Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - UVCCM Kilimanjaro yavurugika

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MGOGORO wa kisiasa umeibuka ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro baada ya Baraza Kuu la umoja huo kutoa tamko la kutomtambua Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Paul Makonda.

Hatua hiyo ya Baraza hilo inatokana na kitendo cha Makonda kutoa kauli hivi karibuni akikikata Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwafikisha mahakamani viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi badala ya viongozi hao kuishia kujivua gamba.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM Wilaya ya Ilala, mjini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Godliving Moshi alisema Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro halimtambui Makonda kuwa mwanachana na kiongozi wa umoja huo.

Moshi alisema Makonda alifukuzwa uongozi na UVCCM tangu Desemba 30, 2009, kwa sababu mbalimbali za utovu wa nidhamu na kupungukiwa na sifa za kimaadili kwa mujibu wa Kanuni ya UVCCM Ibara ya 19 (A) kipengele cha tano.

Moshi alipotakiwa kufafanua juu ya utovu wa nidhamu uliofanywa na Makonda alisema kiongozi huyo aliiasi CCM na kuhamia chama cha upinzani ambacho hata hivyo hakuwa tayari kukitaja.

Alisema pamoja na hilo pia Makonda amekuwa akizungumza mambo mbalimbali kwenye vyombo vya habari kwa kutumia bendera ya UVCCM Wilaya ya Moshi Mjini bila idhini.

Wakati UVCCM Moshi ikitangaza kumtenga Makonda, yeye mwenyewe amesema bado ni mwanachama na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini na kwamba taarifa za kufukuzwa kwake anazisikia kwenye vyombo vya habari.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana Makonda alisema kwa mujibu wa Kanuni za UVCCM mwanachama anafukuzwa baada ya kupitia hatua nne ambazo ni pamoja na kupewa barua ya kuitwa na Kamati ya Maadili na kisha kujadiliwa na kamati hiyo kabla ya kupitisha azimio la kumpa mtuhumiwa onyo.

Alisema hatua ya pili ni kupewa barua ya onyo kali ikifuatiwa na kumvua mhusika uongozi na kama hatajirekebisha ndipo anafukuzwa uanachama, mambo ambayo alisema hayajafanyika kwake.

Alisema mgawanyiko unaojitokeza ndani ya UVCCM unasababishwa na mvutano juu ya mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na kudai kuwa yeye ameingia kwenye mapambano hayo kama Mtanzania mwenye uchungu na nchi yake bila kushinikizwa na mtu wala chama chochote.

“Mimi nimeingia kwenye mapambano na nimejiandaa…wao watatumia fedha mimi nitatumia ukweli na Watanzania ndio waamuzi kwa kuwa mapambano haya ni kati ya wavua gamba dhidi ya wavaa gamba wachache ambao wanadhani wanaweza kuendeleleza vitendo vya rushwa na
ufisadi wakiwa ndani ya CCM ,” alisema Makonda.

Alisema Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete atakuwa na kazi ngumu kama UVCCM itaendelea kutumiwa kwa ajili ya maslahi ya wachache na kuonya kuwa mgogoro ndani ya UVCCM unakipeleka chama hicho mahala pabaya kwa kuwa hivi sasa vijana wengi wameamua
kuhamia vyama vya upinzani na taswira ya umoja huo imeshikiliwa na viongozi katika ngazi za Wilaya, Mkoa na Taifa.

Aliwataka viongozi wa UVCCM kutambua kuwa katika uchaguzi uliopita Mkoa wa Kilimanjaro ulipoteza majimbo manne ambapo wapiga kura wengi walikuwa vijana hivyo kinachotakiwa si kufukuza watu uanachama bali kujirudi na kuweka mikakati dhabiti ya kupata wanachama wengi zaidi.

0 comments

Post a Comment