Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Raisi Kikwete amuweka pabaya Dk. Mwakyembe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
  NI BAADA YA KUMPA CHEO MTUHUMIWA WA RICHMOND



HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Rashid Mrindoko kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji imeanza kumgharimu kisiasa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrisson Mwakyembe.
Hali hiyo inatokana na kumbukumbu kuwa ripoti ya kamati teule ya Bunge iliyokuwa chini ya Dk. Mwakyembe ilimtaja Mrindoko na wenzake kuwa walihusika katika kuibeba kampuni ya Richamond na kuipa kazi ya kufua umeme wa dharura wakati haikustahili.
Kwa sababu ya uteuzi huo uliofanywa hivi karibuni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema ni aibu kubwa kwa Dk. Mwakyembe kuendelea kufanya kazi na Rais Jakaya Kikwete, kwani amemteua mmoja wa watuhumiwa wa kashfa ya Richmond kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji.
Chama hicho kimemtaka Dk. Mwakyembe ajiuzulu serikalini, kwani kuteuliwa kwa Mrindoko kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji ni kinyume na ripoti ya kamati teule ya Bunge kuhusu kashfa ya Richmond aliyoiongoza mwenyewe ambayo pamoja na mambo mengine iliitaka serikali imuwajibishe Mrindoko na wenzake baada ya kuonekana kuhusika katika kashfa hiyo.
Tamko hilo la CHADEMA lilitolewa jana na kada mwandamizi wa chama hicho, Fred Mpendazoe, wakati akiwahutubia wakazi wa Chunya na Tunduma katika ziara ya maandamano na mikutano ya chama hicho inayoendelea katika mikoa ya kanda ya kusini.
Mpendazoe ambaye alikuwa ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika Bunge lililopita, alisema Mrindoko wakati huo akiwa Kamishna wa Nishati alitajwa na ripoti ya kamati ya Mwakyembe kuwa mmoja wa watumishi wa umma waliohusika katika kuipa zabuni ya kufua umeme wa dharura kampuni ya Richmond Development LLC ya nchini Marekani, wakati haikustahili kupewa zabuni hiyo.
“Ripoti ya kamati ya Mwakyembe ilitaka Mrindoko na wenzake wawajibishwe kwa ufisadi waliohusishwa nao katika zabuni ya Richmond, lakini badala ya kumuwajibisha juzi Rais Kikwete amempa cheo cha kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji.
“Nilidhani Mwakyembe angejiuzulu lakini bila aibu ameendelea kubaki ndani ya serikali huku akijua fika kuwa Rais Kikwete amemdhalilisha kwa kumpa cheo Mrindoko ambaye yeye alitaka awajibishwe,” aliseema.
Alisema uteuzi huo unazidi kulipa taifa ushahidi jinsi Rais Kikwete na chama chake wanavyoendelea kukumbatia ufisadi licha ya kujidai kujivua gamba hivi karibuni.
“Mtuhumiwa wa ufisadi aliyepaswa kuchukuliwa hatua za nidhamu na za kisheria leo amepewa cheo kipya cha kuwa Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji. Ni rahisi kwa ngamia kuingia kwenye tundu la sindano kuliko CCM kuachana na mafisadi. Namtaka Mwakyembe ajiuzulu kama anajiheshimu,” alisema Mpendazoe na kushangiliwa.
Alibainisha kama Mwakyembe hatajiuzulu basi CHADEMA itaendelea kumtangaza kuwa ni kiongozi mwenye uchu wa madaraka na asiye na msimamo katika kusimamia mambo yenye manufaa kwa taifa.
“Kama ataendelea kubaki serikalini basi ile ripoti ya kamati yake kuhusu Richmond itakuwa imepoteza umuhimu. Kiongozi asiye na uchu wa madaraka hawezi kuendelea kufanya kazi na serikali inayokumbatia mafisadi ambao yeye mwenyewe alishiriki kuwachunguza na kutaka wachukuliwe hatua. Mwakyembe anapaswa kujiuzulu,” alisisitiza Mpendazoe.
Katika hatua nyingine, CHADEMA imetamba kupata mafanikio makubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana licha ya kile kilichoelezwa kuwa matokeo ya uchaguzi huo, yalichakachukuliwa.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, akiwashukuru wakazi wa mkoa wa Mbeya alisema kwa hesabu za jumla chama hicho kimekuwa na kuimarika kwa asilimia 400 kutoka mwaka 2005 hadi 2010.
Akifafanua ukuaji huo, Zitto alisema mwaka 2005 chama hicho kilipata wabunge 11 na madiwani 101, lakini katika uchaguzi wa mwaka jana walifanikiwa kupata wabunge 48 na madiwani 466 nchi nzima.
“Tunawashukuru sana wananchi wa Mbeya na Watanzania wote kwa kutuunga mkono katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Kazi tunayoendelea nayo sasa ni kuwatetea na kuwapigania…ni kuhakikisha kodi yenu inatumika kuwaletea maendeleo.
“Tunashukuru zaidi kwa kura nyingi za urais mlizompa Dk. Willbrod Slaa, yeye ndiye aliyeshinda urais lakini katika baadhi ya maeneo wananchi hamkujipanga vema tukapokonywa urais na ubunge. Sasa tumeanza kazi ya kuzidi kukiimarisha chama chetu kwa ajili ya kuchukua dola mwaka 2015,” alisema Zitto na kushangiliwa.
Wakati huohuo Joseph Senga kutoka Chunya anaripoti kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, amewataka maaskofu kutohubiri amani na badala yake wahubiri kwanza kupatikana kwa haki.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kanga, wilayani Chunya, jana, Dk. Slaa alieleza kushangazwa kwake na viongozi hao wa dini ambao wanahubiri sana suala la amani ambalo ni tunda la haki.
“Nawaomba hawa maaskofu wanisamehe tu, kuhubiri amani wakati hakuna haki haitoshi,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kuwa maaskofu wanashutumu vyama vya siasa vinaharibu amani wakati amani ni zao la haki.
Amesema baadhi ya maaskofu na masheikh wamekuwa wakiunga mkono yanayotolewa na viongozi mbalimbali ambao wao wana maslahi katika hilo.
“Yesu alihubiri haki kwanza, na hawa wanatakiwa kuzingatia hilo kwani amani haiwezi kuwepo bila haki,” alisema.

0 comments

Post a Comment