaidi ya 20 walipoteza maisha na 35 kulazwa katika hospitali ya Iramba, huku ajali ya Dodoma walikufa watu watano na 15 kulazwa katika hospitali ya Mkoa ya Dodoma. Wakati ajali ya Singida ilitokea juzi saa 2.30 asubuhi katika Mlima Sekenke ilihusisha basi la Zuberi lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, ya Dodoma ilihusisha basi la Sai Baba lililokuwa likitoka Dodoma kwqenda Dar es Sakaam na kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso. Basi la Zuberi ni aina ya Scania lenye namba T 677 AGJ wakati la Sai Baba ni namba T 700 ADK na lori la Fuso ni namba T 870 ASK. Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Bibi Celina Kaluba alisema chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa basi hilo na mwendo wa kasi. Kamanda Kaluba alisema hadi jana idadi kamili ya watu waliofunikwa na basi hilo ilikuwa haijajulikana vizuri kutokana na ugumu wa kazi ya uopoaji ambapo basi hilo lilipinduka na kuporomoka kwenye korongo na kulala chali. Hata hivyo, Kamanda Kaluba alisema hadi juzi saa 10 jioni idadi ya abiria waliokuwa wamekufa ilifikia 17 na kazi kubwa ilikuwa ni namna ya kuligeuza basi hilo ambalo limepinduka chali huku zana zinazotumika zikiwa duni, hali iliyofanya kazi ya uopoaji kuwa ngumu. Akisimulia chanzo halisi cha ajali hiyo Kamanda Kaluba alisema imetokea kutokana na ubovu wa basi hilo na ubishi wa abiria wakimlazimisha dereva kuendelea na safari huku wakijua kuwa basi hilo lilikuwa likihitaji matengenezo. Alisema baada ya mabishano makali dereva wa basi hilo, ambaye alinusurika katika ajali na kukimbia, aliamua kulipeleka gari hilo kituo cha Polisi kwa ajili ya ukaguzi. "Baada ya ukaguzi tuliwaamuru walipeleke gereji iliyopo eneo la Namfua mjini hapa lakini baadae tukasikia kuwa abiria walimlazimisha dereva kuendelea na safari," alisema Kamanda Kaluba na kuongeza kuwa basi hilo lilikuwa na matatizo kwenye 'kompresa' na breki. Alisema majina kamili ya waliokufa bado hayajajulikana lakini kazi inaendelea kwenye eneo hilo na majina kamili ya marehemu na majeruhi yalitarajiwa kupatikana jana baada ya kazi hiyo kumalizika. Mmoja wa majeruhi aliyenusurika kwenye ajali hiyo, Bw. Ahmad Seleman mfanyabiashara wa Mwanza, alidai kuwa mara baada ya kufika kwenye mlima huo mkali, aliona basi likiwa katika mwendo mkali. "Baadaye lilipanda kwenye kilima kikali kwa kasi na kujikuta likitumbukia kwenye korongo kubwa la mlima huu, kwa kusema kweli dereva pale hakuwa na ujanja, kwani mwendo ulikuwa mkali mno, we fikiria kupanda kwenye kile kilima si mchezo," alisema. Akizungumza kwenye eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bw. Parseko Kone, alisema alisikia kuwapo kwa ajali hiyo akiwa kwenye ziara ikabidi kuahirisha na kwenda eneo la tukio hilo saa 3 asubuhi jana. Hata hivyo, Bw. Kone alisema tayari ameagiza tingatinga kutoka kampuni ya kichina ya CGC iliyoko Isuna kwenda Sekenke kusaidia kuligeuza basi hilo ili kuopoa miili zaidi iliyokandamizwa kwenye korongo hilo. Bw. Kone alisema vifaa vinavyotumika ni duni, hivyo kazi ya kuopoa miili ni ngumu, lakini aliwapongeza vijana wa Shelui kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha miili hiyo inaopolewa yote ili kupata idadi kamili. "Kwa kweli hii ni ajali mbaya sana kutokea katika mkoa wangu, huwezi kuamini kama kuna watu wamepona kwenye ajali hii, inanisikitisha sana," alisema kwa masikitiko Mkuu huyo wa Mkoa, huku machozi yakimlengalenga. Nako Dodoma, Flora Amon anaripoti, kwamba watu hao watano walikufa papo hapo na wengine 15 kujeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea Manchali. Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Godfrey Mtey, aliwaambia waandishi wa habari hospitalini hapo jana kuwa walianza kupokea maiti na majeruhi jana saa 7.30 mchana. Dkt. Mtey alisema kati ya watu watano waliokufa ni mmoja tu ndiye aliyetambuliwa kwa jina la Bw. Seleman Hassan, mkazi wa Tanga ambapo wengine wanne majina yao bado hayajafahamika. Aliwataja walijeruhiwa kuwa ni Bw. Miraji Omar (17) mkazi wa Kiteto, Bw. Michael Kibisa mkazi wa Chinangali, Bibi Scholastica Zakaria, Bw. Jonas Jefunila wa Maili mbili, Dodoma, Bw. Zacharia Mgalo (30), mkazi wa Dar es Salaam, mtoto Erasto Peter miezi 9, wa Mpalanga na Bw. Baraka Mlumba wa Ihumwa. Wengine ni Bw. Maneno Ngomai (29), Bw. Mahomanyika, Bibi Mariam Senyo (23) mkazi wa Chadulu, Dodoma, Bw. Shaaban Mustapha (14) wa Vingunguti Dar es Salaam, Bw. Yohana Seterina (26) wa Dar es Salaam, Bw. Shaaban Bakari (10) wa Kiteto na Bw. Haruna Saimon wa Majengo, Dodoma, Bibi Feli Nemsudi (28) wa Arusha na Bw. Alikadi Emmanuel (32) wa Singida. Alisema jumla ya majeruhi 49 walifikishwa hospitalini hapo na kati yao 34 walitibiwa na kuruhusiwa na aliongeza kuwa waliolazwa wamevunjika mbavu, miguu na mikono.

Tags:

0 comments

Post a Comment