Date::25/11/2008 |
SERIKALI imesema haitarudi nyuma katika utekelezaji wa sera ya uchangiaji elimu na kwamba sasa itaangalia kwa makini vigezo vya utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwaambia wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jana kwamba serikali imefunga vyuo vikuu saba baada ya wanafunzi kugoma kuingia darasani wakishinikiza kusitishwa kwa sera hiyo na kupewa mikopo kwa asilimia 100 wakidai kuwa utaratibu wa sasa wa uchambuaji wa uwezo wa wanafunzi kuchangia, unabagua na hautoi haki kwa wanaostahili.
Katika mkutano wake na wahariri, Waziri Mkuu Pinda alisema serikali inataka kuangalia vigezo vinavyotumika kutoa mikopo kwa wanafunzi hao wa elimu ya juu.
"Jamani hebu tuambiane ukweli, hivi mnadhani kweli hata dhamira yangu mimi wakati mwingine hainitumi... kuna watoto wa wanasiasa ambao wana uwezo... na watoto wa wafanyabiashara wakubwa, mnataka wote hawa walipiwe na serikali hii hii, ni lazima tuchangie," alisema na kuongeza:
"Kama serikali inakosa fedha kwa ajili ya bajeti, tutapata wapi mabilioni mengine ya kutoa mikopo kwa asilimia 100 kwa wanafunzi wote wa vyuo. Kama serikali tulikusudia kupata Sh12.8 trilioni, lakini tukapata Sh7.2 trilioni na hii tumevutana mashati, tutapata wapi mabilioni mengine?"
Alisema kama tatizo ni mfumo unaotumika sasa kuchambua uwezo wa kiuchumi wa wanafunzi (means testing), basi wanachuo wakae na serikali wazungumze wajue namna kukabiliana nalo badala ya kugoma tu bila ukomo.
Akizungumzia mgomo wa walimu alisema suala hilo linamtia simazi kwa sababu limesababishwa na uzembe wa halmashauri mbalimbali kulimbikiza malipo ya walimu kwa muda.
Kuhusu kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi alisema kama yeye limemuudhi na limetia doa serikali, lakini akasema limetokea kwa sababu ya uvunjifu wa maadili, hivyo kuwataka wanahabari kusimamia taaluma.
Kuhusu kilimo na alisema hivi sasa serikali haitakuwa na mchezo na suala la kilimo na kwamba sasa imeshaanza kampeni ya kuboresha kilimo itakayodumu kwa miaka saba.
Kuhusu Shirika la Ndege la Tanzania(ATCL), alisema amedhamiria kulishughulikia kwa nguvu zake zote na anaamini kwamba atafanikiwa.
Alisema kuwa shirika hilo halijaishinda serikali na kwamba ameshakutana na watendaji wa shirika hilo mara mbili, kujadili jinsi ya kulifanya lifanye kazi vizuri zaidi.
Kwa upande ya Kampuni ya Reli Tanzania(TRL), Pinda alisema serikali inaangalia mkataba wa shirika hilo kwa undani, ili kujua kama una maslahi kwa Taifa au hapana.
Alisema TRL ni chombo muhimu kutokana na nauli yake kuwa chini kuliko mabasi yaendayo mikoani na inatumiwa na wananchi wengi. |
You Are Here: Home - - Serikali kutobadili Msimamo kuhusu sera
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments