Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Zitto Kabwe: Tutawabana matajiri kwenye kodi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WAZIRI Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe amesema katika Bajeti ijayo ya Serikali, atapendekeza matajiri wabanwe ili kupunguza makali ya maisha kwa Watanzania walio wengi ambao kwa sasa wanataabika kutokana na umaskini.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbarali, mjini Rujewa, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kutatua matatizo ya ugumu wa maisha yanayowakabili Watanzania.
"Tofauti ya kipato Tanzania inakuzwa na sababu mbili, moja ni matajiri kuzidi kuwa matajiri na maskini kuendelea kuwa maskini, hivyo hatua za kisera zinapaswa kuchukuliwa kuwazuia maskini kuwa maskini zaidi kwa kuwapunguzia gharama za maisha," alisema Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema).
Alisema katika Bajeti ijayo, atapendekeza kuziba pengo la kodi kwa kupandisha kodi ya kampuni kufikia asilimia 35, kuuza hisa za serikali katika kampuni za Airtel, NBC na BP hivyo kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia moja ya pato la taifa.
Alisema bei za vyakula, mafuta na usafiri ni maeneo ambayo yanachangia asilimia 60 ya matumizi ya Mtanzania na ndiyo yanayosababisha mfumuko wa bei.
"Nia ni kutoa suluhisho katika matatizo yanayolikumba taifa," alisisitiza Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Alisema mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba mfumuko wa bei unaathiri watu maskini ambao kupanda kidogo kwa bei za vitu kunawashusha kwenye umaskini zaidi.
Alisema kuwa mapendekezo hayo yatasaidia bei ya mafuta kushuka kwa Sh520 hivyo kupunguza gharama za usafirishaji na bei ya bidhaa muhimu kwa kuwa mfumuko wa bei ya bidhaa nchini inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mafuta, usafiri na vyakula.
"Kwa sasa misamaha ya kodi ni asilimia 2.5 ya pato la taifa sawa na Sh630 bilioni hivyo nitapendekeza pia kuweka msukumo maalumu kuongeza uzalishaji wa chakula ili bei zipungue," alisema.
Zitto alisema uchumi wa taifa unakuwa na hakuna atakayebisha hilo sababu umekuwa kwa asilimia 7.5, lakini akasema sekta zinazokuwa hazimhusu mwananchi wa kawaida kwani zimeshikwa na matajiri.
Alizitaja sekta hizo kuwa ni utalii, madini na mawasiliano ambazo zimekuwa kwa asilimia 20 kitu ambacho ni kasi kubwa, lakini zile ambazo zinahusu wananchi wa kawaida kama kilimo imekuwa kwa asilimia tatu ambayo haina kupanda wala kushuka na ndiyo ambayo wamo asilimia 75 ya wananchi wengi wa Tanzania. Kwa hili hii, ndiyo maana matajiri wanakuwa matajiri zaidi na maskini wanaendelea kubakia maskini."
Alisema mfumuko wa bei umekuwa mkubwa na ndiyo maana sukari iko juu; “Kwa mfano, Januari kilo ilikuwa Sh1,500 sasa hivi Mei kilo imekuwa Sh1,800 hiyo inamaanisha kwa mtu maskini kipato kimebaki palepale na matumizi yake yamepanda.”
"Sh1,000 ya Januari hainunui bidhaa zilezile kwa Mei, Januari ingeweza kununua nusu kilo ya sukari, lakini kwa sasa hivi haiwezekani, kule bungeni kambi ya upinzani ina mawaziri kivuli, tunatakiwa twende na sera mbadala kwenye bajeti hii kupunguza gharama za kodi na zile za maisha," alisema.
Alisema wanataka kupunguza bei ya kodi na petroli akihoji petroli inauzwa je Mbarali na kujibiwa kuwa ni Sh2,200 akisema hiyo inamaanisha kwamba serikali inachukua kodi ya Sh1,100, lakini akasema atapendekeza ichukue Sh500 ili bei ya petroli ishuke wananchi wafaidike.
"Kutokana na gharama za maisha, nchi yetu ni mbili katika moja. Kuna taifa la matajiri na la maskini. Watoto wa maskini wanakwenda shule za kata ambazo hazina maabara, wakati watoto wa matajiri wanaandaliwa kuwa watawala kama jinsi wazazi wao walivyo," alisema.
Alisema katika mustakabali huo, matajiri wana hospitali zao na maskini wana zao na kwamba watawaagiza mawaziri wao waende kupambana kuhakikisha gharama za maisha zinashuka. "Sisi ni mbwa wa wananchi na tutabweka kwa ajili ya wananchi ili tuweze kushusha gharama za maisha.
Serikali inamiliki asilimia 30 ya NBC tunataka tuuze asilimia 15, ili tupate Sh 15 bilioni kwa hiyo hili pamoja na mambo mengine ndiyo mambo ambayo chama kimetutuma kwenda kupambana bungeni na kuhakikisha hali ya maisha ya Mtanzania wa kawaida inakuwa katika hali nzuri," alisema.
Viongozi wa juu wa Chadema hivi sasa wako katika ziara ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakiendesha mikutano na maandamano kupinga nia ya serikali kutaka kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kujipa fursa ya kununua vifaa na mali chakavu kama mitambo ya Dowans. Pia kutaka ipunguze kodi zinazotozwa katika bidhaa mbalimbali ili kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida.

0 comments

Post a Comment